HEADER AD

HEADER AD

CCM YAIAGIZA BARRICK KUCHANGIA MILIONI 150 UJENZI JENGO LA MAMA NA MTOTO NYAMONGO


>>Ni baada ya Barrick North Mara kuahidi kuchangia Milioni 350 fedha za CSR

>>Mwenyekiti CCM Mara asema Mgodi kuchangia CSR ni wajibu hivyo mbali na pesa hizo lazima wachangie Milioni 150

>>Diwani Kata ya Matongo asema  Mgodi usikwepe kuchangia ujenzi kwani Milioni 350 ni fedha za CSR zilizopitishwa na vijiji kusaidia kituo cha afya

>>Chandi aendesha harambee na kufanikisha kupatikana Tsh. Milioni 18,  ahadi zaidi ya Milioni 583 mifuko ya saruji 600, na tripu 10 za mawe.

Na Dinna Maningo, Nyamongo

MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi ( CCM) mkoa wa Mara, Patrick Chandi ameuagiza uongozi wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara uliopo Nyamongo, Wilaya ya Tarime mkoa wa Mara, kuhakikisha  unatoa fedha Tsh. Milioni 150 kuchangia ujenzi wa jengo la mama na mtoto katika Kituo cha Afya Nyangoto maarufu Sungusungu.

Mwenyekiti huyo wa CCM ametoa agizo hilo Desemba, 15, 2023 wakati alipokuwa mgeni rasmi katika harambee ya kuchangia ujenzi wa jengo la Mama na Mtoto.

   Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi ( CCM) mkoa wa Mara, Patrick Chandi akizungumza wakati wa harambee ya kuchangia Jengo la mama na mtoto.

Harambee hiyo iliandaliwa na Mwanamke mzawa wa Nyamongo Emmyliana Julius Range ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la kiserikali la Heath and Safe Delivery Foundation (HSF) lenye makao yake makuu Nyamongo.

Agizo la Mwenyekiti limekuja baada ya wawakilishi kutoka mgodi wa Barrick North Mara kuahidi kuwa mgodi utachangia Tsh.Milioni 350 fedha ambazo ni za mpango wa uwajibikaji wa makampuni kwa Jamii CRS kutoka katika Mgodi huo.

"Tunapenda kumpongeza Mkurugenzi wa HSF kwa jambo hili la kuchangia ujenzi tunamuunga mkono kupitia mpango wa CSR wa mwaka 2023/2024, Mgodi hutatoa Tsh. Milioni 350 ambapo tunaamini utaanza kutekelezwa mwakani, fedha hizo zitatolewa kama njia mojawapo ya kumsapoti Emmy" alisema Happness kutoka mgodi huo.

Diwani wa Kata ya Matongo Godfrey Kegoye akasimama na kusema " Nataka hieleweke vizuri Mh. mgeni rasmi, nilitamani nje ya CSR ambayo pesa hiyo tulikaa kwenye WDC fedha inayotakiwa iingie kwenye vijiji vinne tukasema tuchangie kile kituo cha afya hiyo Milioni 350.

        Walioketi mbele ni Madiwani WA Halmashauri ya wilaya ya Tarime wakiwa kwenye harambee

" Ni kweli inatoka mgodi wa Barrick kwa gawiwo la CSR tunataka watuambie mbali na gawio hilo Barrick inatuchangia nini kama sisi tulivyofika kuchangia?

Mwakilishi wa Meneja Mahusiano wa mgodi huo aliyetambulishwa kwa jina moja la Zakayo alisema" 

" Niseme kwamba kwa maelezo ambayo Happnes ameongea kwa niaba ya Meneja Mahusiano wa mgodi ni kwamba Barrick kupitia mpango wa CSR tulikuwa tumekubaliana katika utekelezaji wa mwakani zitengwe hizo Milioni 350 kwa ajili ya kukipatia Kituo cha Afya cha Sungusungu.

"Kwasababu sisi siyo wasemaji wa kampuni niseme kwamba Mh. Diwani tunayachukua haya maagizo tutayafikisha kwa Meneja wa Mahusinao" alisema Zakayo.

Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mara alisema " Natoa agizo nyie wawakilishi wa mgodi nenda mtuchangie Milioni 150 peleka hizo taarifa mgodini" alisema Chandi.

Diwani Matongo afunguka

Diwani Godfrey Kegoye amesikitishwa kwa kitendo cha mgodi kusema imechangia Milioni 350 licha ya kwamba fedha hizo ni za vijiji zilizopangiwa matumizi na vijiji kwa ajili ya Kituo cha Afya Nyangoto.

