SERIKALI NA UTEKELEZAJI WA ILANI UJENZI WA BARABARA YA LAMI TARIME- SERENGETI
>>Ibara ya 55 ya Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025, inaielekeza Serikali kujenga barabara ya Tarime- Mugumu Kilomita 87 kwa kiwango cha Lami
>> Katika kutekeleza Ilani ya CCM, Serikali imetoa Tsh. Bilioni 81.146 kujenga kipande cha barabara Tarime-Mogabiri, Nyamongo-Mugumu.
>> TANROADS Mara yamkabidhi barabara Mkandarasi kampuni ya STECOL ya China
>> Dc Tarime asisitiza mradi ukamilike kwa wakati.
Na Dinna Maningo, Tarime
SERIKALI ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa fedha Tsh. Bilioni 81.146 kwa ajili ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha Lami kutoka Wilayani Tarime hadi Mugumu Wilayani Serengeti mkoa wa Mara yenye urefu wa Kilomita 61 itakayojengwa kwa kipindi cha miaka miwili.
Barabara hiyo itajegwa na Kampuni ya STECOL Corporation ya China, kipande cha kutoka Jembe la Nyundo Tarime mjini hadi Mogabiri yenye urefu wa (km 9.3) na kutoka Kwinogo - Nyamongo hadi Mugumu Serengeti (km 51.75).
Kipande kingine cha ujenzi wa barabara kutoka Mogabiri hadi Nyamongo chenye urefu wa (km) 25 kinachogharimu zaidi ya Tsh. Bilioni 34.6 ujenzi wake unaendelea, barabara inayojengwa na Kampuni ya ujenzi ya Nyanza Road Works Limited ya hapa nchini.
Hatua hiyo ni utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2020-2025. Ibara ya 55 inaielekeza Serikali katika kipindi cha miaka 5 Serikali ijenge na kukarabati barabara ya Tarime - Mugumu (km 87) kwa kiwango cha lami.
Akizungumza eneo la jembe la Nyundo Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania ( TANROADS) mkoa wa Mara, Mhandisi Vedastus Maribe amesema;
"Hiki Kipande cha kutoka Jembe la Nyundo -Mogabiri na Nyamongo -Mugumu kilikuwa hakijapata mkandarasi, serikali imeshampata mkandarasi kampuni ya STECOL CORPORATION LTD ya China.
"Leo tumekuja kumkabidhi mkandarasi barabara aanze kazi ya ujenzi. Nakumbuka wananchi wa eneo hili nyumba zilipobomolewa walilalamika kuwa mbona ujenzi hauanzi?, kwa hiyo Serikali imeanza kazi na ujenzi utagharimu Bilioni 81.146" amesema Meneja.
Meneja ameongeza " Barabara itajengwa kwa viwango vya upana wa barabara itakuwa mita 9.5 ambapo mita 6.5 ni kwa ajili ya magari kupita na mita 1.5 ni kwa ajili ya watembea kwa miguu. Itajengwa kwa makaravati, madaraja, itakuwa na viwango vya lami nyepesi" amesema Mhandisi Vedastus.
Kauli ya DC Tarime
Mkuu wa Wilaya ya Tarime Kanali Michael Mntenjele ameishukuru Serikali kutoka fedha za ujenzi huku akimtaka mkandarasi kutimiza kazi kwa wakati kama mkataba wake unavyomtaka na amesisitiza ujenzi uanzie mjini Tarime kwakuwa ni mjini wenye watu wengi.
Mkuu wa Wilaya ya Tarime Kanali Michael Mntenjele katikati akiwa na viongozi wengine akizungumza makabidhiano ya barabara
"Kipande hiki kutoka jembe la Nyundo hadi Mogabiri na Nyamongo-Mugumu sisi tunamtaka mkandarasi kutimiza kazi yake kwa wakati, ni kipande kidogo sana atumie muda vizuri kukamilisha maana hapa ni mjini na kuna watu wengi, wakamilishe kwanza hiki kipande cha mjini alafu waendelee na kwingine" amesema.
DC Michael amesema ujenzi huo uwe wa kiwango ambacho kimekubalika kulingana na mkataba na mradi ukamilike kwa wakati.
Amesema barabara hiyo ni muhimu sana kwa watalii wanaotokea Kenya kupita barabara hiyo kwenda kutalii hifadhi ya Serengeti ambapo ukikamilika utasaidia utalii kukua zaidi.
