MADIWANI SIMIYU WAJIFUNZA MFUMO WA STAKABADHI GHALANI MTWARA
Na Samwel Mwanga, Mtwara
MADIWANI wa kamati ya Fedha,Utawala na Mipango katika halmashauri za wilaya ya Maswa, Bariadi, Itilima,Meatu na Bariadi Mji katika mkoa wa Simiyu wamefanya ziara ya kujifunza.
Ziara hiyo imefanyika katika Halmashauri ya Manispaa ya Mikindani mkoani Mtwara kuhusu mfumo wa uuzaji mazao kupitia stakabadhi ghalani ambao umekua ukinufaisha kwa kuipatia mapato halmashauri hiyo inayotumia mfumo huo.
Baadhi ya madiwani kutoka halmashauri za mkoa wa Simiyu wakiwa kwenye mafunzo ya Mfumo wa stakabadhi ghalani katika Mkutano wa mikutano wa Manispaa ya Mikindani,Mtwara.Hatua hiyo inakuja kufuatia mkoa wa Simiyu kutaka kuanza kutumia mfumo wa mauzo mazao stakabadhi ghalani katika zao la pamba ambapo mkoa wa Ruvuma umefanikiwa kutumia mfumo huo katika zao la korosho na kuwanufaisha wakulima.
Mkuu wa wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, Saimon Simalenga ambaye ndiye alikuwa mkuu wa msafara za ziara hiyo amesema kuwa lengo la ziara yao ni kujifunza kuhusu mfumo wa stakabadhi ghalani kwa madiwani na wataalamu wa halmashauri hizo za mkoa huo.
Hivi karibuni wanategemea kwenda kuanza kuutumia mfumo huo mara baada ya elimu kutolewa na kupitishwa na vikao vya kisheria vikiwemo Baraza la Madiwani.
Amesema kuwa suluhisho la matatizo kwa wakulima wa zao la pamba sambamba na halmashauri za mkoa wa Simiyu kupata mapato ni kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani ambapo mkoa wa Mtwara wanafanikiwa na ndiyo maana wamekwenda kujifunza katika mkoa huo.
“Tumewaleta madiwani na wataalam kutoka mkoa wa Simiyu wajifunze kuhusu mfumo huu wa stakabadhi ghalani kwa kuwa wenzetu ninyi wa mkoa wa Mtwara mmefanikiwa kwa kiwango kikubwa katika zao la korosho ambapo mkulima ananufaika na halmshauri nazo zinanufaika kwa kupata mapato yao ya ndani kupitia mfumo huo” amesema.
Amesema kuwa mkoa wa Simiyu umekuwa ukilima zao la pamba kama zao la biashara lakini mfumo wanaotumia wa zao hilo kwa mkulima kuuza zao lake kwa Chama cha Ushirika cha Msingi(Amcos)ambao na wenyewe kutafuta soko kwa Kampuni umekuwa haumufaishi mkulima pamoja na kuzinyima mapato ya kutosha halmashauri.
Awali Mkuu wa wilaya ya Mtwara,Mwanahamis Munkunda akizungumza na madiwani hao amesema kuwa mfumo huo kwa Halmashauri ya Manispaa ya Mikindani, Mtwara umeleta manufaa kuliko mfumo wa awali ikiwa pamoja na kuongeza mapato ya Halmasahauri hiyo.
Mkuu wa wilaya ya Mtwara, Mwanahamis Munkunda (aliyesimama) akieleza faida ya Mfumo wa uuzaji wa mazao kutumia stakabadhi ghalani kwa madiwani wa mkoa wa Simiyu waliofanya ziara katika Manispaa ya Mikindani,Mtwara aliyeko kulia kwake ni Mkuu wa wilaya ya Itilima,Faidha Salim na kushoto kwake ni Mkuu wa wilaya ya Bariadi,Saimon Simalenga wote kutoka mkoa wa Simiyu.Amesema kuwa wakulima wamepata bei nzuri ya mazao hususani mazao yanayouzwa kupitia mfumo huo sambamba na kuwepo kwa ushirikiano nzuri kwa wadau wa stakabadhi ghalani kwa ngazi zote inapelekea mfumo kufanya kazi vizuri.