Walioketi mbele ni Madiwani WA Halmashauri ya wilaya ya Tarime wakiwa kwenye harambee

"Barrick walivyosimama kuongea nilisikitika sana hiyo pesa inatoka Kata yangu ya Matongo yenye vijiji vinne nikaomba kila Kijiji kulingana na umuhimu wa afya ichangie Milioni 75 na ndiyo hiyo wamekuja hapa wanaisema ambayo ni Milioni 350 tuliyokaa WDC tukasema tuchangie kituo chetu cha afya.

" Hivyo sisi kama Kata ya Matongo tutachagia hiyo Milioni 350 kwa ajili ya Kituo cha Afya. Nimpongeze Mwenyekiti wa Kijiji cha mjini kati amekuwa msikivu sana tulipoingia madarakani tulikuta kile kituo kina changamoto nyingi lakini kila nikienda Serikali ya Kijiji cha mjini Kati inanisikiliza na kutekeleza.

Diwani ameongeza kusema " Nilienda mara ya kwanza tukawaomba wakatupatia fedha tumejenga Mochari nzuri imekamilika lakini sikuchoka niliomba tena mjini kati tupate Jokofu wakatoa fedha na Jokofu limefika, hivyo tunaona ni jinsi gani tunaendeleza Kituo chetu cha afya.


Diwani huyo alisema anamuunga mkono Mkurugenzi wa HSF na kuahidi kuchangia Milioni tano huku Diwani wa Kata ya Kemambo Rashid Bogomba akiahidi kuchangia  Milioni mbili, Diwani wa Viti maalumu Mariam Mkono alitoa laki moja taslimu ambapo alitoa fedha Tsh. laki mbili akimwalikisha Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Tarime Samwel  Kilesi huku mzazi wa Emmyliana akitoa Milioni mbili.

Katika harambee hiyo Mwenyekiti wa CCM mkoa huo Patrick Chandi alichangia Milioni tano taslimu ambapo amempongeza Mkurugenzi wa HSF kwa wazo lake la ujenzi wa jengo la mama na mtoto.

" Kiukweli Nyamongo tunaitamani siye tuliopo Serengeti, lakini ukija Nyamongo haina hospitali nzuri kama ya wilaya ya Serengeti ambayo ina hospitali nzuri. Zamani tulikuwa tunadhalau watoto wa kike lakini sasa hivi watoto wa kike wanawapiga fimbo watoto wa kiume.

       Mwenyekiti CCM mkoa WA Mara Patrick Chandi ( kushoto) akiteta jambo na Mwenyekiti Wazazi mkoa wa Mara

" Mama endelea na moyo huo, ulinijia pale mkoani ukanieleza habari nzima na uchungu unaokuumiza kutokana na akina mama wanavyopata shida wanalala wawiliwawili kwenye kitanda.

Ameongeza " Sasa nimefika mwenyewe nataka changamoto hiyo iishe tupate jengo la mama na mtoto. Nishukuru kwa taarifa kwamba jengo litagharimu zaidi ya Bilioni mbili na ramani yake ni nzuri ina mvuto.

" Mimi nachangia Milioni tano keshi, kuna rafiki zangu wameniahidi kuniunga mkono kuchangia fedha za ujenzi. Mbunge ameahidi Milioni moja, Kiribo Milioni 2, PKM Milioni 2, Stanley Milioni 2, Gody Kubyo Milioni 2 , Gachuma Milioni 2, Wambura Ryoba Milioni 2, RIN Milioni 2, NBC Milioni 2, Damu ya Mara Milioni 2, Peter Zakaria Milioni 2, Eliachim Maswi Milioni 1.5 na Tindo Milioni moja. 

Chandi aliahidi kuwa ataendelea kuisisitiza Serikali kuhakikisha inachangia ujenzi huo ili kuunga juhudi za Rais Samia Suluhu katika sekta ya afya.

     Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi ( CCM) mkoa wa Mara, Patrick Chandi

"Yale ambayo hayatafanikiwa nitayachukua na kupeleka kwa Waziri wa afya naye atafute pesa kuhakikisha jengo linakamilika .

" Kama wananchi wameamua kufanya jambo lao alafu Chama kisiwaunge tutakuwa tumewakosea sana, mimi ni mkubwa kwa hiyo usihuzunike kuwa DC hayupo Mkurugenzi wa Halmashauri hayupo nitawaagiza kuna mambo ambayo nao watayasimamia, nikuombe usife moyo serikali ya mkoa ipo pamoja na wewe" alisema.

Nicodemas Keryaro ashangazwa viongozi wa Serikali kukacha harambee

Watu mbalimbali wakiwemo wakandarasi wameahidi kuchangia fedha, miongoni mwao ni Nicodemas Keryaro aliahidi kuchangia Milioni tano.

