BILIONI 1.3 KUJENGA MRADI WA MAJI IPILILO
>> Utahudumia Wananchi 6871
>> Wananchi kutotembea km 10 kutafuta maji
>> CCM yaagiza mradi ukamilike kwa wakati
Na Samwel Mwanga, Maswa
ZAIDI ya Shilingi Bilioni 1.3 zinatarajia kutumika kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maji katika kijiji cha Ipililo wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu na baada ya kukamilika utawahudumia wananchi wapatao 6,871.
Mradi huo unakuja wakati tayari Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini(Ruwasa)wilaya ya Maswa imeongeza upatikanaji wa maji vijijini kufikia asilimia 74.6 kwa sasa.
Hayo yameelezwa Novemba 21 mwaka huu na Meneja wa RUWASA wilaya ya Maswa, Mhandisi Lucas Madaha wakati akitoa taarifa ya uchimbaji na ujenzi wa kisima kirefu katika kijiji cga Ipililo wilayani humo kwa Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya mkoa ya Chama cha Mapinduzi(CCM)ambayo ilitembelea eneo ambalo ndicho chanzo cha maji cha Mradi huo.
Meneja wa Ruwasa wilaya ya Maswa,Mhandisi Lucas Madaha(wa kwanza kulia)akisoma taarifa ya ujenzi wa Mradi wa Maji Kijiji Cha Ipililo kwa wajumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM mkoa wa Simiyu.
Amesema kuwa kupatikana kwa chanzo hicho cha maji katika kijiji hicho kinakwenda kumaliza kero ya muda mrefu ya upatikanaji wa maji safi na salama katika kijiji hicho baada ya kupata chanzo cha maji chenye maji mengi yanayofaa kwa matumizi ya binadamu.
Amesema kuwa utafiti wa maeneo ya uwezekano wa kuchimba visima virefu ulifanywa na Wataalam wa upimaji maji chini ya ardhi kutoka ofisi ya Ruwasa kitengo cha Uchimbaji wa visima virefu na ujenzi wa mabwawa chenye makao makuu yake Jijini Dodoma na kubaini kuwepo kwa chanzo hicho cha maji katika kijiji hicho.
“Baada ya utafiti tuliweza kuchimba kisima na kujengwa lengo kuu ikiwa ni kusafisha kisima,kupanua mkondo wa maji na kutoa vumbi kwenye kokoto zilizowekwa pembeni mwa kisima ili kuzuia kitendo cha kuziba kwa bomba zinazochuja maji kuingia ndani,”amesema.
“Kisima kilifunikwa kwa kutumia uPVC ili kukilinda na shughuli iliyofuata ni upimaji wa uwingi wa maji ili kutambua uwezo wa kisima na kununua pampu yenye uwezo wa chini au unaolingana na uwezo wa kisima,”amesema.
Mhandisi Madaha amesema kuwa baada ya zoezi hilo kisima hicho kiliweza kutoa lita 19,800 kwa saa na hiyo imeonyesha kuwa kina maji ya kutosha na hivyo kinafaa kujengwa mradi huo wa maji.
Mkuu wa mkoa wa Simiyu,Dkt Yahaya Nawanda(wa kwanza kushoto)akitoa maelezo kwa Mwenyekiti wa CCM mkoa huo,Shemsa Mohamed(wa pili toka kulia)juu ya Mradi wa Maji utakaojengwa Kijiji Cha Ipililo wilaya ya Maswa.
Amesema kuwa baada ya sampuli ya maji kuchukuliwa na kupelekwa kwenye maabara ya maji ya Wizara ya Maji iliyopo mjini Shinyanga kwa ajili ya kupima ubora wa maji kikemia,kibaiolojia na kifizikia yalibainika kuwa yanafaa kwa ajili ya matumizi ya binadamu.
