HEADER AD

HEADER AD

BILIONI 8 KUJENGA DARAJA LA MTO ITEMBE WILAYANI MEATU

Na Samwel Mwanga, Meatu

SERIKALI kupitia Wakala wa Barabara(Tanroad)inatekeleza ujenzi wa daraja lenye urefu wa Mita 150 katika Mto Itembe wilaya ya Meatu mkoa wa Simiyu ili kuweza kurahisisha mawasiliano ya barabara kati ya mkoa wa Simiyu na mkoa wa Singida.

Mto huo ulikuwa ni kikwazo cha mawasiliano  nyakati za mvua za masika hasa usafiri wa barabara kati ya wilaya ya Meatu na wilaya ya Mkalama iliyoko mkoani Singida.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa ujenzi wa daraja hilo,Kaimu Meneja wa Tanroads mkoa wa Simiyu,Mhandisi Raphael Chasama kwa Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi(CCM)mkoa huo, amesema kuwa daraja hilo linajengwa na Mkandarasi Kampuni ya M/S Roctronic ya Mjini Moshi mkoani Kilimanjaro kwa gharama ya zaidi ya Tsh. Bilioni 8 kwa mkataba wa mwaka mmoja.

      Kaimu Meneja wa TANROADS mkoa wa Simiyu,Raphael Chasama(wa pili kulia)akitoa taarifa kwa Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu,Shemsa Mohamed(wa kwanza kushoto)ya ujenzi wa daraja katika mto Itembe wilaya ya Meatu.

Amesema kuwa ujenzi huo ulianza Oktoba 27 mwaka jana na ulitakiwa ukamilike mwezi Machi 3 mwaka huu lakini hadi sasa ujenzi huo haujakamilika ila umefikia asilimia 63.

Mhandisi Chasama amesema kuwa miongoni mwa kazi ambazo hadi sasa zimefanyika ni pamoja na ujenzi wa nguzo sita katika urefu wa Meta 26 zenye kina cha wastani wa Meta 6 na upana wa meta 11.

Sehemu ya ujenzi wa daraja katika Mto Itembe wilaya ya Meatu mkoa wa Simiyu linalojengwa na TANROADS.

 “Moja ya manufaa yatakayopatikana baada ya kukamilika kwa ujenzi wa daraja hilo ni pamoja na kuwa kichocheo cha uchumi na mawasiliano kwa wananchi wa wilaya za Meatu katika mkoa wa Simiyu na wilaya ya Mkalama katika mkoa wa Singida,”amesema.

Amesema kuwa changamoto kubwa inayokabili utekelezaji wa mradi wa ujenzi huo ni ucheleweshaji wa malipo kwa mkandarasi hadi sasa amelipwa kiasi cha fedha Shilingi Milioni 2.2 ikijumisha Shilingi Milioni 1.2 za malipo ya awali.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu,Shemsa  Mohammed amempongeza Rais Dkt Samia suluhu Hassan ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa kwa kutoa fedha hizo kwa ajili ya ujenzi huo wa daraja hilo.

      Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu,Shemsa Mohamed (wa kwanza kulia)akisoma taarifa ya ujenzi wa daraja la Mto Itembe wilaya ya Meatu.

“Nichukue fursa hii kumpongeza Rais Dkt Samia Suluhu kwa kutoa kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo ambalo litakuwa ni kiungo kikubwa katika ya wilaya ya Meatu na Wilaya ya Mkalama wilayani Meatu".

‘’Mto huu ulikuwa unakata mawasiliano niombe mujenzi huu ukamilishwe kwa wakati ambao ameongezewa Mkandarasi na kila Mkandarasi anayetekeleza mradi  katika mkoa wa Simiyu wengi wao wanaacha madeni kwa vibarua na mamalishe.

"Meneja wa TANROADS hakikisha mkandarasi huyu haachi madeni kwa vibarua kwa sababu serikali inatoa fedha ya kutekeleza mradi husika, hakikisheni hakuna madeni yanayobakia baada ya mkandarasi kukamilisha ujenzi wa mradi huu wa ujenzi wa daraja,”amesema.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Dkt Yahaya Nawanda alimhakikishia Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu kuwa watahakikisha wanasimamia utekelezaji wa mradi huo ikiwemo kumsimamia mkandarasi anayetekeleza miradi huo.

      Nguzo zilizojengwa kwenye daraja la Mto Itembe wilaya ya Meatu mkoa wa Simiyu.

Baadhi ya wananchi wametoa pongezi mbele ya Wajumbe wa  Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Simiyu kukagua ujenzi huo  wamesema siku za nyuma mifugo na binadamu walikuwa wanapoteza maisha nyakati za masika kwa kusombwa na maji na pia kukwama kusafiri kutokana na mto huo kujaa maji.

‘’Tunaishukuru Serikali ya Dkt Samia Suluhu kwa kutujengea daraja hili hakika tumeona matunda ya serikali ya Chama Cha Mapinduzi tunaishukuru serikali imetukomboa kwa kujenga daraja katika  Mto Itembe,’’ amesema Matei Mashauri.

       Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu,Shemsa Mohamed(wa kwanza kulia)akimsikiliza Kaimu Meneja wa TANROADS mkoa huo,Raphael Chasama(aliye mbele mwenye kuzibao cha njano)juu ya ujenzi wa daraja katika mto Itembe wilaya ya Meatu.


No comments