HEADER AD

HEADER AD

MBUNGE KOKA AKABIDHI MATANKI YA MAJI SOKO LA LOLIONDO

Na Gustafu Haule, Pwani

MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka (CCM)amefanya ziara katika soko la Loliondo lililopo katika Kata ya Tangini kwa ajili ya kujua changamoto zinazowakabili wafanyabiashara pamoja  na kutekeleza aadi alizozitoa kwa wafanyabiashara wa soko hilo.

Koka,amefanya ziara hiyo sokoni hapo  Septemba 11 mwaka huu akiwa ameambatana na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson Saimon, mwenyekiti wa halmashauri ya Kibaha Mjini Musa Ndomba pamoja na viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali.

Aidha katika ziara hiyo Koka amekabidhi matanki matatu ya kuhifadhia maji katika Soko hilo ambapo Mamalishe wamepata tanki la lita 5000,wauzaji wa Kuku lita 2000, upande wa mazao mchanganyiko na matunda wakipata tanki la lita 2000 huku banda la mchele wakipata Television mbili za kisasa.



Akizungumza katika mkutano wa pamoja na wafanyabiashara wa soko hilo Koka, amesema kuwa pamoja na kutekeleza aadi yake lakini lengo la ziara hiyo ni kukagua maendeleo ya soko hilo pamoja na kutambua changamoto zinazowakabili wafanyabiashara hao.

Amesema kuwa lengo lake ni kutaka kuendelea kuboresha zaidi soko hilo kwa kutatua changamoto za wafanyabiashara hao ili waweze kufanya biashara zao katika mazingira mazuri na yenye ubora wa kuwavutia wateja wao.

      Mbunge Kibaha Mjini Silvestry Koka, akikabidhi television kwa wafanyabiashara wa soko la Loliondo Septemba 11 mwaka huu.

"Mkuu wa Wilaya alikuja hapa kufanya ziara na alikuta changamoto ya vifaa vya kuhifadhia maji pale yanapokatika lakini aliwasiliana namimi na nikachukua maamuzi ya haraka kuja kutatua changamoto yenu na leo nimekuja kuwaletea matanki matatu pamoja na kuwaletea TV mbili wafanyabiashara wa banda la mchele,"amesema Koka

Koka ameongeza kuwa ofisi ya Mbunge,ofisi ya Mkuu wa Wilaya pamoja na Halmashauri ni mapacha kwani wanafanyakazi moja ya kuhudumia wananchi ndio maana changamoto zilizopo sokoni hapo zinafanyiwa kazi kwa haraka. 

Amesema anatambua wafanyabiashara wa Loliondo wanachangamoto nyingi ikiwemo sehemu ya wauzaji wamatunda kukosa paa hali ambayo wanakuwa wakati mgumu wakati mvua ikinyesha lakini banda la mazao mchanganyiko na banda la mchele paa zake zimeharibika na zinapitisha maji pamoja na changamoto za umeme.

    Mbunge wa Kibaha Mjini Silvestry Koka akiwa katika Soko la Loliondo Kibaha Mjini Septemba 11 mwaka huu.

Amesema changamoto zote zinafanyiwa kazi kupitia ofisi ya Mbunge na Halmashauri ya Mji ambapo mpaka sasa tayari ipo mipango madhubuti ya kuboresha soko hilo na kipindi cha Septemba na Desemba yapo baadhi ya maeneo tayari yatakuwa yamekamilika.

"Nimefanya ziara hapa sokoni lakini nimeona changamoto nyingi na niseme ,ndani ya miezi miwili marekebisho ya paa yatafanyika kwa kuweka mabati mapya yenye kuingiza mwanga katika Soko la mchanyiko na mchele na soko la matunda Halmashauri itajenga paa ifikapo Disemba mwaka huu,"amesema Koka

Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson Saimon,amesema kuwa changamoto zilizokuwepo sokoni hapo zitafanyiwa kazi na kwamba kwasasa wanatafuta zaidi ya milioni 200 kwa ajili ya kukarabati miundombinu ya soko hilo.



Saimoni ,amesema ofisi yake na ofisi ya Mbunge kupitia Halmashauri ya Kibaha Mjini inadhamira ya dhati katika kuboresha soko hilo huku akimshukuru Mbunge Koka kwa kuchukua hatua ya kutatua changamoto ya maji sokoni hapo.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Halmashauri ya Kibaha Mjini Musa Ndomba,ameahidi kutatua changamoto za soko hilo kwa urahisi lakini kwasasa wapo katika mipango ya kutenga pesa ambapo katika robo ya pili ya mwaka fedha za kukarabati soko hilo zitakuwa zimepatikana .

Ndomba amesema kuwa kukamilika kwa soko hilo kutasaidia Halmashauri kukusanya ushuru ambao utaongeza kipato lakini wafanyabiashara watakuwa katika mazingira salama na bora .

  Mwenyekiti wa soko la Loliondo Mohamed Mnembwe, amemshukuru mbunge huyo kwa kutekeleza aadi zake huku akiomba Halmashauri na mbunge kuendelea kuzitafutia majibu changamoto zilizopo.

Hata hivyo mmoja wa wafanyabiashara wa soko hilo Saida Hassan,amesema kuwa kazi iliyofanywa na mbunge imeleta matumaini kwa wafanyabiashara wa soko la Loliondo na kwamba wataendelea kutoa ushirikiano kwake ili kuhakikisha changamoto zao zinafanyiwa kazi.


No comments