UWT YAWASHAURI VIJANA KUTUMIA MAFUNZO YA VYUO VYA VETA KUJIAJIRI
Na Samwel Mwanga, Meatu
VIJANA kote nchini wametakiwa kuvitumia Vyuo vya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi(VETA)kwa ajili ya kupata mafunzo ili waweze kujiajiri wao wenyewe kuliko kusubiri ajira serikalini.
Hayo yameelezwa leo na Makamu Mwenyekiti UWT Taifa, Zainabu Shomari mara baada ya kukagua ujenzi wa Chuo cha VETA katika Kijiji cha Bulyashi wilaya ya Meatu mkoa wa Simiyu.
Makamu Mwenyekiti UWT Taifa,Zainab Shomari(aliyeko kati),Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu,Shemsha Mohamed (wa kwanza kushoto)na Mbunge wa Vijana CCM mkoa wa Simiyu,Lucy Sabu(wa kwanza kulia)wakisikiliza taarifa ya ujenzi wa Chuo Cha VETA wilaya ya Meatu mkoa wa Simiyu.
Amesema kuwa ujenzi wa chuo hicho ni utekekezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi(CCM)ya mwaka 2020 ambayo imeeleza kuwa vitajengwa Vyuo hivyo kwa kila wilaya.
Makamu Mwenyekiti huyo ambaye yuko kwenye ziara ya kikazi katika mkoa wa Simiyu amesema kuwa mafunzo yanayotolewa kwenye Vyuo hivyo yanawaandaa vijana kupata mafunzo Stadi ambayo yatawafanya waweze kujiajiri wenyewe.
"Leo tupo kwenye utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020 na hivi Vyuo vimelenga kuwanufaisha vijana ili waweze kupata mafunzo ya fani mbalimbali ambayo yatawasaidia ili waweze kujiajiri wao wenyewe kuliko kutegemea kupata Ajira serikali ambazo huwa ni chache,"
"Hivi vyuo vya VETA pia vinaweza kuwasaidia watu wazima kuweza kujiendeleza katika fani mbalimbali na kuongeza ujuzi wao katika fani mbalimbali na kupata vyeti ambavyo vitawasaidia katika utendaji kazi wa majukumu yao,"amesema.
Pia amemtaka msimamizi wa ujenzi wa chuo hicho ambaye ni Mdhibiti Mkuu wa ubora wa shule wilaya ya Meatu kuhakikisha ujenzi huo unakamilika Mwezi Januari mwakani ili chuo kianze kutoa mafunzo ya fani mbalimbali.
Ujenzi wa nyumba ya Mkuu wa Chuo Cha VETA wilaya ya Meatu mkoa wa Simiyu unaendelea katika katika Kijiji Cha Bulyashi.
Naye Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu,Shemsha Mohamed amesema kuwa chama hicho katika mkoa huo kitaendelea kufuatilia kwa karibu sana miradi yote ya maendeleo inayotekeleza na serikali kupitia fedha za walipakodi.
Amesema kuwa Rais,Dkt Samia Suluhu ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa CCM Taifa ametoa fedha nyingi kwa ajili ya miradi mbalimbali ya serikali katika mkoa huo ukiwemo Mradi wa ujenzi wa chuo hicho katika wilaya ya Meatu.
"Chama Cha Mapinduzi sisi ndilo jicho la Rais ili kuhakikisha fedha zote zinazoletwa na serikali ambayo Iko chini ya CCM katika miradi mbalimbali ya maendeleo katika mkoa wetu hivyo tutaendelea kufuatilia kwa ukaribu miradi yote ili iweze kukamilika kwa kiwango na kukidhi matakwa yaliyokusudiwa na Rais Dkt Samia Suluhu,"amesema.
Awali Msimamizi wa Ujenzi wa Mradi huo,Mthibiti Mkuu wa Ubora wa SHULE wilaya ya Meatu,Faustina Lagwen akisoma taarifa ya ujenzi wa chuo hicho amesema kuwa zaidi ya kiasi cha Bilioni 1.4 kitatumika katika ujenzi wa chuo Cha VETA Meatu.
Msimamizi wa Ujenzi wa Chuo Cha VETA wilaya ya Meatu,Faustina Lagwen(wa kwanza kulia)akisoma taarifa ya utekelezaji wa ujenzi wa chuo hicho kwa Makamu Mwenyekiti wa UWT Taifa,Zainab Shomari(wa pili kushoto)alipotembelea eneo la ujenzi kwenye kijiji Cha Bulyashi.
Amesema kuwa Miundombinu itakayojengwa katika awamu ya kwanza ni pamoja na karakana ya Mapishi na ushonaji,karakana ya useremala, uashi na karakana ya bomba na umeme.
Miundombinu mingine ni pamoja na jengo la Utawala,jengo la madarasa lenye chumba cha TEHAMA,Mifumo ya Maji safi na Maji taka,Nyumba ya Mkuu wa Chuo,jengo la kupokelea umeme na Ofisi ya mlinzi.
Amesema kuwa ujenzi huo unaofanywa na mafundi wazawa(Local Fundis) na hadi sasa ujenzi unaendelea na kiasi Shilingi Milioni 353.1 zimepokelewa na hadi sasa Tsh. Milioni 252.4 zimetumika katika ujenzi.
Mwenyekiti wa UWT Taifa,Zainabu Shomari(mwenye kofia nyeupe)akisoma taarifa ya ujenzi wa chuo Cha VETA katika Kijiji Cha Bulyashi wilaya ya Meatu mkoa wa Simiyu
Amesema kuwa moja ya manufaa ya mradi huo utakapokamilika utatoa fursa kwa vijana wengi na watu wazima kupata ujuzi na Stadi mbalimbali ambazo ni pamoja na Mapishi, ushonaji, Useremala, Uashi, Ufundi umeme,Ufundi Bomba na Ufundi wa magari na kozi nyingine kutegemea na mtaala wa VETA.
Aidha wamemshukuru Rais Dkt Samia Hassan kwa azma yake ya kujenga Vyuo vya VETA katika kila wikaya ili vijana wengi na watu wazima wapate fursa za mafunzo ya Ufundi Stadi yatakayowawezesha kujiajiri au kuajiriwa.
Post a Comment