        Nicodemas Keryaro

" Taasisi ya HSF imefanya jambo zuri Chama cha Mapinduzi kina haki ya kuisaidia Nyamongo kupata afya iliyokamilika , Nyamongo ni sehemu inayotoa pato kubwa kwa Serikali, nilitamani kwenye hii harambee ningemuona DMO.

"Nilitamani ningemwona Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Tarime, nilitamani ningemwona mbunge, nilitamani ningemwona Mwenyekiti wa CCM wilaya kwasababu Emmy anamsaidia Rais, anamsaidia Mbunge Waitara katika kuhakikisha akina mama wanapata huduma nzuri" alisema Nicodemas.

Josephat Mwita atamani auone mkataba wa awali kuhusu kituo cha afya

Josephat Mwita mkazi wa Nyamongo aliyewahi kufanya kazi Mgodi wa North Mara amesema mkataba wa awali mgodi ulitakiwa kujenga Kituo cha Afya Nyangoto kwa hadhi ya hospitali ya wilaya lakini haikufanyika hivyo.

              Josephat Mwita

" Mgodi wa North Mara watambue kwamba wakati tunaingia mkataba wa awali na mimi nilikuwa timu ya North Mara wakati huo, mkataba ulikuwa ni kwamba hospitali ya sungusungu itajengwa na mgodi kwa hadhi ya wilaya ndivyo mkataba ulivyosema.

" Natamani kama ule mkataba ungeweza kutolewa uoneshwe tena, na walikuwa wanasema kwamba wangeleta vifaa na Wataalam kutoka nje kusudi hospitali ya Sungusungu ihudumie na mgodi wa North Mara, lakini mambo yalikuja kubadilika sijui kwa vipi, tunaona hospitali ya Sungusungu wakaitelekeza  haikuwa na Mochari, jengo la mama na mtoto" alisema Josephat.

Josephat alichangia Tsh.500,000 na kuahidi kuchangia tena Milioni 4.5, ambapo John Marecho na familia yake aliahidi kutoa mifuko 100 ya saruji ya Twiga Plus na Lori 10 za mawe, Kampuni ya Kemanyaki iliahidi kuchangia tofari 1000 na mifuko 50 ya Saruji, Kampuni ya Trust Fund iliahidi kuchangia Milioni tatu.

Wengine ni kampuni ya ZAPCO iliyotoa Milioni tano taslimu na kuahidi kutoa Milioni tano zingine,Magau Marwa Ryoba aliahidi kutoa Milioni 10, Calvin Mroni aliahidi Milioni 3, Remmy Machage aliahidi Milioni 5, Hussein Mwinyi Milioni moja.


Mkurugenzi wa Mara Online amechangia 200,000 , Ofisi ya DIMA Online imechangia 100,000, Bibi Enock amechangia 40,000 pamoja na wengineo walioahidi kuchangia kiasi cha fedha ujenzi wa jengo hilo, Benadeta Julius Range Milioni 2, Emmanuel Julius Range Milioni 5.

Katika harambee hiyo jumla ya fedha  Milioni 18.9 Taslimu zilichangwa, ahadi Milioni 583, mifuko ya saruji 690 na mawe tripu 10 huku Mkurugenzi wa  Taasisi ya HSF akichangia Milioni 10.

Mwandaaji wa gharama za ujenzi wa jengo hilo Mbaruku Renatus alisema wamedizaini mradi huo kwa kushirikiana na wadau wengine utakaogharimu Bilioni 2.97.

          Mfano wa jengo linalotarajiwa kujengwa la mama na mtoto kituo cha afya Nyangoto.

"Jengo letu ni la ghorofa moja, urefu ni nusu kiwanja cha mpira, upana mita 25, itakuwa na wodi, chumba cha upasuaji n.k, kati ya fedha hizo Milioni 39 zitatumika katika hatua ya awali, kazi ya msingi na kumwaga zege ya chini mpaka kukamilika msingi ni Milioni 210.

"Ujenzi chini hadi juu Milioni 600, kupaua Milioni 40, milango Milioni 117, umaliziaji wa jengo Milioni 192, upakaji wa rangi na kupendezesha Milioni 50, vifaa Milioni 60, dharura Milioni 78, gharama za ufundi Milioni 260

Mkurugenzi HSF Emmyliana Range amemshukuru Mwenyekiti CCM mkoa na na msafara wake pamoja na watu wote walioguswa kuchangia na kusema kuwa anatamani kuona akina mama wanajifungulia kwenye jengo la kisasa na watoto wanapata huduma bora na kwamba harambee hiyo ni enderevu lengo ni kuhakikisha jengo linakamilika na kutoa huduma.

      Emmyliana Julius Range ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la kiserikali la Heath and Safe Delivery Foundation (HSF)









No comments