HEADER AD

HEADER AD

TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI YATINGA RORYA UBORESHAJI WA MAJARIBIO DAFTARI LA WAPIGA KURA


>>Yakutana na wadau wa uchaguzi wakiwemo viongozi wa Dini, Vyama vya Siasa, Makundi maalum

>>Zoezi la uboreshaji wa majaribio  kufanyika Kata ya Ikoma-Rorya 

>>Tume kutumia mfumo wa VRS uandikishaji wapiga kura

>>Yaanzisha mchakato wa kuboresha taarifa mtandaoni kwa wapiga kura wanaotaka kubadilisha, kuhamisha taarifa zao

>>Mkurugenzi wa uchaguzi awataka wananchi kujitokeza kuandikishwa na kuboresha taarifa zao

Na Dinna Maningo, Rorya 

IBARA ya 74 (6) (a) na (d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, inaipa Tume ya Taifa ya Uchaguzi jukumu la kusimamia na kuratibu uandikishaji wa wapiga kura katika uchaguzi wa Rais na Wabunge wa Jamhuri ya Muungano na Madiwani kwa Tanzania Bara.

Kifungu cha 15 (5) cha sheria ya uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292, Tume inatakiwa kuboresha Daftari la kudumu la wapiga kura mara mbili kati ya uchaguzi mkuu uliomalizika na uchaguzi unaofuata.

Katika kutekeleza jukumu hilo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania inafanya uboreshaji wa majaribio katika kata ya Ng'ambo iliyopo halmashauri ya Manispaa ya Tabora, mkoani Tabora na Kata ya Ikoma iliyopo halmashauri ya Wilaya ya Rorya, mkoani Mara kuanzia tarehe 24 hadi 30, Novemba, 2023.

Novemba, 20, 2023, Tume ya Taifa ya Uchaguzi imefanya mkutano na wadau wa uchaguzi uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Mapsap Wilayani Rorya, mkoani Mara.

Mkutano huo umeongozwa na Mkurugenzi wa uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Ramadhani Kailima pamoja na maafisa wengine wa Tume ambapo ilieleza lengo la kuwakutanisha wadau wa uchaguzi na kutoa fursa kwa wadau kuchangia hoja, kuuliza maswali juu ya uboreshaji wa majaribio wa daftari la kudumu la wapiga kura.

     Mkurugenzi wa uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Ramadhani Kailima

Ramadhani anasema kuwa lengo la uboreshaji wa majaribio ni kuvifanyia majaribio vifaa na mfumo wa uboreshaji wa Daftari ili kuweza kubaini changamoto zinazoweza kujitokeza na kuzipatia ufumbuzi mapema kabla ya kuanza rasmi kwa zoezi la uboreshaji nchi nzima.

" Itakumbukwa kuwa kwenye uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura wa mwaka 2019 na 2020, Tume ilitumia teknolojia ya Biometric Voter Registration (BVR) iliyohusisha matumizi ya BVR Kit zenye uzito wa kilo 35 na mara kadhaa kulikuwa na changamoto ya usafirishaji kutoka eneo moja kwenda lingine" anasema Ramadhani.

Mkurugenzi huyo wa uchaguzi anasema kuwa zoezi lijalo Tume itatumia mfumo wa uandikishaji wa wapiga kura (Voters Registration System- VRS) ambao umewekwa katika Mini BVR Kit yenye uzito wa kilo 15 pamoja na vifaa mbalimbali vya kisasa vinavyowasiliana na vyenye uwezo wa kuchukua na kutunza taarifa za wapiga kura na vinavyobebeka kwa urahisi.

" Mfumo wa VRS utatumika kumuandikisha mpiga kura mpya, kuboresha taarifa za mpiga kura aliyeandikishwa awali, kumuondoa kwenye daftari mpiga kura aliyepoteza sifa na kumpatia kadi mpiga kura aliyepoteza au kadi yake kuharibika.

Uboreshaji wa taarifa mtandaoni

Mkurugenzi huyo anasema mbali na mfumo wa VRS Tume imeanzisha mchakato wa kuboresha taarifa mtandaoni ambapo utaratibu huo unamlenga mpiga kura aliyeandikishwa katika daftari la kudumu la mpiga kura anayetaka kurekebisha au kubadilisha taarifa zake, anayetaka kuhamisha taarifa zake kutoka kituo cha awali kwenda kingine au anayetaka kufanya vyote kwa pamoja.

