HEADER AD

HEADER AD

SERIKALI YANUNUA VIFAA TIBA VYA MILIONI 300 ITILIMA

>> CCM Simiyu yavutiwa na wingi wa miradi ya maendeleo

>> Serikali ya awamu ya sita yapongezwa


Na Samwel Mwanga, Itilima

VIFAA Tiba vyenye thamani ya Tsh. Milioni 300 vimenunuliwa katika Zahanati,Vituo vya Afya na Hospitali katika wilaya ya Itilima mkoa wa Simiyu ili kuboresha upatikanaji wa huduma za afya.

Hayo yameelezwa Novemba 24 mwaka huu na Mganga Mkuu wa wilaya ya Itilima, Dr Emanuel Costantine wakati akisoma taarifa ya utekelezaji wa ununuzi wa vifaa tiba kwa wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi(CCM) wakati wa ziara ya kutembelea Hospitali ya wilaya hiyo iliyoko maeneo ya Nguno ili kuona sehemu ya vifaa hivyo vilivyonunuliwa.


Amesema kuwa katika bajeti ya halmashauri ya wilaya hiyo kwa mwaka wa fedha 2022/2023 katika bajeti yake ilitenga kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba kwa mchanganuo kuwa vifaa vya Zahanati ni Tsh Milioni 50,Vituo vya afya Sh 150 na Hospitali Sh Milioni 100.

Dr Costantine amesema kuwa kupatikana kwa vifaa hivyo kulitokana  na kuidhinishwa na  vikao vya Timu ya Uendeshaji huduma za Afya Wilaya (CHMT) na timu ya uendeshaji shughuli za Wilaya(CMT) na Kamati ya Fedha ya Halmashauri ya wilaya ya Itilima.

Akielezea mchanganuo wa vifaa tiba vilivyonunuliwa amesema kuwa Vifaa hivyo ni pamoja na Vifaa vya Meno vyenye thamani ya  Milioni 49.9,Vifaa vya macho vyenye thamani ya Sh Milioni 49.9 na Kituo cha afya Ikindilo Sh Milioni 14.

       Mganga Mkuu wa wilaya ya Itilima,Dr Emanuel Constantine(aliye kati)akitoa maelezo ya Vifaa tiba vya kutibu macho kwa Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu,Shemsa Mohamed (wa kwanza kushoto)katika hospitali ya Wilaya hiyo

Vifaa tiba vingine vilivyonunuliwa ni pamoja na kwenye Kituo cha afya Nkoma vyenye thamani ya Tsh. Milioni 36.8, Kituo cha afya Mwanhunda Tsh. Milioni 69.2, Zahanati ya Senani Tsh. Milioni 19.9 na Zahanati ya Tembo Longalombogo Tsh. Milioni 29.7 na vifaa tiba vyote vimekwisha pokelewa .

“Kwa sasa katika hospitali yetu ya wilaya ya Itilima tumeanza kutoa huduma ya kinywa na meno pamoja na huduma ya macho baada ya kupata vifaa hivi ambavyo tumevinunua baada ya kupata fedha kutoka serikali inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu.

“Tunahaidi kuendelea kuvitunza vifaa hivyo ili huduma iendelee kutolewa hapa wilayani kwetu na kuwapunguzia wananchi gharama za kufuata huduma za afya katika wilaya jirani.”amesema.

Amesema kuwa kiasi cha fedha Tsh. Milioni 2.7 zilizobaki wakati wa ununuzi wa vifaa hivyo zitatumika katika mwaka wa fedha 2023/2023 na tayari kwa sasa wamepokea kiasi cha fedha Tsh Milioni 400 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba.

       Mganga Mkuu wa wilaya ya Itilima,Dr Emanuel Constantine(,mwenye koti jeusi)akitoa maelezo ya Vifaa tiba katika hospitali ya wilaya ya Itilima kwa Viongozi wa Serikali na Viongozi wa CCM

Aidha hospitali hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto  mbalimbali zikiwemo kutokuwa na uzio,kutokuwa na barabara za kuhamisha wagonjwa (walk way)kutoka sehemu moja kwenda nyingine na kutokuwa na nyumba za watumishi kwani kuna nyumba moja tu.

Mbunge wa jimbo la Itilima, Njalu Silanga amempongeza Rais Dkt Samia Suluhu kwa kuendelea kujali afya za wananchi wa wilaya hiyo kwa kuwapatia fedha za ununuzi wa dawa na vifaa tiba pamoja na kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya.

