MADEREVA 44 TARIME RORYA WAHITIMU MAFUNZO YA UDEREVA MAHIRI
Na ASP Richard Minja, Tarime Rorya
MADEREVA wapatao 44 kutoka mkoa wa Polisi Tarime Rorya mkoani Mara, wamehitimu mafunzo ya udereva mahiri yaliyotolewa na chuo cha udereva Tarime Community Driving shool kwakushirikiana na chuo cha Ufundi Arusha.
Mafunzo hayo yamehirimishwa Septemba, 08, 09, 2023 ambao wahitimu wa mafunzo hayo watapewa leseni madaraja C,C1,C2,C3 na E.
Akizungumza katika ufungaji wa mafunzo hayo Mhandisi Mukumba toka Chuo cha Ufundi Arusha amesema kuwa mafunzo hayo yalizingatia mada kuu mbalimbali ikiwemo Uadilifu wa dereva, udereva wa kujihami, ukaguzi wa vyombo vya usafiri, nadharia ya matairi, sheria za usalama barabarani, huduma ya kwanza na huduma ya uzimaji wa moto.
Mhandisi Mukumba amemweleza aliyekuwa mgeni rasmi ambaye ni Kaimu Kamanda wa Mkoa wa Polisi Tarime Rorya ACP Ame Anoqie kuwa mafunzo hayo yamefanikiwa kwa kiwango kikubwa katika nadharia na vitendo.
Ameishukuru ofisi ya Mkuu wa Kikosi cha usalama barabarani Mkoa wa Tarime Rorya kupitia kwa Kamanda wa Polisi mkoa kwa ushirikiano mzuri wa kipindi chote cha mafunzo hayo.
Akizungumza katika ufungaji wa mafunzo hayo ACP Ame Anoqie amesema kuwa mafunzo hayo ya umahiri wa kuendesha vyombo vya usafiri wa kujihami ni muhimu kwa madereva wote na kwamba yatapunguza ajali zinazozuilika lakini pia kulipunguzia mzigo Jeshi la Polisi kitengo cha Usalama barabarani.
Pia amewapongeza wahitimu wote 44 kwa kujitokeza na kuhudhuria mafunzo hayo na kuwataka kuwa mabalozi kwa madereva wengine kujifunza na pia kuwaelimisha wale wasiofuata sheria na taratibu za udereva mahiri kuzifuata ipasavyo.
Naye mwakilishi wa wahitimu hao ameomba mafunzo hayo kuwa endelevu na pia ofisi ya Mkuu wa Usalama barabani kuhakikisha maeneo ya maegesho kusimamiwa vizuri na kuepusha msongamano wa vyombo vya usafiri ili kuepusha ajali.
ACP Ame Anoqie ametoa wito kwa madereva wote kutii sheria ya usalama barabarani na pia kuongeza ujuzi na maarifa kutoka katika vyuo vinavyotambulika na Serikali .
Pia amewataka madereva wote kuzingatia kauli mbiu isemayo, 'Tanzania Bila ajali inawezekana, Tarime Rorya bila ajali inawezekana'.
Awali chuo cha Tarime driving school kilichopata usajili wake 2013 kilikuwa kinatoa mafunzo kwa madereva wa awali kwa nadharia na vitendo ambapo 2023 kimeanza ushirikiano na Chuo cha Ufundi Arusha kwa ajili ya udereva wa magari ya mizigo na abiria.
Mafunzo hayo ya awamu ya kwanza yalianza 30.08.2023 yaliendeshwa na wakufunzi toka Jeshi la Polisi, Jeshi la Zima moto na uokoaji, Tarime community Driving school na Chuo cha Ufundi Arusha.
Imeelezwa kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya mafunzo yanayoendeshwa na chuo cha Ufundi Arusha katika Mikoa mbalimbali hapa nchini ili kuwajengea uwezo madereva wawapo barabarani.
Post a Comment