HEADER AD

HEADER AD

WAZIRI MKUU AWAAGIZA WAKUU WA MIKOA KUTOA MAFUNZO YA UONGOZI KWA WATUMISHI


 Alodia Babara, Bukoba

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kasimu Majaliwa ametoa maagizo 11 kwa viongozi r wa  Kagera ikiwemo kuonyesha kwa vitendo kaulimbiu inayosema ni wakati wa vitendo timiza wajibu wako huku akiagiza wakuu wa mikoa wote nchini kuendesha mafunzo ya uongozi kwa watumishi wa Serikali nchi nzima. 

 Ametoa maagizo hayo Septemba 22, mwaka huu wakati akifunga mafunzo ya siku tano ya uongozi kwa viongozi wa kada mbalimbali za Serikali na Chama cha Mapinduzi  (CCM) mkoani humo yaliyoandaliwa na mkuu wa mkoa huo Hajati Fatma Mwassa.

        Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kasimu Majaliwa.

"Kaulimbiu hii imekuja wakati muafaka ambapo mkoa unahitaji mabadiliko katika kila eneo la ustawi wa jamii ya wana Kagera, kaulimbiu hii ni wito kwa kila kiongozi aliyepo hapa kutafakari nini ameufanyia mkoa huu katika kuleta maendeleo ya haraka.

" Aidha inamtaka kila kiongozi atimize wajibu wake katika dhamana aliyopewa na kuleta tija inayotarajiwa, kaulimbiu hii ni kichocheo cha kuamsha kila kiongozi aliyepo kuchukua hatua za makusudi kuunusuru Mkoa wa Kagera"amesema Majaliwa.

Amesema hiyo ni kutokana na ukweli kwamba, Kagera imekuwa inasuasua na upande wa ukuaji uchumi kwa takribani miaka kumi mfululizo imekuwa haifanyi vizuri licha ya uwezo wa mazingira mazuri ya kiuchumi.

Aidha ametoa maagizo kumi na moja kwa viongozi hao ambapo amesema kuwa anatambua kupitia mafunzo hayo wamejiwekea maazimio ambayo yanahitaji mkakati wa utekelezaji hivyo, basi kila mmoja atoe taarifa ya utekelezaji wa maazimio hayo.


"Wekeni utaratibu wa kufanya tathmini ili kubaini mafanikio ya mafunzo haya ambayo yamegharimu fedha nyingi za Serikali, kila robo mwaka hakikisheni mnafanya kikao cha kupeana mrejesho kuhusu utekelezaji wa maazimio hayo" aliagiza

Amemtaka mkuu wa Mkoa huo kuweka mikataba ya utendaji kazi na wakuu wote wa idara na vitengo katika halmashauri zote,pia amewataka viongozi na watendaji wote kukumbuka  wajibu wao.

Wajibu huo ni kuwatumikia zaidi wananchi na kutatua kero zao kwa kuweka utaratibu wa kuwafuata, kuwasikiliza na kupata ufumbuzi wa kero zao hususani kero za masuala ya migogoro ya ardhi na makundi mbalimbali katika jamii kama wakulima na wafugaji. 

"Kumbukeni kwamba ninyi mnawajibika moja kwa moja kwa wananchi, wasikilizeni na kutatua kero kwa wakati ili waendelee kuiamini Serikali iliyopo madarakani kwani dhamira ya Mheshimiwa Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuwatumikia wananchi.

" Nasi tuliopewa dhamana ya kumsaidia kila mmoja atimize wajibu wake ili wote tuwe tunaongea lugha moja ambayo ni kuwatumikia wananchi na kwa kuwatatulia kero zao"ameagiza Majaliwa  

Pia amewataka watumishi hao kukumbuka kuwa mwaka kesho kutakuwepo na uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambayo ni tathimini ya utumishi wao kwa wananchi na ni kipimo cha imani ya wananchi kwa Serikali iliyopo madarakani.

Amewataka kuweka mikakati mahsusi ya kutatua kero za wananchi zinazoweza kuwa kikwazo katika uchaguzi ujao na si kuongeza kero kwa wananchi, ikiwemo kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na kuepuka vitendo vya rushwa,urasimu usio na tija katika kuwahudumia wananchi.

"Hakikisheni uwepo wa usimamizi wa Fedha zinazoletwa na Serikali pamoja na mapato ya ndani ili zitumike ipasavyo katika maeneo yenu, miradi itekelezwe kwa ubora, ufanisi na ilingane na thamani ya fedha inayoletwa ili wananchi wanufaike na kuendelea kuiamini Serikali yao.

"Vongozi wote wafuatilieni kwa karibu wakandarasi wanaopewa kazi, iwapo mtabaini mapungufu chukueni hatua za haraka msisubiri mpaka Viongozi wakuu waje kwenye maeneo yenu na kubaini mapungufu kwenye miradi wakati ninyi mpo.

 "Wakandarasi wanapojenga miradi chini ya viwango na kusababisha upotevu wa fedha za kodi za Watanzania pia kuwashirikisha watumishi waliopo katika idara na ofisi zetu"amesema 

Naye mkuu wa mkoa wa Kagera Hajat Fatma Mwassa katika taarifa yake kwa waziri mkuu amesema mkoa huo unakabiliwa na utapiamlo mkubwa udumavu mkali kwa watu wake ambapo ni asilimia 34.6.

Pia hari ya uchumi mkoa huo ni mkoa wa 25 kati ya 26 ambapo wamevuka nafasi moja kwa sababu miaka kumi iliyopita Kagera imekuwa ikishika nafasi ya 26 ambayo kwa sasa imechukuliwa na mkoa wa Simiyu.

 "Tunao mdondoko mkubwa kwa wanafunzi ambapo tumebaini  wanafunzi 16,000 wa shule za msingi  na 6,700 wa sekondari hawakumaliza masomo yao kwa kipindi kilichopita.

"Namba ya utapiamlo ni kali sana na hatuwezi kuendelea kubaki nyuma namna hii tumeamua kuleta mafunzo haya ya uongozi ili yatusaidie kujipanga upya kimkakati kuhakikisha hari hii inatoweka"amesema Mwassa. 

Naye Emmanuel Alfred  kutoka Taasisi ya uongozi aliyekuwa mkufunzi mkuu wa mafunzo hayo  amesema matarajio yao ni kwamba watumishi hao wataenda kwa chachu ya maendeleo katika maeneo yao ya kazi ili kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo ipasavyo.

No comments