DC KAMINYOGE : TUPANDE MITI KUREJESHA UOTO WA ASILI
Na Samwel Mwanga, Maswa
MKUU wa Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Aswege Kaminyoge ameongoza wananchi wa wilaya hiyo kushiriki katika zoezi la kampeni ya kupanda Miche ya Miti 1,500,000 ili kurudisha Uoto wa Asili.
Zoezi hilo la Kampeni ya upandaji wa Miti limefanyika leo Novemba 10 mwaka huu katika shule ya sekondari Zanzui ambapo zaidi ya miti 600 imepandwa.
Akizungumza na viongozi mbalimbali pamoja na wananchi walioshiriki katika zoezi hilo la uzinduzi wa upandaji miti amesema kuna umuhimu mkubwa na faida nyingi katika utunzaji wa mazingira hususani kupanda miti ambapo faida zake ni pamoja na kupata hewa safi, mvua za kutosha , kivuli, kutumika kama mipaka na kulinda vyanzo vya maji.
Amesema kuwa pamoja na kuwepo na faida hizo lakini bado wako baadhi ya watu wamekuwa wakikata miti kwa kasi kubwa kwa ajili ya matumizi mbalimbali hali ambayo inasababisha hali ya ukame katika wilaya hiyo.
Dc Kaminyoge amesema kuwa serikali kwa kuona hali hiyo ilitoa agizo kupitia kwa Rais Dkt Samia Suluhu ya kuwa kila musimu wa mvua unapoanza ni lazima ipandwe miti 1,500,000 ili tuweze kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Mkuu wa wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge akimwagilia mti ambao ameupanda wakati wa zoezi la uzinduzi wa upandaji miti 1,500,000 wilayani humo katika shule ya Sekondari Zanzui.“Tungekuwa tunafanya vizuri kila mwaka kupanda miti 1,500,000 kama alivyoagiza Mheshimiwa Rais wilaya yetu ya Maswa ingekuwa ya kijani kwani agizo hili la serikali ni la muda mrefu takribani miaka 10 lakini utekelezaji wake ni sawa na sifuri,”
“Wilaya yetu miti mingi imekuwa ikikatwa kwa kasi sana sasa tunajukumu la kila mmoja wetu kupitia taasisi na mtu mmoja mmoja tuhakikishe tunapanda miti kwenye maeneo yetu ili tuweze kurejesha uoto wa asili wa wilaya yetu kwa ujumla kwani utunzaji wa mazingira ni kupanda miti,”amesema.
Aidha ameipongeza Halmashauri ya wilaya ya Maswa kwa kutekeleza agizo lake alilolitoa mwaka jana la kutaka iwe na kitalu chake cha miti ambapo kwa sasa miti ya aina mbalimbali imeoteshwa na ndiyo itakayotumika kupandwa katika taasisi zote za serikali pamoja na watu binafsi wilayani humo ili kufikia malengo yaliyowekwa na serikali ya uapandaji wa Miti.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Maswa,Maisha Mtipa amesema kuwa watahakikisha kuwa wanapanda miti 1,500,000 kama agizo agizo la serikali na kwa kuanzia watapanda miti katika taasisi zote za serikali zilizoko chini ya halmashauri hiyo ambazo ni shule za Msingi,Shule za Sekondari,Vituo vya afya na Zahanati.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Maisha Mtipa akipanda mti katika eneo la shule ya Sekondari Zanzui ikiwa ni sehemu ya uzinduzi wa upandaji miti 1,500,000 katika wilaya hiyo.Amesema kuwa kwa kupitia kitalu cha miche ya miti kinachomilikiwa na Halmashauri hiyo wameweza kuotesha miche ya miti ipatayo 421,000 ambayo itapandwa katika taasisi hizo ili waweze kutunza mazingira kwa kuzingatia kuwa wilaya ya Maswa maeneo mengi hayana miti ili kurejesha Uoto wa Asili ambao umepotea.
“Tumefika hapa katika tukio la uzinduzi wa upandaji wa miti sisi kama halmashauri ya wilaya ya Maswa tumetengeza kitalu cha miti na hadi sasa tuna miche ya miti 421,000 ambayo tumeianda kwa ajili ya kutunza mazingira na tutaisambaza katika taasisi zilizo chini ya halmashauri ambazo ni shule za msingi,shule za sekondari,vituo vya afya na zahanati ili ipandwe.
"Kwa kufanya hivi tunaendeleza sera ya serikali ya utunzaji wa mazingira na tukiangalia katika maeneo yetu ya wilaya ya Maswa hayana miti hivyo sisi halmashauri tunafanya kazi kubwa ya kuotesha miti ili kurejesha uoto wa asili,”amesema.
Naye Fabian Mosha ambaye ni Mhifadhi wa Misitu wilaya ya Maswa kutoka Wakala wa Huduma ya Misitu Tanzania(TFS)amesema kuwa kwa mwaka 2023/2024 watateleza agizo la serikali ambalo limetolewa na Rais ya kupanda miti 1,500,000 hivyo katika musimu huu wa mvua watahakikisha miti hiyo inapandwa kama walivyoelekezwa.
Mhifadhi Misitu wa TFS wilaya ya Maswa,Fabian Mosha akikagua Miche katika kitalu cha miti kinachomilikiwa na halmashauri ya Wilaya hiyo kilichopo Kijiji Cha Zanzui.“Kwa niaba ya Kamishina wa Hifadhi Wakala wa Huduma ya Misitu Tanzania kwanza kabisa natoa shukrani kwa kamati nzima ya ulinzi na usalama katika zoezi hili la uzinduzi wa upandaji miti kwa mwaka 2023/2024 umekuwa ni utaratibu wa maagizo yaliyowekwa na Rais kuwa kila mwaka tupande miti 1,500,000 katika kipindi hiki cha mvua watahakikisha wanapanda idadi hiyo ya miti katika wilaya hiyo,”amesema.
Mhifadhi Misitu Wilaya ya Maswa kutoka TFS,Fabian Mosha akipanda mti wakati wa zoezi la uzinduzi wa upandaji miti wilayani humo katika shule ya Sekondari Zanzui.Afisa wa Maliasili,Suzana Buyamba wa halmashauri ya Wilaya ya Maswa akionyesha Miche ya miti ya Malimao ambayo itakwenda kubadilishwa ili itoe matunda ya machungwa. Msimamizi wa kitalu cha Miche ya miti,Emanuel Yehoze katika halmashauri ya Wilaya ya Maswa akitoa maelezo juu ya faida za kupanda miti katika Mazingira yetu.
Post a Comment