HEADER AD

HEADER AD

WAZAZI WAKUMBUSHWA KUWALEA WATOTO KATIKA MAADILI

Na Alodia Babara, Bukoba

SERIKALI pamoja na Viongozi wa madhehebu ya dini katika Wilaya ya Bukoba Mkoani Kagera wamekemea vitendo vya ubakaji na urawiti na kuwaasa wazazi kuchukua tahadhari dhidi ya watoto wao ili kuwaepusha na vitendo hivyo ambavyo  vinaharibu ndoto za badae kwa watoto hao.

Viongozi hao wameyasema hayo Septemba 15,2023 kwenye kongamano la watoto, vijana na makundi maalumu lililotolewa na shirika lisilo la serikali la Tanzania Youth Development Organization (TYDO) lililopo Manispaa ya Bukoba linalojihusisha na kuibua vipaji vya watoto na vijana kimichezo lengo la kongamano lilikuwa ni kutoa Elimu kuhusu unyanyasaji wa kijinsia.

Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Erasto Sima akifungua kongamano hilo amesema wazazi wanapaswa kutimiza wajibu wao kwa kuwalea watoto wao katika maadili mema ili badae nao waweze kuwasaidia.

   Aliyesimama ni mkuu wa wilaya ya Bukoba Erasto Sima na kulia kwake ni Mkurugenzi wa Taasisi ya TYDO Shadrack Bernadi akifungua kongamano la watoto, vijana na makundi maalumu lililolenga kutoa elimu juu ya kupinga vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia

"Kuna wazazi wanakumbatia tabia ovu za watu wanaowanyanyasa watoto wao mfano unakuta mtoto anabakwa au anarawitiwa lakini familia mbili zinashirikiana na kumaliza tatizo hilo bila kuhusisha vyombo vya sheria.

" Baadae mtoto atakapokua akajua kuwa  alifanyiwa kitendo kibaya wazazi wakala fedha bila kuchukua hatua mtoto atachukia sana wazazi, tuache tabia hiyo" amesema Sima

Amesema wazazi wawatunze watoto wao kwa kuwapeleka shule na kuhakikisha wanafuatilia tabia na  mienendo ya masomo yao kwani watakaposomesha watoto nao watawatunza badae.

Dc Sima amemtia moyo Mkurugenzi wa Taasisi ya TYDO Shadrack Bernadi kwa kuanzisha Taasisi hiyo ambayo inasaidia kuwaweka pamoja watoto, vijana na makundi maalumu na kutoa elimu kwao jinsi ya kuchukua tahadhari dhini ya watu wanaotaka kuharibu maisha yao.

Kwa upande wa Shehe wa wilaya ya Bukoba Yusuph Kakwekwe amesema kuwa, wazazi wametupilia mbali malezi ya watoto wao, wazazi hawapeleki watoto wao madrasa au shule za jumapili kwa wakristo huko ndiko wangejifunza maadili na kuwa na hofu ya Mungu.

     Aliyesimama ni shehe wa wilaya ya Bukoba Yusuph Kakwekwe akizungumza na wazazi na watoto hawako kwenye picha juu ya kupinga vitendo vya ukatili vinavyoathiri malezi na makuzi ya mtoto

Amesema kuwa, kuna wazazi wanawatuma watoto,vijana wao waende kuhemea bila kuwapa fedha na kuwa wanakuwa wana maana kwamba mtoto aende akatende mambo maovu ili apewe chochote.

"Wewe mzazi unapomtuma mtoto/ kijana aende kuhemea mahitaji ya familia bila kumpa fedha unakuwa unahitaji atoke katika malezi, wazazi mmesababisha talaka ambazo zimekuwa kiini cha watoto kupoteza maadili, mzazi unapata fedheha ukiwa duniani na ahera utaulizwa" amesema Shehe Kakwekwe

Amesema vijana wanaosaka vipaji mbalimbali wanapaswa kuwa na elimu kwani wenye vipaji bila elimu hawana uwezo wa kutunga nyimbo na wanaporomoka haraka.

Akitoa mada ya unyanyasaji wa kijinsia sagent Dorothea Samwel kutoka dawati la polisi Bukoba, ametoa somo kwa watoto na vijana kuacha kupokea vizawadi mbalimbali zikiwemo pipi, chipsi kutoka kwa watu wasio wa karibu nao na kuwa watu hao wanakuwa wanaandaa mazingira ya kuwabaka na kuwarawiti.

Sajant Samwel amewataka wazazi kuacha migogoro kwenye familia zao kwani wanatoa mwanya mkubwa wa waharifu wa watoto na vijana wao na kuwa migogoro hiyo inarudisha nyuma maendeleo ya familia.

Mkurugenzi wa Taasisi ya TYDO Shadrack Bernadi amesema kuwa, kampein ya kupinga unyanyasaji ni endelevu na wamesajiri watoto na vijana 100 ambao wamekuwa wakiwaweka pamoja kwa ajili ya michezo na kuibua vipaji vyao pamoja na kutoa elimu ya kuepukana na unyanyasaji wa kijinsia ambao unahatarisha maisha yao.

No comments