TANROADS NA MPANGO WA KUFUNGA TAA ZA KUONGOZEA MAGARI BARABARANI KUPUNGUZA MSONGAMANO
Na Gustafu Haule, Pwani
SERIKALI kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Pwani wameanza mpango maalum wa kufunga taa za kuongozea magari katika barabara ya Tanzania - Zambia( TAZAM) ikiwa ni sehemu ya kupunguza msongamano wa magari katika barabara hiyo.
Taa hizo tayari zimeanza kufungwa katika eneo la kwa Mathias katika Halmashauri ya Mji wa Kibaha pamoja na eneo la Mlandizi katika Halmashauri ya Kibaha Vijijini maeneo ambayo yanatajwa kuwa na msongamano mkubwa wa magari yanayosababisha foleni kubwa.
Aidha utekelezaji wa mpango huo utahusisha barabara inayounganisha Tanzania na Zambia kwakuwa ndiyo yenye magari mengi yanayosafirisha bidhaa mbalimbali za kibiashara zinazochangia uchumi wa nchi hizo.
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Pwani Mhandisi Baraka Mwambage amesema katika Mpango huo taa za kuongoza magari zitawekwa katika makutano ya kwa Mathias, kwa Mfipa na Mlandizi lakini baadhi ya maeneo utekelezaji huo umeshafanyika.
Meneja wa TANROADS Mkoa wa Pwani Mhandisi Baraka Mwambage"Serikali ya awamu ya Sita chini Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan inaendelea na utatuzi wa changamoto za barabarani na kwa upande wa Mkoa wa Pwani tayari tumeanza na mpango wa kufunga taa za kuongozea magari ili kupunguza msongamano wa magari barabrani,"amesema Mwambage
Aidha Mwambage ameongeza kuwa kwasasa tayari wameanza kufunga taa hizo katika makutano ya eneo la kwa Mathias kazi ambayo imefanyika tangu Septemba 7 usiku na kisha eneo la Mlandizi.
Mwambage ameeleza kwamba ukarabati wa barabara ya zamani ya Morogoro na njia za mchepuko(Diversions) zitahimarishwa na kuwekewa alama za barabarani ili kusudi ziweze kusaidia katika dharula mbalimbali na hivyo kuondoa changamoto za foleni.
Amesema mbali na kukarabati barabara ya zamani ya Morogoro lakini upo mpango mkubwa wa kudumu wa kujenga barabara ya Kibaha -Chalinze -Morogoro itakayokuwa na njia za haraka(Expressway) .
Barabara hiyo yenye kilomita 205 itajengwa kwa kushirikisha sekta binafsi (Public Private Partnership,P3 na utekelezaji wa mradi huo upo katika hatua za manunuzi na kwamba baada ya kukamilika mtumiaji anaweza kutumia lisaa limoja kutoka Kibaha mpaka Morogoro.
Hatahivyo Mwambage amewaomba wananchi kuendelea kushirikiana na Tanroad ikiwemo katika kutunza miundombinu inayowekwa barabarani kwa ajili ya kuhakikisha usalama wa barabara unazidi kuimarika.
Post a Comment