DC KAMINYOGE : ELIMISHENI WANANCHI MASUALA YA KUKABILIANA NA MAAFA
Na Samwel Mwanga, Maswa
MKUU wa wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu, Aswege Kaminyoge amewaagiza viongozi wote wa wilaya hiyo kuanzia ngazi ya kitongoji hadi wilaya kuweka mikakati madhubuti ya kukabiliana na maafa pindi yanapojitokeza.
Pia amewataka kutoa elimu kwa wananchi hatua itakayosaidia kupunguza athari za maafa.
Ametoa agizo hilo katika kikao kazi cha kamati ya maafa cha wilaya hiyo kilichowashirikisha wadau mbalimbali ili kukabiliana na maafa katika ngazi mbalimbali Wilayani humo kilichofanyika kwenye ukumbi wa halmashauri ya wilaya hiyo mjini Maswa.
Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge (aliyesimama)akisisitiza jambo kwenye kikao kazi Cha Kamati ya Maafa cha wilaya hiyo.Dc Kaminyoge amesema kuwa tayari serikali kupitia Mamlaka ya hali hewa nchini (TMA) imetoa utabiri wa mwelekeo wa mvua za msimu wa vuli zilizoanza kunyesha katika kipindi hiki kuanzia mwezi Septemba mwaka huu ambao umeonesha uwepo wa El-Nino itakayosababisha vipindi vya mvua kubwa.
‘Serikali kupitia Mamlaka ya hali ya hewa(TMA)imeshatoa utabiri wa hali ya hewa na umeonyesha kutakuwa na mvua kubwa katika mikoa mbalimbali na mikoa ya kanda ya ziwa ukiwemo mkoa wetu wa Simiyu.
"Hizi mvua zilizoanza kunyesha ambazo ni mvua za vuli hivyo ni vizuri tuanze kuchukua tahadhari kwa kuwaelimisha wananchi wetu jinsi ya kukabiliana na maafa hayo ambayo yanayoweza kutokea,”amesema.
Amesema kuwa idara zote katika wilaya hiyo zinazohusiana na masuala ya kukabiliana na maafa ni vyema zikajipanga vizuri kwa kuweka mipango yao na kuwa tayari kukabiliana na hali hiyo iwapo maafa yatatokea sambamba na kubaini vihatarishi na kupima utayari wa kukabiliana na matukio hayo.
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Maafa wilaya ya Maswa wakiwa kwenye kikao.“Tunakutana hapa kupeana mikakati na kuandaa mpango madhubuti wa kukabiliana na maafa iwapo yatatokea ni matumaini yangu mpango huu utasaidia kupunguza vihatarishi kama vile mafuriko.
"Kila mmoja wetu kwenye eneo lake aende kutoa elimu kwa wananchi juu ya kukabiliana na maafa ambayo yanayoweza kujitokeza hasa katika kipindi hiki ambacho tunaelezwa kutakuwa na mvua nyingi ” amesisitiza.
Aidha amewataka Wakala wa Barabara nchini(Tanroad)na Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini(Tarura) kuhakikisha mitaro yote waliyoijenga kwa ajili ya maji ya mvua kwenye barabara zao inazibuliwa na wananchi washirikishwe kwenye jambo hilo.
Wajumbe wa Kamati ya Maafa ya Wilaya ya Maswa wakiwa kwenye kikao Cha Kamati ya Maafa wilaya hiyo
"Wananchi waelezwe ni marufuku kutupa taka kwenye mitaro hiyo ili kuweza kuyaruhusu maji kuelekea mahali yalipoelekezwa ili kunusuru uharibifu wa nyumba za makazi ya watu pamoja na barabara.
Naye Mratibu wa Maafa wa Halmashauri ya wilaya ya Maswa, Ana Tulitoza amesema kuwa wameamua kufanya kikao hicho kwa lengo la kujiweka tayari kukabilian na matukio yoyote ya maafa ambayo yanaweza kujitokeza kama ilivyotabiliwa na Mamlaka ya hali ya hewa nchini.
Amesema kuwa wameweza kuwaeleza juu ya Dhana ya usimamizi wa maafa, Mfumo wa Usimamizi wa Maafa,Udhibiti wa eneo la tukio kubwa la dharula pamoja na mkakati wa kukabiliana na Maafa.
Amesisitiza kuwa kiongozi kila eneo anapaswa kutoa taarifa kwa ngazi ya wilaya iwapo kuna tukio lolote la maafa na kuanza kutoa misaada inayohitajika ila taarifa ya matukio ya Maafa ya wilaya haitatolewa na kiongozi yeyote isipokuwa Mkuu wa wilaya tu.
Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge(mwenye suti ya bluu)akifuatilia mada zilizokuwa zinatolewa kwenye kikao kazi cha Kamati ya Maafa wilaya hiyo.Amesema kuwa wataendelea kutoa elimu kwa wananchi katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo juu ya namna ya kujikinga na maafa mbalimbali pindi yanapotokea ili kupunguza athari za majanga hayo.
Kwa upande wake,Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Maswa,Paul Maige amesema kuwa akiwa kiongozi wa madiwani ambao wanaisimamia halmashauri hiyo watahakikisha ya kuwa halmashauri hiyo kwa kushirikiana na wadau wanahakikisha kuwa uwezo wao unakuwa imara wa kukabiliana na maafa na majanga mengine yanapotokea.
Ameongezea kuwa halmashauri hiyo itaendelea kuratibu vyema masuala ya menejimenti ya maafa kwa kuzingatia mifumo ya kitehama ili kuwafikia wananchi kwa wakati kuendelea kuleta matokeo yanayokusudiwa.
“Sisi tumejipanga kuendelea kujenga uwezo kwa wadau wetu ili kuhakikisha uwezo wetu wa kukabiliana na maafa na majanga ya aina mbalimbali unaboreshwa kwa kuzingatia athari zake kiuchumi, kijamii na nyingi.
Post a Comment