      Mbunge wa Jimbo la Itilima,Njalu Silanga(wa kwanza kulia)akizungumza na wananchi katika hospitali ya Wilaya ya Itilima

Amesema kuwa ni vizuri kwa watumishi wa hospitali hiyo kuvitumia vifaa hivyo hasa vya macho pamoja na meno kwa malengo yaliyokusudiwa  ili kuweza kuboresha afya za wananchi wa wilaya hiyo.

Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu, Shemsa Mohamed amesema kuwa serikali ya awamu ya sita imekuwa ikitumia fedha nyingi katika sekta ya afya kwa lengo kutoa huduma bora za afya kwa wananchi.

           Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu,Shemsa Mohamed akizungumza na wananchi(hawapo pichani,)kwenye hospitali ya Wilaya ya Itilima.

Amesema licha ya hospitali hiyo kuwa na idadi ndogo  ya watumishi katika kada mbalimbali hivyo amewaomba kutumia lugha nzuri kwa wagonjwa wanapofika  katika hospitali hiyo kupata huduma huku akimuagiza Mkuu wa mkoa wa Simiyu kuhakikisha hospitali hiyo inapata watumishi wa kutosha.

“Tunajua mko wachache watumishi katika hospitali hii kwa kada tofauti tofauti hivyo niwaombe pamoja na hali hiyo  fanyeni kazi zenu vizuri pia tumieni lugha nzuri za upendo kwa wagonjwa wenu,”amesema.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu,Dkt Yahaya Nawanda amemuomba Mwenyekiti huyo wa CCM mkoa kusaidiana naye suala la kupata watumishi wa Afya katika Hospitali zote za Wilaya za mkoa huo kwani bado zina upungufu kwa kada mbalimbali.

      Mkuu wa mkoa wa Simiyu,Dkt Yahaya Nawanda(aliye kati)akitoa maelezo kwa Mwenyekiti wa CCM mkoa hu,Shemsa Mohamed(wa kwanza kulia) wakiwa kwenye Hospitali ya Wilaya ya Itilima.

Pia amehaidi kusimamia matumizi sahihi ya vifaa hivyo pamoja na kutatua changamoto zilizopo kwenye Hospitali huku akihaidi kusimamia kutolewa kwa huduma bora katika hospitali hiyo.

“Nikuombe mheshimiwa Mwenyekiti  si orodha ya Itilima tu bali ya kimkoa nawe uweze kusukuma kwa njia zako unazojua maana kuna mahali wengine sisi hatufiki ila wewe unafika ili suala la walk way mimi pamoja na Mkuu wa wilaya ya Itilima na Mkurugenzi wa halmashauri hii tutaliweka kwenye mipango yetu na bahati nzuri na mbunge yuko hapa “

“Mheshimiwa Mwenyekiti mimi nikuombe nikushukuru tena,Mheshimiwa Rais ametuletea hizo Sh Milioni 300 tumenunua vifaa tiba, mimi naomba nikuhakikishie tutatoa huduma nzuri kwa wananchi lakini watumishi ambao walioko chini yangu lugha yetu itaendelea kuwa nzuri sana na kwa sababu kutibu pia ni lugha mgonjwa ukimpa lugha nzuri kama ulivyotuasa basi sisi tutaendeleza mazuri yote na mimi nitatekeleza maagizo yako,”amesema.

Katika hatua nyingine Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu,Shemsha Mohamed amemkabidhi  Mkuu wa mkoa wa Simiyu,Dkt Yahaya Nawanda gari la wagonjwa lililotolewa na Serikali ambalo litatumika katika kituo cha Afya Mwanunda kilichoko katika wilaya ya Itilima.

Hafla fupi ya makabidhiano hayo yamefanyika katika kituo hicho cha afya na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali Serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM)wa mkoa wa Simiyu na wilaya ya Itilima pamoja na wananchi.

         Moja ya Majengo katika Hospitali ya wilaya ya Itilima mkoa wa Simiyu ambayo hayana uzio.

        Mkuu wa mkoa wa Simiyu,Dk Yahaya Nawanda(wa kwanza kulia) akiwa na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu,Shemsa Mohamed wakifurahia gari jipya la kubebea wagonjwa katika Kituo Cha Afya Mwanunda

No comments