HEADER AD

HEADER AD

WANUFAIKA WA TASAF WATAKIWA KUBUNI MIRADI ENDELEVU


Na Gustafu Haule, Pwani

MENEJA ufuatiliaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii nchini(TASAF) Salome Mwakigomba amewataka wanufaika wa mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kuhakikisha wanabuni miradi endelevu ambayo wataitumia katika maeneo wanayoishi hata katika kipindi ambacho Tasaf itakoma.

Mwakigomba ametoa ushauri huo Septemba 16 mwaka huu wakati akizungumza na wanufaika wa mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wa awamu ya tatu waliopo katika Kitongoji cha Mwembebaraza kilichopo Kata ya Janga katika Halmashauri ya Kibaha Vijijini.

       Meneja ufuatiliaji kutoka Tasaf Salome Mwakigomba (Kushoto) akiuliza maswali kwa  afisa kilimo Kata ya Janga Mugisha Vicent namna ambavyo mradi wa Kilimo Mjini unavyoweza kutekelezwa.

Mwakigomba amefika katika Kitongoji hicho akiwa na waratibu na wahasibu wa Tasaf kutoka Halmashauri tisa za mkoa wa Pwani kwa ajili ya kujifunza namna ya ubunifu wa Kilimo Mjini uliofanywa na walengwa hao kupitia afisa kilimo wa Kata ya Janga Mugisha Vicent.

Ziara hiyo ambayo iliongozwa na mratibu wa Tasaf Mkoa wa Pwani Roseline Kimaro, ilikuja baada ya kikao cha mwaka cha kujadili utekelezaji wa shughuli za mpango wa Kunusuru Kaya maskini (TASAF) awamu ya tatu kilichofanyika katika ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge .

Mwakigomba amesema kuwa lengo la Serikali kuanzisha mpango wa TASAF ni kutaka kuwainua wananchi kutoka katika hali duni na kuwa katika hali ya unafuu wa maisha ikiwa pamoja na kuhakikisha wanapata mila mitatu .


Amesema kuwa ili kufikia malengo hayo walengwa wa Tasaf wanatakiwa kubuni miradi endelevu ambayo itawasaidia kupata ujuzi ambao watakwenda kuutumia hata kama Tasaf itakoma au mnufaika kutolewa kwenye mpango.

Mwakigomba amewaomba maafisa kilimo waliopo katika Halmashauri mbalimbali kuwasaidia walengwa wa TASAF katika kubuni miradi ya ajira za muda mfupi(PWP) kama ambavyo Mugisha Vicent amefanya kwa walengwa wa Mwembebaraza.

" Mimi niwaombe ninyi wanufaika ambao mpo kwenye mpango huu hakikisheni mnabuni miradi yenye kuleta tija ili kusudi hata kama ukitoka katika mpango utakwenda kuutumia nyumbani na ukakuletea faida ya kupata chakula na hata kipato," amesema Mwakigomba.

Amesema ameona maeneo mengine wanabuni mradi wa pevingi lakini mradi kama huo inakuwa ngumu kwa mtu kwenda kuutekeleza nyumbani kwake lakini wakibuni miradi ya kilimo inakuwa rahisi kila mmoja kufanya katika eneo lake.

Aidha , amesema TASAF inaendelea kutokana na busara za Rais wa awamu ya sita Dkt.Samia Suluhu Hassan na ndio maana anapenda kuona mpango huo unafanikiwa hivyo ni vyema akaona wale anaowahangaikia wanauthamini mpango huo.

Mratibu wa TASAF mkoa wa Pwani Roseline Kimaro,wamefanya ziara ya mafunzo katika Kitongoji hicho ili kuona kitu gani wataenda kujipanga katika utekelezaji wa mpango huo kwa miaka ijayo.

       Mratibu wa Tasaf Mkoa wa Pwani Roseline Kimaro

Kimaro amesema waratibu hao watajifunza namna ya kufanya marekebisho ya changamoto zilizopo na hivyo kwenda kutumia elimu hiyo katika maeneo yao hasa katika kuwasaidia walengwa wa TASAF upande wa kuimarisha miradi.

Hata hivyo,Kimaro amesema mpango wa Kunusuru kaya maskini (Tasaf)unatekelezwa katika Halmashauri tisa zenye jumla ya Vijiji 417 na hadi kufikia Juni 2023 kaya zinazonufaika ni 35,427.

Mmoja wa wanufaika wa mpango huo Ashura Omari, amesema mpango wa Tasaf kwao ni mkombozi mkubwa katika maisha yao kwani umewasaidia kuwavusha kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine.


Omari amesema kuwa katika kikundi chao wameweza kuanzisha mradi wa Kilimo Mjini kupitia afisa kilimo Mugisha Vicent na kwamba ujuzi waliohupata umewasaidia kuutumia hata katika maeneo ya nyumbani kwao.

"Tunaishukuru TASAF, tunamshukuru Rais Samia kwa kuendelea kutoa fedha nyingi  katika Mpango wa Tasaf na sisi walengwa wa hapa Mwembebaraza umetusaidia kupata mradi wa Kilimo Mjini sehemu ambayo inatusaidia kupata ujuzi na kwenda kuutumia katika maeneo yetu,"amesema Omari

Diwani wa Kata ya Janga Abdallah Kiddo, ameishukuru TASAF chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza TASAF kwani imefanya mambo makubwa katika eneo lake .

Ameongeza kuwa amesema Tasaf imewafanya wananchi wa Kata hiyo kupata mafanikio makubwa na watu wengi wanatoka sehemu mbalimbali kwa ajili ya kwenda katika Kata hiyo kujifunza namna mradi huo unavyotekelezwa.



No comments