MWENYEKITI UWT TAIFA AAGIZA KUZIBWA NYUFA KITUO CHA AFYA SHISHIYU
Na Samwel Mwanga, Maswa
MWENYEKITI wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania(UWT)Taifa,Mary Chatanda amemuagiza Mhandisi wa Majengo wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu,Mhandisi Saimon Salum kuhakikisha nyufa zote ambazo zipo kwenye baadhi ya Majengo katika Kituo Cha Afya Shishiyu wilayani humo zinazibwa.
Chatanda ametoa kauli hiyo Septemba, 17, 2023 mara baada ya kutembelea ujenzi wa wodi ya Wazazi na chumba cha upasuaji katika kituo hicho.
Amesema kuwa Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Rais,Dkt Samia Suluhu Hassan imetoa kiasi cha fedha zaidi ya Tsh. Milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho kwa ajili kutoa huduma za Afya hasa kwa wakinamama wajawazito na watoto.
Amesema kuwa ni vizuri majengo hayo ya serikali yakajengwa vizuri na nyufa zote ambazo zimeonekana kwenye jengo hilo ni lazima zizibwe na hivyo kumtaka Mhandisi huyo kuhakikisha anawasimamia vizuri mafundi wanaowapa kazi za ujenzi wa majengo hayo.
"Hili tatizo la nyufa kwenye hili jengo tulilokagua ujenzi wake ambao unaendelea wa chumba cha upasuaji na Wodi ya Wazazi huenda umetokana na matofali kutomwagiliwa maji ya kutosha baada ya kufyatuliwa.
" Hivyo nikuagize Mhandisi wa halmashauri hakikisha nyufa hizo zinazibwa na katika haya majengo majengo ya serikali ambayo tunatumia mafundi wazawa(local fundi)ni vizuri mkawasimamia ili wafanye kazi kwa ufanisi"amesema.
Mkuu wa wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge amesema kuwa Kijiji hicho kilikuwa na zahanati lakini serikali kwa kutambua mahitaji makubwa ya Afya katika eneo hilo na Kata ya Shishiyu imeamua kujenga kituo cha Afya na kumhakikishia kuwa agizo ambalo amelitoa atalisimamia kwa ajili ya utekekezaji.
"Hapa kulikuwa na zahanati ambayo ilijengwa mwaka 1965 na ilikuwa inahudumia wananchi wa Vijiji vinne vya Kata ya Shishiyu ambavyo ni Shishiyu,Kakola,Mwaliga na Mwatumbe vyenye wakazi 12,492 kutoka na zahanati hiyo kuzidiwa na idadi kubwa ya wagonjwa serikali ilileta fedha zaidi ya Shilingi Milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha Afya Cha Shishiyu hivyo tunaishukuru sana serikali kwa ujenzi huu,"amesema.
Awali akitoa taarifa ya ujenzi wa kituo hicho,Mganga Mfawidhi wa kituo Cha Afya Shishiyu,Dk Ali Kitambulio amesema kuwa ujenzi huo umefanyika kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza imehusisha Jengo la Wagonjwa wa nje,(OPD),Maabara na kichomea taka ambapo yote yamekamilika kwa gharama ya Tsh 250.
Amesema kuwa awamu ya pili imehusisha ujenzi wa jengo la Wodi ya Wazazi lililounganishwa na chumba cha upasuaji ambapo yako asilimia 86 ya utekekezaji na tayari Shilingi Milioni 250 zimeshapokelewa kwa ajili ya kukamilisha ujenzi huo.
Dk Kitambulio amesema kuwa kukamilika kwa ujenzi huo kutaboresha huduma za upasuaji wa dharula kwa wakinamama wanaopata uchungu pingamizi,huduma ya Maabara pamoja na Huduma ya damu salama ambapo awali walikuwa wakismbuka kwenda kupata huduma hizo katika Hospitali ya wilaya iliyopo Umbali wa kilomita 42.
Aidha amesema kuwa pia kukamilika kwa ujenzi wa kituo hicho utapunguza vifo vya mama na watoto chini ya umri wa miaka mitano.
"Tunaishukuru sana Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Samia Suluhu kwa kutuwesha kupata Mradi huu pamoja na kutuletea Tsh.Milioni 112.5 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba kwenye kituo chetu cha Afya "amesema.
Katika hatua nyingine mwenyekiti wa UWT Taifa, Mary Chatanda ametembelea ujenzi wa shule mpya ya msingi ya Majengo iliyoko katika kijiji hicho ambayo imejengwa na serikali kwa gharama ya Tsh Milioni 348.5 kutokana na shule ya msingi Shishiyu kuwa na idadi kubwa ya Wanafunzi.
Katika Ukaguzi huo,Chatanda ameridhishwa na ujenzi wa shule hiyo na kumtaka Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge kuhakikisha darasa la Elimu ya Awali katika shule hiyo linawekewa uzio ili kuhakikisha wanakuwa kwenye ulinzi mzuri wanapokuwa shuleni hapo.
Post a Comment