DC SERENGETI AWATAKA WALIOJENGA NYUMBA HIFADHI YA BARABARA WAONDOKE
>> Asema barabara ya Mugumu-Tarime ilipimwa Mwaka 1967
>>Wananchi Kijiji cha Nyansurura wasema waliojenga karibu na barabara hakuna atakayesalimika
>>Wasema Kijiji kilianzishwa Mwaka 1974, waiomba Serikali iwaonee huruma iwalipe fidia
Na Dinna Maningo, Serengeti
MKUU wa wilaya ya Serengeti mkoani Mara, Dkt. Vincent Mashinji amewataka wananchi waliojenga nyumba kando kando ya barabara ndani ya Hifadhi ya barabara kuondoka kistaarabu kwakuwa barabara ya Serengeti inayokwenda hadi Tarime ilipimwa Mwaka 1967.
Mkuu huyo wa wilaya ameyasema hayo hivi karibuni wakati wa makabidhiano ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Jembe la nyundo Tarime mjini hadi Mugumu -Serengeti baina ya Wakala wa Barabara Tanzania ( TANROADS) mkoa wa Mara na mkandarasi kampuni ya STECOL Corporation ya China.
Mkuu wa wilaya ya Serengeti mkoani Mara, Dkt. Vincent Mashinji akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Nyansurura
Ujenzi huo utagharimu Tsh. Bilioni 81.146 barabara yenye urefu wa Kilomita 61.
"Naomba zile mita za barabara zilindwe hazikuwekwa kwa bahati mbaya. Hii barabara imepimwa miaka mingi toka 1967.
"Kwahiyo wewe kama barabara ilikukuta tutakuaga kistaarabu ila kama umeikuta barabara utatuaga kistaarabu, kwahiyo yule ambaye ameikuta barabara aanze kuhama polepole mwenyewe" amesema Dkt. Vincent.
Ameongeza kusema " Barabara ni faida kwa watu wote hatujengi barabara la kupitia Dkt. Mashinji peke yake tunajenga barabara yakupita watu wote" amesema.
Mkazi wa Kijiji cha Nyansurura Mhoni Issa amesema Kijiji kilianzishwa 1974 wananchi wakajenga nyumba kwa kutokujua hivyo wameiomba serikali iwaonee huruma iwalipe fidia ili wakatafute maeneo mengine ya kujenga nyumba kwani baadhi yao wana maisha duni hawana fedha za kununua viwanja na kujenga nyumba.
" Kijiji kilianzishwa Mwaka 1974, na wanasema barabara ilipimwa tangu mwaka 1967 hii inaonesha hakuna mwananchi yeyote atakayefidiwa.
"Tunaiomba Serikali yetu sikivu ya mama Samia Suluhu ituhurumie itulipe fidia kwakuwa watu wameishi kwenye hizo ardhi kwa zaidi ya miaka 20 na serikali ilikuwepo inawaona wakiendelea kuishi bila kuwaondoa" amesema Mhoni.
Oteigo Chacha ameongeza kusema " Maisha kwa sasa ni magumu sana hasa ukiangalia mazingira yetu ya vijijini tinategemea kilimo na ufugaji, biashara zetu ni ndogo ndogo sasa unapomwambia mtu abomoe nyumba bila kufidiwa aondoke anaenda kuishi wapi?" amehoji.
"Kuna watu wamejenga karibu na barabara na eneo likaisha hana kipande kingine kuwa abomoe arudi nyumba nje ya eneo la hifadhi ajenge nyumba nyingine, tunaomwomba Rais atuonee huruma wengine ni wajane, wengine ni maskini ukiwaondoa bila kuwalipa unakuwa umewapa mateso makubwa katika maisha yao.
"Yawezekana watu walijenga karibu na barabara kwa kutokujua na wameishi miaka yote basi serikali iliangalie hili kwa jicho pana ili isijekuwa sehemu ya mateso kwa familia zilizojenga nyumba karibu na barabara, barabara iwe ni furaha kwetu na sio kuleta hudhuni "amesema Oteigo.
Akikabidhi Barabara kwa mkandarasi, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania ( TANROADS) mkoa wa Mara, Mhandisi Vedastus Maribe amesema;
Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania ( TANROADS) mkoa wa Mara, Mhandisi Vedastus Maribe (Katikati aliyevaa miwani) akizungumza
"Leo tumekuja kumkabidhi mkandarasi barabara ajenge kwa kiwango cha lami itajegwa na Kampuni ya STECOL Corporation ya China, kwa hiyo Serikali imeanza kazi na ujenzi utagharimu Bilioni 81.146" amesema Meneja.
Ameongeza " Barabara itajengwa kwa viwango vya upana wa barabara itakuwa mita 9.5 ambapo mita 6.5 ni kwa ajili ya magari kupita na Mita 1.5 ni kwa ajili ya watembea kwa miguu. Itajengwa kwa makaravati, madaraja, itakuwa na viwango vya lami nyepesi" amesema Mhandisi Vedastus.
Amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa mkandarasi na kusisitiza kuwa ujenzi utakapoanza wananchi watapata fursa za ajira huku akiwataka kulinda mali zitakazotumika kwenye ujenzi wa barabara.
Post a Comment