WARATIBU TASAF WATAKIWA KUWAONDOA WALIOFANIKIWA NA KUWAINGIZA KWENYE MPANGO WENYE HALI DUNI
Na Gustafu Haule, Pwani
MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge amewataka waratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) waliopo katika Halmashauri za Mkoa huo kuhakikisha wanafanya ufuatiliaji kwa wanufaika wa mpango huo ili kuwatoa ambao tayari wamefanikiwa na kuwaingiza katika mpango wale ambao wana hali duni zaidi.
Aidha,amewaagiza Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Mkoa huo kuendelea kutoa kipaumbele katika kutokomeza umasikini kwenye maeneo yao na kusimamia mpango wa Tasaf kwakuwa ndio mpango pekee wa kumtoa Mtanzania kwenye wimbi la umaskini.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge akifungua kikao kazi cha mwaka cha kujadili shughuli za utekelezaji wa mpango wa kunusuru Kaya maskini kupitia (Tasaf )awamu ya pili Septemba 15.
Kunenge ametoa kauli hiyo wakati akifungua kikao kazi cha mwaka cha kujadili utekelezaji wa shughuli za kunusuru Kaya maskini kupitia mpango wa Tasaf 3 wa awamu ya pili uliokwenda sambamba na kutoa tuzo kwa Halmashauri zilizofanya vizuri.
Amesema kukiwa na ufuatiliaji itasaidia kujua changamoto zilizopo na hivyo kuondoa vikwazo ambavyo kwa namna moja au nyingine zinasababisha baadhi ya maeneo mradi kusuasua.
"Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi kwa ajili ya kuboresha mfuko wa TASAF kwa lengo la kuondoa umasikini hivyo lazima kila mratibu,Wakurugenzi na Wakuu wa Wilaya kuwajibika katika nafasi zao kwa ajili ya kuhakikisha Kaya maskini zinanufaika na mpango huo," amesema Kunenge
" Nawasisitiza Wakuu wa Wilaya hili ni eneo muhimu ambalo linapaswa tulisimamie vizuri TASAF ni kipaumbele cha Rais na vipaumbele vyetu tunavipata kutokana na vipaumbele vya nchi namshukuru Rais kwa kuendelea kugusa maisha ya kaya masikini" amesisitiza.
Mratibu wa TASAF mkoa wa Pwani Roseline Kimaro amesema mafanikio yanayopatikana Pwani katika utekelezaji wa miradi inatokana na ushirikiano uliopo baina ya Mkoa na waratibu wa Tasaf katika Halmashauri mbalimbali.
Kimaro,amesema kuwa kwasasa wanafunzi 52 wapo vyuo vikuu ambao wanasoma kupitia mpango huo na walianza kunufaika kuanzia shule za msingi baada ya wazazi wao kuingizwa kwenye mradi.
Aidha,Kimaro amesema kwasasa amepokea changamoto zote zilizojitokeza katika kikao hicho na kwamba watakwenda kuzifanyiakazi changamoto hizo ili kusudi kuweka urahisi wa jamii iliyopo katika mfuko huo kufikiwa kirahisi.
Hata hivyo Katika kikao hicho Kunenge amekabidhi tuzo kwa Halmashauri zilizofanya vizuri kwenye miradi ya TASAF sambamba na afisa kilimo Kata ya Janga Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Mugisha Vicent ambaye amefanya vizuri kwenye mradi wa kilimo cha Mjini.
Post a Comment