Aidha amesema kuwa mradi huo utaanza kutekelezwa mwezi Januari 2024 kwa kipindi cha miezi tisa na kwa sasa upo katika hatua ya manunuzi ambapo baadhi ya kazi zilizopangwa kufanyika ni pamoja na ujenzi wa vituo 12 vya kuchotea maji,Ujenzi wa nyumba ya mitambo na ujenzi wa tenki ka maji lenye ujazo wa mita za ujazo 135 kwenye mhimili wa mita 15.
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu, Shemsa Mohamed ambaye amewaongoza wajumbe hao kufanya ziara kwenye eneo hilo ameuagiza Uongozi wa mkoa wa Simiyu kuhakikisha unasimamia ujenzi huo ili uweze kukamilika kwa wakati ili kufikia malengo ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ya kumtua Mama ndoo kichwani.
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu,Shemsa Mohamed(aliye kati)akimsikiliza Meneja wa Ruwasa wilaya ya Maswa,Mhandisi Lucas Madaha(mwenye kofia nyeupe)kwenye eneo ambalo utajengwa Mradi wa Maji katika Kijiji cha Ipililo.
Amesema kuwa Rais Dkt Samia amekuwa akitoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya sekta ya maji hivyo ni vizuri serikali ikasimamia fedha hizo zinazopelekwa kujenga miradi kama hiyo ili ziweze kutumika kama ilivyokusudiwa ili wananchi waweze kunufaika nayo.
“Rais Dkt Samia Suluhu ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM anatoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa miradi kama hii hivyo binafsi nampongeza sana na hizi fedha zinazoletwa zitumike kama zilivyokusudiwa hivyo nikuagize mkuu wa mkoa wa Simiyu hakikisha mradi huu unakamilika kama ulivyopangwa kwa kuwa fedha zipo kwa ajili ya ujenzi wa mradi huu wa maji katika kijiji cha Ipililo,”amesema.
Naye Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki,Stanslaus Nyongo amesema kuwa kijiji cha Ipililo kina idadi kubwa ya wananchi zaidi ya 10,000 hivyo mradi huo utakapokamilika utasaidia kupatikana kwa maji safi na salama na utawapungizia muda wa kutafuta maji wakinamama kwani maji sasa yatapatika kwa umbali mfupi kutoka kwenye nyumba zao na wengine watayavuta ndani ya nyumba.
Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki,Stanslaus Nyongo (aliye kati) akizungumza kwenye eneo la Kijiji Cha Ipililo wilaya ya Maswa ambapo patajengwa Mradi wa Maji.
Amesema kuwa awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu imekuwa ikiiwezesha RUWASA kwa kuipatia fedha nyingi za kutekeleza miradi ya maji maeneo ya vijijini kwa lengo la kutekeleza ilani ya CCM ya mwaka 2020 -2025 inayotaka kufikisha huduma ya maji vijiji kwa asilimia 85 ifikapo mwaka 2025.
Diwani wa Kata ya Ipililo, Sayi Maige amesema kuwa ujio wa mradi huo utaondoa kero ya upatikanaji wa maji safi na salama katika kijiji hicho ambapo wakinamama walikuwa wakitembea umbali mrefu wa kilomita 10 kwenda kufuata maji kwenye mto ambayo si safi na salama kwa matumizi ya binadamu kwani na mifugo nayo imekuwa ikiyatumia maji hao kwa kunywa.
Amesema kuwa ameona dhamira ya dhati ya Rais Dkt Samia ya kumtua Mama ndoo kichwani inakwenda kutimia katika kijiji hicho kwani kwa sasa wana matumaini makubwa ya kuishi na kuwa na maisha bora na kuondokana na tabu na mateso makubwa yanayo sababishwa na ukosefu wa maji ya bomba.
Agnes Marco mkazi wa kijiji cha Ipililo ameipongeza serikali kupitia wakala wa maji safi na Usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa)wilaya ya Maswa kwa kuona umuhimu wa kujenga mradi huo ambao utahudumia wananchi wa kijiji hicho kwani ndilo suluhusho pekee la kuwapunguzi umbali mrefu wa kwenda kutafuta maji kwenye vyanzo vya maji ambavyo si salama kwa matumizi ya binadamu.
Post a Comment