Amewaomba wananchi wa Tarime kutoa ushirikiano na wasifanye udokozi wa mali kwani utarudisha nyuma mradi na watoe taarifa mapema ili watakojihusisha na uhalifu wachukuliwe hatua.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime Petro Kurate amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fedha za kutekeleza miradi mikubwa kwenye halmashauri hiyo.
" Tunamshukuru Rais Samia kutuletea miradi mikubwa, nina mhakikishia mkandarasi kuwa usalama na amani upo wa kutosha.
"Naomba mnapopewa kazi mjitahidi kumaliza kwa wakati kwasababu watu hupewa kazi lakini inachukua muda mrefu kuisha na hivyo kuleta changamoto" amesema.
Mwendesha pikipiki mkazi wa Kijiji cha Kewanja, Mnanka Ikwabe amesema wamesubiri sana barabara ya lami kwani barabara ya vumbi imekuwa ikiwapa changamoto na kwamba ikijengwa wataepukana na vumbi.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Murito- Nyamongo, Chacha Ryoba Irondo ameishukuru Serikali, TANROADS, Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini Mwita Waitara na Diwani wa Kata ya Kemambo Rashid Bogomba kwa mradi huo.
Amewaomba viongozi wa Serikali ya Kijiji cha Kerende na Kewanja kutoa ushirikiano kwa mkandarasi na kwamba Kijiji hicho kimetoa eneo la kujenga kambi kwa ajili ya mkandarasi anayejenga barabara hiyo.
Mkazi wa Kijiji cha Murito Joseph Mangure amesema barabara hiyo imekuwa ikileta shida kwa wasafiri wa Tarime- Serengeti hivyo ikiwekwa lami itarahisisha usafiri.
Katibu wa Mbunge, Paskali Mkapa ameipongeza Serikali ya awamu ya sita kwa kusikiliza kilio cha wananchi cha barabara ya Tarime - Mugumu kujengwa kwa kiwango cha Lami.
"Hii ni historia barabara kujengwa kwa kiwango cha lami nampongeza Meneja TANROADS mkoa wa Mara kwa kazi nzuri katika ujenzi wa miundombinu ya barabara. Naomba kuwepo ushirikiano kati ya mkandarasi na vijiji ambako mradi unatekelezwa " amesema Paskali.
Katibu wa Chama cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Tarime, Novertus Kibaji ameipongeza Serikali na Rais Samia kwa kazi kubwa inayoendelea ya utekelezaji wa miradi huku akiomba wilaya ya Tarime iwe mkoa wa kiserikali.
" Tunashuhudia ujenzi kwa kiwango cha lami, shukrani zetu kwa Rais, Wabunge ambao wamekuwa wakiisukuma serikali katika utekelezaji wa miradi. Barabara hii ikikamilika na zile km 18 za mjini ni hakika mji utakuwa mzuri zaidi .
" Niombe mkandarasi kazi ifanyike kwa wakati, tunahitaji kuona matokeo chanya kwa haraka zaidi. Wilaya yetu ina hadhi ya kuwa mkoa wa kiserikali, tunaomba iwe mkoa badala ya kuwa wilaya" amesema Novertus.
Ilani ya CCM
Ilani ya Uchaguzi ya 2020- 2025 ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Ibara ya 50 inasema Chama kinatambua umuhimu wa ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya barabara, uchukuzi, mawasiliano kwa lengo la kuwezesha ujenzi wa uchumi imara unaojitegemea.
Pia manufaa ya sekta hii ni pamoja na Kuboresha maisha ya watanzania kwa kuwawezesha usafiri na usafirishaji wa bidhaa, kuongezeka kwa matumizi ya fursa za kijiografia na mapato nchini.
Ibara ya 55 ya Ilani hiyo inasema Chama cha Mapinduzi kitaielekeza Serikali kuendeleza shughuli za ujenzi wa miundombinu mbalimbali ili kuifanya sekta ya ujenzi ifikie malengo yake ya kuwezesha wananchi kuendelea na uzalishaji kwa ajili ya kuongeza kipato chao ambapo pia imeelekeza Serikali kujenga Barabara ya lami ya Tarime - Mugumu ( km 87) kama inavyoelezwa katika ibara hiyo.
Barabara inayopita Kijiji cha Murito kwenda Mugumu -Serengeti
Post a Comment