UKOSEFU WA FEDHA CHANZO CHA WANACHAMA WASIOONA KUTOFANYA VIKAO
>>Chama cha Wasioona mkoa wa Mara hakina ofisi ya mkoa na wilaya.
>>Chajikongoja kufanya shughuli za Chama vikiwemo vikao kutokana na ukosefu wa fedha.
>>Wanachama walazimika kujichanga fedha za nauli, chakula kufanya vikao vya uchaguzi wa viongozi.
>>Wasema Serikali iko mbali nao.
Na Dinna Maningo, Tarime
CHAMA cha Wasioona Tanzania (TLB) mkoa wa Mara kinakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa fedha za kuendesha shughuli za chama vikiwemo vikao vya uchaguzi jambo linalosababisha kutofikia malengo.
Ukosefu wa fedha umetajwa kuwa ni chanzo kikubwa kinachosababisha Wasioona kutojiunga na chama kwani waliopo kwenye chama hicho wanalazimika kutumia fedha zao kwa ajili ya usafiri, chakula na mahitaji mengine wanaposhiriki vikao.
Vikao hivyo ni pamoja na vikao vya kiutendaji, uchaguzi, na kwamba wakati mwingine vikao havifanyiki kutokana na ukosefu wa fedha za kuendesha vikao.
Pia Chama hicho hakina ofisi ya mkoa wala ofisi katika Wilaya yoyote mkoani Mara na kwamba wanapotaka kukutana wanalazimika kuomba majengo ya shule ili kufanya vikao vyao.
Viongozi wa Chama hicho mkoa wa Mara wanaiomba Serikali, Taasisi, Mashirika na wadau mbalimbali kujitokeza kuwaunga mkono kuwasaidia fedha ili ziwawezeshe kufanikisha shughuli za uendeshaji wa Chama na shughuli za kiuchumi.
Wakizungumza wakati wa uchaguzi wa Viongozi wa Chama cha Wasioona wilaya ya Tarime, uliofanyika Septemba, 29,2023 katika shule ya msingi Magufuli, Mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Mara, Nyamlanga John Lwakatare amesema ukosefu wa fedha unakididimiza chama hicho.
"Tumekutana hapa kufanya uchaguzi ngazi ya wilaya hapa Tarime, lakini waliojitokeza kushiriki ni wachache hatuzidi kumi. Watu hawakufika kwasababu ya kukosa nauli na watu wa kuwaongoza kuja kwenye kikao cha uchaguzi kwakuwa hakuna nauli.
"Hata hiki kikao sisi walemavu tumejichanga wenyewe kwa gharama zetu, Serikali imetutelekeza, ilitakiwa watupatie mafungu, ilitakiwa vikao tuwezeshwe fedha, mbona watu wazima wasio na ulemavu wanawezeshwa lakini wenye ulemavu hatusaidiwi wanatuacha tunahangaika wenyewe" amesema.
Mwenyekiti huyo amesema kuwa wamekuwa wakiomba ufadhili wa fedha Serikalini hususani halmashauri kwa ajili ya kuendesha vikao lakini hawawezeshwi.
"Halmashauri zitoe fedha kwa haya makundi ya walemavu angalau hata laki mbili kwa mwezi za uendeshaji wa ofisi. Walemavu wasioona wengi wao ni wa maisha ya chini na vipato vyao ni vidogo, alafu huyo huyo ajilipie naulia kushiriki vikao.
"Hata huu uchaguzi tumesafiri kwa nauli zetu na wengine wanatoka maeneo ya mbali, mfano Bhoke Orindo anatoka Nyamongo ili afike kushiriki kikao cha wilaya Tarime mjini nauli kwenda na kurudi ni Tsh.14,000 bado chakula, bado kuna baadhi mpaka waongozane na mtu wa kuwaongoza" amesema Nyamlanga.
