RC MARA : UCHUMI IMARA UNATENGENEZA TAIFA IMARA, WAFANYABIASHARA WENYE MAKAMPUNI LIPENI KODI
>Aipongeza Kampuni ya Barrick kwa ulipaji mzuri wa Kodi
Na Dinna Maningo, Tarime
MKUU wa mkoa wa Mara Said Mtanda ameyataka makampuni yaliyopo mkoani Mara kulipa kodi kwa wakati bila kukwepa kwa kile alichoeleza kwamba hakuna Taifa imara kama hakuna uchumi imara.
Amesema uchumi imara ndiyo utengeneza Taifa imara hivyo wafanyabiashara wenye makampuni wanatakiwa kulipa Kodi kwa wakati ili Taifa liwe na uchumi imara
RC Mtanda ameyasema hayo Novemba,23, 2023 wakati akizindua mafunzo ya siku mbili ya uendeshaji biashara kwa wafanyabiashara wa mkoa wa Mara yaliyoandaliwa na Mgodi wa dhahabu wa Barrick North Mara ambapo wawezeshaji wa mafunzo hayo ni kutoka Kampuni ya Impacten Afrika limited.
RC Mtanda amesema mgodi wa Barrick North Mara ni miongoni mwa walipa kodi wakubwa Tanzania kupitia Kampuni yao ya uchimbaji wa Dhahabu.
" Kila mtu anafahamu kuwa kodi ndiyo uchumi wa nchi kwahiyo niendelee kutoa msisitizo juu ya ulipaji wa kodi na kwakuwa ninyi ni wafanyabiashara wazalendo na mafunzo haya mnayoyapata yawe chachu kwenu na mshirikiane na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuweza kulipa kodi" amesema Mtanda.
Pia amesisitiza kutoa risiti halali za mashine za EFD na kupewa risiti halali baada ya ulipaji kodi na wasifanye udanganyifu kwani kufanya hivyo ni kuikosesha serikali mapato.
"Tuna changamoto kubwa kwa wenzetu wa mapato, wapo watu wengine wamejitengenezea mashine zao feki wanawauzia watu risiti.suala la namna hiyo linaikosesha serikali Mapato"
" Taifa likiwa halina uwezo wa kujitosheleza katika mahitaji yake haliwezi kuwa Taifa endelevu na uchumi wa Taifa letu utajengwa na watanzania wenyewe ndiyo watu wa kwanza kujenga uchumi wa nchi yao na wajenzi sio wengine ni ninyi" amesema.
Amewataka wafanyabiashara kukumbushana wajibu wa kulipa kodi huku akizidi kuipongeza kampuni ya Barrick kwa ulipaji mzuri wa kodi.
" Nakumbuka hivi karibuni upo mkataba wa utoaji fedha baina ya serikali na mgodi wa Barrick Tsh.Bilioni 70 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya elimu nchini.
"Katika mkoa wa wetu wa Mara yapo mabweni ya kidato cha tano na cha sita katika kila Wilaya ambao unafadhiliwa kutokana na mradi huu wa Bilioni 70 ambao ni mkataba na Rais wetu na Kampuni ya Barrick kwa ajili ya kuboresha sekta hiyo nchini." amesema Kiongozi huyo.
Ameushukuru Mgodi wa North Mara kwa kukukusanya wafanyabiashara na makampuni mbalimbali ili waweze kushiriki katika mkutano wa ukuzaji uchumi kupitia elimu ya biashara.
Kaimu Meneja wa Mgodi wa Barrick North Mara Hermence Christopher Lulah amesema Kampuni ya Barrick North Mara ni walipa kodi na kwa mwaka huu kampuni imeshika namba moja kama walipa kodi bora.
" Manufaa mengine ni fedha ambazo mgodi wa North Mara Barrick umetoa kwenye makampuni yaliyowekeza kwetu yakiwemo ya wazawa. Kwa mwaka huu kumekuwa na ongezeko la fedha zilizotolewa kwa makampuni kiasi cha Dola Milioni 29 ambazo zimekwenda kwenye makampuni" amesema.
Ameongeza kuwa mgodi unaendelea kutoa fursa hizo chamsingi kampuni hizo ziwe zimekidhi vigezo vinavyotakiwa vya uombaji zabuni mgodini.
Walioketi mbele ni Wafanyakazi wa kampuni ya Rin co.ltd wakisikiliza mafunzo, katikati ni Mkurugenzi wa kampuni huyo Isaack Range.
Akizungumzia mafunzo ya kukuza biashara yaliyotolewa kwa wafanyabiashara na makampuni, amesema kuwa wameanzisha programu ya kuwajengea uwezo wafanyabiashara wa makampuni na wajasiliamali.
Amesema mafunzo hayo ni kwa ngazi zote za wafanyabiashara wakubwa na wadogo ambayo yalianzishwa mwaka 2021 ambapo makampuni 50 yalituma maombi na makampuni 20 yalishiriki mafunzo na makampuni 15 yalitunukiwa vyeti kwa kuhitimu mafunzo.
Amesema kwa mwaka huu wa 2023/2024 wafanyabiashara 47 mkoani Mara wametuma maombi na wameshiriki mafunzo ya uendeshaji wa biashara yaliyofanyika Novemba,2023 hadi Novemba, 24,2023 katika ukumbi wa Blue Sky mjini Tarime.
Post a Comment