HEADER AD

HEADER AD

DC KAMINYOGE : HALMASHAURI YA MASWA KUSANYENI MAPAT0

Na Samwel Mwanga, Maswa

HALMASHAURI ya wilaya ya Maswa mkoani Simiyu imetakiwa kuweka mikakati madhubuti ili kuhakikisha inakusanya mapato yote ya serikali ili iweze kujiendesha sambamba na kufikia malengo ya makusanyo ya ndani waliojiwekea.

Hayo yameelezwa Novemba 17 mwaka huu na Mkuu wa wilaya ya Maswa ,Aswege Kaminyoge wakati akitoa salamu za serikali katika kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo kilichofanyika mjini Maswa katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Maswa.

        Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge akizungumza katika kikao cha baraza la madiwani la halmashauri ya wilaya hiyo

Amesema kuwa moja ya vigezo wanavyopimwa katika utendaji wa kazi zao wakiwemo Madiwani ,Watendaji wa Halmashauri hiyo,Mkuu wa wilaya na Mkuu wa mkoa ni ukusanyaji wa mapato ya ndani katika halmashauri.

Dc Kaminiyoge amewaomba Madiwani kuhakikisha wanawasisitiza watendaji katika halmashauri hiyo wanaendelea kukusanya mapato huku wakikumbuka kuwa kipengere hicho na wenyewe wanapimwa nacho katika utendaji wao wa kazi.

      Baadhi ya Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Maswa wakiwa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani.

“Rai yangu kwenu waheshimiwa madiwani ni kushauriana na kuwasisitiza watendaji wa halmashauri yetu ya kuhakikisha wanaendelea kukusanya mapato ya halmashauri ya wilaya ya Maswa.

"Rais ameweka kama kigezo mojawapo cha utendaji kazi wetu kuanzia ninyi madiwani,watendaji wa halmashauri, sisi wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa kwa hiyo tukumbuke tunapimwa wote kwa kigezo hiki cha kukusanya mapato,”amesema.

Amesema kuwa madiwani hao wakumbuke kuwa katika bajeti walitenga fedha asilimia 40 kwa ajili ya miradi ya maendeleo,asilimia 30 ya fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya miradi ya maendeleo na asilimia 10 kwa ajili ya kuwawezesha Wanawake,Vijana na Walemavu fedha za mapato ya ndani hivyo ni vizuri kuweka nguvu kubwa na ubunifu mkubwa katika ukusanyaji wa mapato.

      Wajumbe wa baraza la Madiwani la halmashauri ya Wilaya ya Maswa wakiwa kwenye kikao

Amesema taarifa ambazo amezipata zinaonyesha mwelekeo wa ukusanyaji wa mapato katika halmashauri ya wilaya hiyo unakwenda vizuri hivyo ni vizuri wajitahidi walau kufikia Desemba 30 mwaka huu waweze kufikia kiwango cha makusanyo kwa asilimia 50.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa,Paul Maige ambaye ni diwani wa Kata ya Shanwa amesema kuwa ili waweze kufikia malengo waliyojiwekea katika kuwahudumia wananchi wa wilaya hiyo ni lazima uwepo umoja na mshikamano kwa ajili ya ustawi wa wilaya ya Maswa.

        Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa,Paul Maige(aliyesimama)akifunga kikao cha baraza la madiwani la halmashauri hiyo.

Amesema ili waweze kuleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi katika wilaya hiyo ni lazima washikamane katika kutekeleza mambo mbalimbali ambayo wamekubaliana kupitia vikao na mojawapo ni suala la ukusanyaji wa mapato.

“Nitoe wito tudumishe umoja na mshikamano wetu kwa kila mmoja kwenye eneo lake tukumbuke sisi sote tukiwemo madiwani na watendaji wetu ni lazima tuwe wamoja kwani wote tuna jukumu la kuhudumia mwanachi wa wilaya hii na tukiwa wamoja nina imani kubwa tutaleta mapinduzi makubwa kwa ustawi wa wilaya yetu,”

“Pasipo umoja wetu maendeleo ya wilaya ya Maswa yatakuwa mashakani tukumbuke hawa wananchi ndiyo waliotuchangua na kusababisha siye kuwa humu wanatutegemea katika kuwaletea maendeleo hivyo kwa umoja wetu tuhakikishe tunakusanya mapato yetu ya ndani kwa uaminifu mkubwa,”amesema.

Pia ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais Dkt Samia Suluhu kwa kuendelea kuwapatia fedha halmashauri ya wilaya hiyo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta mbalimbali zikiwemo elimu,afya,maji,maendeleo ya jamii na  miundombinu.

Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo,Vivian Chirstian amewaagiza Watendaji wa Kata zote kusimamia mawakala lengo ikiwa ni kuhakikisha yanapatikana mapato stahiki kulingana na kinachopatikana na kwamba mtendaji atakayeshindwa  kufanya hivyo hatua za kisheria na kinidhamu zitachukua mkondo wake.

       Baadhi ya Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Maswa wakiwa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani.

“Tumewaagiza watendaji wote wa Kata zote 36 zilizoko ndani ya halmashauri yetu kuhakikisha wanawasimamia hao mawakala wanaokusanya mapato yanapatikana mapato stahiki kulingana na kinachopatikana na Mtendaji ambaye atashindwa kufanya hivyo  tutamchukulia hatua kali za kisheria na kinidhamu,”amesema.


         Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Maswa,Paul Maige akiendesha kikao cha Baraza la Madiwani cha Halmashauri ya wilaya hiyo.

No comments