Mweka Hazina wa TLB mkoa wa Mara, David Siriwa Daniel amesema " Hatuna ofisi ya mkoa wala ofisi katika wilaya yoyote, tukitaka kufanya vikao tunaomba shule kama tulivyofanya kikao chetu hapa shule ya msingi Magufuli.
"Hakuna wa kutuwezesha fedha za kuendesha vikao, tunachangishana wenyewe, wasioona wengi hawana vipato na walivyonavyo ni vidogo visivyoendana na mahitaji, Serikali kutowasaidia walemavu wasioona ni chanzo cha kukwamisha jitihada za walemavu" amesema .
Ameongeza" Sisi walemavu tunadharauliwa, ukienda kuomba msaada hupati lakini mtu mzima asiye mlemavu yeye akiomba msaada anasaidiwa, na ukiomba msaada hupewi wakidhani unaomba pesa kwa shida zako binafsi. Serikali itusaidie fedha ngazi za mkoa na Wilaya tunateseka kuendesha Chama" amesema David.
Katibu wa TLB Wilaya ya Tarime ambaye pia ni Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya watu wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) Halmashauri ya mji Tarime, Sara Marwa amesema changamoto nyingine ni ukosefu wa fimbo nyeupe kwa wasioona hivyo wanaomba msaada wa fimbo nyeupe lakini pia kufadhiliwa fedha kwa ajili ya kushiriki maadhimisho ya siku ya fimbo nyeupe.
Katibu wa Shirikisho la Vyama vya watu wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) Halmashauri ya mji Tarime, ambaye pia ni Mwalimu wa shule ya msingi Magufuli ya wanafunzi wenye mahitaji maalum, Mekaus Maingu ameiomba Serikali kuwa Karibu na vyama vya walemavu.
"Tuliwahi kuandika bajeti ya walemavu Milioni 30 tukapeleka halmashauri, mwisho wa siku wakasema hakuna fedha kwamba bajeti haikupita.
"Watu wenye ulemavu tunatengwa sana hata vikao vya WDC, DCC walemavu hatualikwi kushiriki, tuna changamoto nyingi zikiwemo za ukosefu wa vifaa kwa Wanachama wa vyama vya walemavu" amesema.
Mekaus amesema endapo Serikali itafadhili fedha za usafiri na za kuendesha vikao kwa walemavu pamoja na kutatua changamoto zao itakuwa imesaidia jitihada chanya za watu wenye Ulemavu na walemavu watapata maendeleo na kuinuka kiuchumi.
Rejea
>>Desemba, 03, 2022 Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu ilizindua mwongozo wa utekelezaji, ujumuishwaji na uimarishaji wa huduma kwa watu wenye ulemavu Tanzania.
Uzinduzi huo ulifanyika wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya watu wenye Ulemavu Duniani ambapo Kitaifa ulifanyika Jijini Arusha.
Madhumuni ya Mwongozo huo ilielezwa kuwa ni kutoa mwelekeo, miongozo na maelekezo kwa viongozi na watendaji wa Serikali pamoja na wadau wengine katika kuchochea maendeleo na ustawi wa watu wenye Ulemavu kwa kuongeza hatua za ujumuishwaji na kutoa huduma bora kwao ili kuwawezesha kukabiliana na changamoto za kimaisha zitokanazo na zinazochochewa na ulemavu walionao.
Wakati huohuo, Chama hicho cha Wasioona kimefanya uchaguzi wa viongozi wa Wilaya ya Tarime ambapo Mwenyekiti ni Mseti Chacha, Katibu Sara Marwa, Mweka Hazina Bhoke Orindo pamoja na wajumbe wanne.
Mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Mara, Nyamlanga John Lwakatare amesema mkakati wao ni kuhakikisha wanaongeza idadi ya wanachama kwa kile alichoeleza kuwa huko vijijini kuna watu wasioona hivyo ni vyema wakatambulika.
Ameongeza kuwa watakapotambulika wataunda vikundi ili wapate mikopo wajiinue kiuchumi badala ya kuwa tegemezi.
Post a Comment