"Kuwepo kwa matumizi sahihi ya vipimo vya mizani, ambapo inamsaidia mkulima asinyonywe pindi mkulima anapoleta mazao yake kwenye mfumo
"Pia kuongezeka kwa uamasishaji wa Vyama vya Msingi vya Ushirika navyo vinafanya kazi vizuri na kupelekea kuongezeaka kwa uzalishaji wa mazao yanauzwa kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani" amesema.
Amesema kuwa baada ya wakulima hao kunufaika na mfumo huo wameongeza kasi ya uzalishaji wa mazao yao hivyo kwa kila musimu mazao yamekuwa yakiongezeka maradufu na hivyo kuwafanya awaeze kufaidika vyema na juhudi zao.
Baadhi ya madiwani na viongozi kutoka mkoa wa Simiyu wamesema kuwa mafanikio ya utumiaji wa stakabadhi ghalani kutokana na elimu waliyoipata utawasaidia katika Halmashauri zao ili waweze kuongeza mapato na kumnufaisha mkulima.
”Elimu tuliyoipata ya stakabadhi ghalani itakuwa jawabu,mfumo tunaotumia sasa hata Halmashauri inapoteza mapato lakini sasa tunakwenda kuhamasishana ili tuanze kutumia mfumo huu,”amesema Jeremiah Shigalla (Makondeko)diwani wa Kata ya Zanzui wilaya ya Maswa.
Mkuu wa wilaya ya Meatu mkoani Simiyu, Fauzia Ngatumbura amesema kuwa wamekwenda Mtwara kujifunza baada ya mkoa huo kufanikiwa kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani na kusisitiza kuwa mfumo huo ni mzuri kwani unamnufaisha moja kwa moja mkulima pamoja na halmashauri kutokana na kutokuwepo kwa muda kati yao ambaye anakuwa anatafuta masoko kama ilivyo katika zao la pamba.
Mkuu wa wilaya ya Meatu mkoani Simiyu,Fauzia Ngatumbura (aliyesimama)akitoa Maoni yake juu ya Mfumo wa stakabadhi ghalani katika Ukumbi wa bodi ya Korosho Tanzania mjini Mtwara.“Tunajifunza kwa wenzetu wa Mtwara ambao wamefanya vizuri katika mfumo wa uuzaji wa mazao kwa mfumo wa stakabadhi ghalani tulinganisha na kwenye mkoa wetu ambao tunazalisha zao la pamba bei ya mazao si nzuri naamini kwa kila diwani ambaye tumekuja nao kujifunza na ukizingatia ndiyo wajumbe wa Kamati ya Fedha na Uchumi.
"Kwa elimu hii tuliyoipata na sisi tukaenda kuihubiri kwa wakulima na Vyama vya Ushirika vya Msingi tutafanikiwa,Mimi Mkuu wa wilaya ya Meatu nakwenda kuongoza zoezi hili la utoaji elimi katika wilkaya ninayoiongoza,”amesema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Maisha Mtipa amesema kuwa mfumo huo ukitumiwa vizuri unaweza kusaidia pia kuwepo kwa mifuko mbalimbali ya maendeleio kama vile mifuko ya maendeleo ya Elimu katika wilaya ambayo itasaidia sekta ya elimu katika masuala mbalimbali.
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya Wilaya ya Maswa,Maisha Mtipa akisisitiza jambo kwenye semina ya Stakabadhi ghalani katika Ukumbi wa Manispaa ya Mikindani,Mtwara.Ziara hiyo iliyoanza Oktoba 30 hadi Novemba 1 mwaka huu ambapo madiwani hao walipata taarifa kutoka kwa wataalam wa kilimo na ushirika wa Manispaa hiyo jinsi ya mfumo huo unavyowanufaisha Wakulima na kuongeza mapato katika halmashauri.
Pia walipata nafasi ya kutembelea Makao Makuu ya Bodi ya Korosho Tanzania,Amcos ya Muungano ya Mikindani,Ghala la kuhifadhi Korosho la MCC na Olam,Kiwanda cha kubangulia Korosho cha reli na Bandari ya Mtwara.
Mkuu wa wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu,Aswege Kaminyoge(mwenye miwani)aliangalia jinsi Korosho zinavyomenywa kwenye kiwanda Cha kubangua Korosho Cha Olam kilichoko mjini Mtwara. Baadhi ya Viongozi na Madiwani wa wilaya za mkoa wa Simiyu walipotembelea Bandari ya Mtwara kuona jinsi inavyofanya kazi.
Post a Comment