              Wadau wa uchaguzi wakiwa kwenye mkutano ulioandaliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi 

" Katika kutekeleza mchakato huo, mpiga kura anatakiwa kufuata hatua zifuatazo ; (i) Ataingia kwenye Tovuti ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi www.nec.go.tz kwa kutumia kompyuta au simu janja kisha atabonyeza kiunganishi (link) kilichoandikwa " Boresha taarifa za mpiga kura" au atatumia anuani ya ovrs.nec.go.tz itakayompeleka moja kwa moja kuanzisha mchakato;

" (ii) Baada ya ombi hilo kufanyiwa kazi na Tume, mpiga kura atapokea ujumbe mfupi kupitia namba yake ya simu wenye namba ya kumbukumbu ( token) ambao utamtaka kwenda kwenye kituo cha kuandikisha wapiga kura kwa ajili ya kumaliza hatua zilizobaki" anasema.

Ramadhani anatoka angalizo kuwa wapiga kura waliopoteza kadi au kadi zao kuharibika hawatahusika na utaratibu huu, hivyo watatakiwa kufika kituo cha kuandikisha wapiga kura na kufuata taratibu zote zilizowekwa.

       Mkurugenzi wa uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Ramadhani Kailima

Anawasisitiza wananchi kukagua kadi zao za mpiga kura kabla ya kuondoka kituoni ili kama kuna makosa ya taarifa zao yaweze kurekebishwa na watunze kadi zao.

Wananchi Ikoma jitokezeni 

Mkurugenzi wa uchaguzi wa Tume ya Taifa anawaomba wananchi wa Kata ya Ikoma Wilayani Rorya kujitokeza katika uboreshaji wa majaribio wa daftari la kudumu la wapiga kura zoezi litakalofanyika katika vituo sita katika Kata hiyo.

        Wadau wa uchaguzi wakiwa mkutanoni

" Uboreshaji wa majaribio utahusisha kuandikishwa raia wa Tanzania mwenye umri wa miaka 18 au zaidi na atakayetimiza umri wa miaka 18 kabla au ifikapo tarehe ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Katika mkutano huo wa Tume, wadau wa uchaguzi walipata fursa ya kujadili mada inayohusu maandalizi ya zoezi la uboreshaji wa majaribio, kuonesha kwa vitendo uandikishaji utakavyofanyika kituoni na maboresho yaliyofanyika katika mifumo ya uandikishaji.

    Mmoja wa Wadau wa uchaguzi akichangia mada 

" Hivi sasa mpiga kura anayeboresha au kuhamisha taarifa zake ataweza kuanzisha mchakato kwa njia ya mtandao, jambo hili litasaidia kutoka muda na kurahisisha mchakato, hivyo wadau mnaombwa kushiriki kikamilifu katika kutoa maoni na mapendekezo yenu ili kufanikisha utekelezaji wa zoezi lililopo mbele yetu" anasema Ramadhani.

Anawataka Wananchi, Vyama vya siasa kuwabainisha waliopoteza sifa za kuwa wapiga kura huku akiwaasa wadau wote kuendelea kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo katika kipindi chote cha uboreshaji wa majaribio.

          Wadau wa uchaguzi wakiwa mkutanoni

" Tume tunategemea kuona Vyama vya Siasa, Viongozi wa Dini mnafikisha ujumbe sahihi kwa wananchi ambako uboreshaji wa majaribio utafanyika ili wananchi wenye sifa ya kuandikishwa na kuboresha taarifa zao wajitokeze kwa wingi kushiriki zoezi hili" anasema Ramadhani.

Ameongeza kuwa Vyama vya Siasa vitashiriki katika zoezi hilo kwa kuweka wakala mmoja katika kila kituo cha kuandikisha wapiga kura, lengo ni kushuhudia na kujiridhisha juu ya taratibu zitakazotumika wakati wa uboreshaji wa majaribio wa daftari.

       Mdau wa uchaguzi kutoka chama cha Demokrasia na maendeleo CHADEMA akichangia hoja

Anasema Tume imejipanga kuhakikisha kuwa wananchi wanapata uelewa wa kutosha kuhusu uboreshaji wa majaribio kwa kutumia njia mbalimbali za kutoa Elimu ya mpiga kura zikiwemo; kukutana na wadau wengine wa uchaguzi Kitaifa kama ilivyofanyika kwa Rorya na mikoa husika 

" Njia nyingine zitakazotumika ni vyombo vya habari hasa Redio za kijamii,katika eneo hili tunawategemea waandishi wa habari kushirikiana nasi kwa kutoa taarifa za uwepo wa zoezi hili lakini pia kuwahamasisha wananchi kujitokeza katika vituo vya kujiandikisha.

