HEADER AD

HEADER AD

WAZIRI TAMISEMI AAGIZA KUTENGULIWA MGANGA MKUU MKOA WA KAGERA

Na Alodia Babara, Bukoba 

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mtaa (TAMISEMI) Mhoamed Mchengerwa amemwagiza katibu mkuu wa TAMISEMI nchini kutengua nafasi ya mganga mkuu wa mkoa wa Kagera Issesanda Kaniki baada ya hospitali ya rufaa ya Bukoba ya mkoa huo kuzuia mwili wa mtoto mchanga kwa muda wa siku mbili kutoruhusiwa kwenda kuzikwa wakati wakijua watoto wanatibiwa bure.

Maagizo mengine ameyatoa kwa viongozi wa serikali, siasa na watumishi mbalimbali nchini.

Waziri Mchengerwa ametoa maagizo hayo  Desemba 15, mwaka huu wakati akizungumza na wananchi wa mkoa wa Kagera katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kituo cha mabasi yaendayo mikoani kinachokarabatiwa

Waziri Mchengerwa alishuhudia utiaji wa saini ya mikataba ya usanifu miradi ya uboreshaji wa miundomninu ya miji Tanzania (TACTIC) kwa miji 15 ya kundi la pili.

Ameagiza katibu mkuu TAMISEMI kwa kushirikiana na sekta ya afya kufanyika mapitio ya menejimenti nzima ya hospitali hiyo na kutoa maamuzi kwani alipata malalamiko kuwa wapo baadhi ya watumishi wamekuwa wakitoa lugha chafu kwa wagonjwa. 


     WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mtaa (TAMISEMI) Mhoamed Mchengerwa

Amesema,  muda wa kubembelezana haupo tena kwa nyakati hizi watu wamezoea kufanya kazi kwa mazoea sasa hatuwezi kuendelea na watumishi wa namna hiyo kwa sababu wananchi wanaimani na serikali yao.

Wakati huo huo waziri Mchengerwa alisema mtu yoyote au kiongozi yoyote awe wa kisiasa au mtendaji yeyote wa serikali atakaye jaribu kufanya ubadhilifu au kukwamisha miradi inayotarajiwa kutekelezwa katika manispaa ya Bukoba ikiwemo stend kuu, soko kuu, barabara ya kilomita saba na kingo za mto Kanoni na kufunga taa za barabani hatofumbiwa macho atachukulia hatua kali za kisheria.

"Tunataka  tubadilishe muonekano wa Kagera mhe.Rais alizitafuta fedha hizi maeneo mbalimbali anataka kuibadilisha Kagera hivyo, kiongozi yoyote awe wa kisiasa au serikali atakayejaribu kuingiza mkono bila kujali nafasi yake nitashugulika naye kiwemo kumfukuza kazi, hatutaki ubabaishaji katika miradi hii"amesema Mchengerwa.

Aidha amesema, kama kuna viongozi wa siasa ndani ya manispaa ya Bukoba au mkoa wa Kagera wanaokwamisha miradi ya maendeleo ambayo imekuwa ni kiu ya wanakagera kwa muda mrefu atasimamisha baraza la madiwani mpaka miradi hiyo ikamilike.

"Maagizo yangu ujenzi wa soko uzingatie wale wafanyabiashara  wa zamani waliondolewa kinyume na taratibu wapate vibanda ndipo wapya wapewe mabanda na wale waliko nje ya soko wote wapate nafasi hii pia tukikamilisha hatutaki kuona wafanyabiasha wakiendesha shughuli zao nje ya soko hili ambalo Dk.Samia anakwenda kulijenga katika maeneo haya.

"Kiongozi yoyote atakaye kaidi maagizo, ujeuri na kiburi aliyeko kwenye mamlaka yangu nitamfukuza kazi na walioko kwenye mamlaka za juu nitawafikisha kwa Rais awafukuze kazi”amesema.

Pia waziri aliwaagiza  wakurugenzi wote nchini kuendana na kasi ya Ras Samia ambapo kila mkurugenzi anatakiwa kuanzisha vyanzo viwili vya kuingiza mapato atakayeshindwa kufanya hivyo atahovumiliwa .

Mratibu wa miradi ya ushirikiano na benki ya dunia TACTIC Mhandisi Humphrey  Kanyenye amesema miradi hiyo inatakiwa kutekelezwa kwa miezi nane ikiwezekana mwezi Machi mwakani ujenzi uanze mara moja.

Ujenzi wa kituo cha mabasi Bukoba na soko kuu kimekuwa kitendawili cha muda mrefu baada ya kukwama kujengwa takribani miaka 15 iliyopita baada ya kutokea mgongano wa masrahi ya kisiasa.

Miradi hiyo ya uboreshaji wa miundombinu ya miji Tanzania TACTIC  kwa miji 15 ya kundi la pili (Tier) ambapo Manispaa ya Bukoba ni miongoni mwa miji itakayonufaika na miradi hiyo zilitengwa fedha kiasi cha Tsh. Bilioni 23 kwa ajili ya ujenzi huo kati ya shl trilioni moja ya miradi yote. 

No comments