SERIKALI YAWAONDOLEA ADHA WANAFUNZI KUSOMA KWENYE DARASA LILILOJENGWA KWA MITI, KUEZEKWA KWA NYASI
>> Ni katika Kitongoji cha Kasala- Meatu
>> Serikali yajenga madarasa sita
>> Wafugaji waipongeza Serikali
Na Samwel Mwanga, Meatu
JAMII ya wafugaji katika kitongoji cha Kasala kilichoko kijiji cha Lukale kwenye Kata ya Bukundi wilaya ya Meatu mkoani Simiyu wameipongeza serikali kwa kujenga vyumba sita vya madarasa katika shule ya msingi Kasala.
Awali wanafunzi wa shule hiyo walikuwa wakisomea kwenye darasa ambalo limejengwa kwa miti na kuezekwa kwa nyasi.
Darasa la shule ya Msingi Kasala wilaya ya Meatu mkoa wa Simiyu kabla ya ujenzi wa madarasa mapya sita ya kisasa kujengwa na serikali
Wakizungumza Novemba 22 mwaka huu mbele ya Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM)mkoa wa Simiyu waliofanya ziara katika shule hiyo ili kukagua mradi wa ujenzi wa matundu ya vyoo katika shule hiyo wamesema kuwa kwa sasa wanafunzi hao wanasoma katika mazingira rafiki na salama.
Wamesema kuwa darasa hilo la miti lilijengwa na mwananchi mmoja ambaye aliona umuhimu wa watoto wa eneo hilo kupata elimu kwani shule iliyokuwepo ilikuwa umbali wa kilomita 70 kwenda na kurudi hivyo kuwafanya watoto hao kushindwa kumudu kwenda umbali mrefu kwa ajili ya kupata elimu.
Wamesema kuwa kwa sasa serikali imeweza kujenga vyumba sita vya madarasa na wanafunzi waliko katika shule hiyo wamekuwa wakipata elimu katika mazingira mazuri kutokana na kujengwa kwa madarasa hayo ambayo yamewekewa madawati.
Moja ya vyumba vya madarasa katika Shule ya Msingi Kasala wilaya ya Meatu mkoa wa Simiyu yaliyojengwa na serikali
Mkazi wa Kitongoji hicho Nirey Ndashibajuty amesema “Shule hii ilianza kama shule shikizi kwa wanafunzi kusomea kwenye darasa ambalo limejengwa kwa miti na kuezekwa kwa nyasi kutokana na wanafunzi wa kitongoji hicho kutembea umbali mrefu kwenda kusoma katika shule ya msingi Lukale.
"Shule ambayo iko umbali wa km 70 kwenda na kurudi na hatimaye serikali ikasikia kilio chetu na kutujengea madarasa haya" amesema.
Wamesema kwa sasa shule hiyo ina wanafunzi wa darasa la kwanza hadi darasa la sita ina jumla ya wanafunzi 72 wa jamii ya wafugaji ambao walikuwa wakikosa elimu lakini kwa sasa wanapata elimu katika mazingira mazuri yenye madarasa ya kisasa.
“Hii shule yetu kwa sasa ina wanafunzi 72 ambao ni kuanzia darasa la awali hadi darasa la sita na hili eneo letu sisi ni wafugaji na kwa kipindi hiki tumeelimika ndiyo maana watoto wetu wako shuleni.
"Kwa kweli nitumie fursa hii kuishukuru sana serikali inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu kwa kuweza kutujengea shule hii yenye madarasa ya kisasa,”amesema Bashiru Kidengeles ambaye ni mkazi wa kijiji cha Kasala.
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu, Shemsa Mohamed ametoa pongezi kwa serikali inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa kwa kutoa fedha nyingi katika miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo miradi ya sekta ya Elimu.
Wajumbe wa Kamati ya Siasa ya mkoa wa Simiyu ya CCM na baadhi ya Viongozi wa wilaya ya Meatu wakiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wa darasa la kwanza katika shule ya Msingi Kasala wilaya ya Meatu
Amesema kuwa kujengwa kwa shule hiyo ni kunaonyesha jinsi serikali ya awamu ya sita inavyowajali wananchi wake katika kuwaletea maendeleo katika sekta ya elimu hasa kwa jamii ya wafugaji ambao mara nyingi wamekuwa wakiikosa kutokana na mazingira yao ya kuhamahama.
Pia amesema kuwa kutokana na umuhimu wa shule hiyo kwa wafugaji ni vizuri sasa changamoto zilizoko katika shule hiyo ikiwemo ujenzi wa choo cha wanafunzi ambao unaendelea ukakamilishwa hadi kufikia mwezi Desemba mwaka huu ili kuepuka magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu na kuhara.
“Serikali inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imefanya kazi kubwa sasa katika ujenzi wa shule za msingi na sekondari katika kitongoji hiki ambacho wanafunzi walikuwa wanatembea umbali mrefu kwenda shuleni.
'Lakini leo hii tuna shule yenye madarasa ya kisasa hivyo nikuagize Mkuu wa mkoa wa Simiyu uhakikishe choo hiki cha wanafunzi kinakamilika kwa wakati kama mlivyopanga ili kiweze kutumika,”amesema.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Dkt Yahaya Nawanda amesema kuwa serikali imetumia kiasi cha Tsh Milioni 120 zilizotokana na mapambano ya UVIKO19 kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo na kwa sasa inaendelea na ujenzi wa matundu 10 ya vyoo katika shule hiyo na kuhaidi kutekeleza agizo la Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu la kutaka ujenzi wa vyoo kukamilika kwa muda uliopangwa.
Awali Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Kasala, Peter Simon akisoma taarifa ya ujenzi wa choo cha wanafunzi amesema kuwa utagharimu kiasi cha Tsh. Milioni 11 na ujenzi huo umeanza tangu Mei 15 mwaka huu.
Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Kasala,Peter Simon(mwenye fulana bluu)akisoma taarifa ya ujenzi wa choo Cha shule hiyo kwa wajumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM mkoa wa Simiyu
Amesema ujenzi ulipaswa kukamilika Septemba mosi mwaka huu ila umekuwa ukikumbwa na changamoto mbalimbali zikiwemo ushiriki mdogo wa jamii katika shughuli za maendeleo.
Pia maji kupatikana kwa shida zaidi ya kilomita 70, upatikanaji mgumu wa mafundi kutokana na mazingira ya shule na gharama kubwa ya usafirishaji wa vifaa vya ujenzi kutokana na mazingira ya ujenzi wa choo hicho.
Post a Comment