"Pia Tume itatumia mitandao ya kijamii ambayo matumizi yake yanazidi kukua kila siku, makala za magazeti, vipeperushi na magari ya matangazo" anasema Rammadhani.

Mchango wa Vyombo vya Habari  

Anasema Tume inatambua na kuthamini mchango wa vyombo vya habari kama wadau muhimu katika upashaji habari na ndio maana tunao hapa wawakilishi wa vyombo hivyo.

"Matarajio ni kuwa kundi hili likipata uelewa wa kutosha wa mchakato wa uchaguzi, elimu na taarifa kwa umma kuhusu uchaguzi itatolewa kwa weledi na usahihi. Tunavishukuru vyombo vya habari kwa kuendelea kutoa ushirikiano kwa Tume wakati wote inapokuwa inatimiza majukumu yake.

Wadau waipongeza Tume ushirikishaji

Ester Nyambita ni mkazi wa Obwere- Shirati Kata ya Mkoma anaipongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuja na mfumo mpya wa uandikishaji wa VRS.

        Ester Nyambita ni mkazi wa Obwere- Shirati Kata ya Mkoma

 " Tunaipongeza Tume kuboresha mfumo wa uandikishaji daftari la kudumu la wapiga kura, ule mfumo wa BVR ulikuwa na changamoto sana lakini huu wa VRS ubebaji wake utakuwa rahisi,pia tutaweza kurekebisha taarifa kupitia Tovuti yao" amesema Ester.

Shekh wa Mkoa wa Mara Msabaha Kassim Mgabo amesema kuwa elimu waliyopewa na Tume itasaidia kuondoa minong'ono kwa wapiga kura katika uandikishaji huku akisisitiza ziwepo kadi za uraia kwani zitasaidia katika utambuzi wa wananchi kama ni Watanzania.
  Shekh wa Mkoa wa Mara Msabaha Kassim Mgabo

" Tunaishukuru Tume kutupa elimu ya majaribio ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, itasaidia kuondoa minong'ono. Tunaomba kazi za uraia ziwafikie wananchi hii itasaidia kuwatambua watanzania" anasema Shekh.

Helena Paul  mwenye ulemavu wa ngozi mkazi wa mtaa wa maziwa kata ya Nyakati Manispaa ya Musoma ulemavu wa ngozi ameipongeza Tume ya uchaguzi kuwashirikisha watu wenye ulemavu.

     Helena Paul  mwenye ulemavu wa ngozi mkazi wa mtaa wa maziwa kata ya Nyakati Manispaa ya Musoma

"Watu wenye ulemavu tumeshirikishwa, tumeshiriki watu sita na vyama vya walemavu vipo sita na tumepewa nafasi ya kutoa maoni yetu, kila chama kimetoa maoni yao na yamesikilizwa na maswali yaliyoulizwa yamepata majibu.

Fatuma Adam mkazi wa Musoma ni Katibu wa watu wenye matatizo ya afya ya akili mkoa wa Mara ambaye pia ni mwalimu wa watu wenye Ulemavu shule ya msingi Mwembeni anasema katika zoezi la uandikishaji kuna changamoto ya watafsiri wa lugha ya alama.

    Fatuma Adam mkazi wa Musoma ambaye ni Katibu wa watu wenye matatizo ya afya ya akili mkoa wa Mara

" Mtu mwenye ulemavu wa kusikia anaweza kuwa na ndugu yake aliyemsindikiza kwenye kituo cha kupiga kura lakini hana uwezo wa kumtafsiria lugha ya alama, kwahiyo watu wenye uziwi wanakosa haki ya taarifa, tunaomba vituo vya uandikishaji,kupigia kura kuwe na watafsiri wa lugha ya alama" anasema Fatuma.

Hata hivyo wadau wa uchaguzi wanaiomba  Idara ya Uhamiaji kutoa elimu mipakani kama njia ya kusaidia wananchi kuwafichua watu wanaojiandikisha ambao siyo raia wa Tanzania.

        Wakili wa Serikali Tume ya Taifa ya Uchaguzi akizungumza na wadau wa uchaguzi







No comments