JAMII YATAKIWA KUTOA TAARIFA ZA UKATILI WA KIJINSIA
Na Samwel Mwanga, Maswa
JAMII imetakiwa kutoa taarifa za ukatili wa kijinsia pindi zinapotokea katika mazingira yanayowazunguka ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni njia ya kuendelea kupiga vita na kupinga vitendo vya ukatili.
Hayo yameelezwa Desemba 10 mwaka huu na Mwakilishi wa Mkuu wa wilaya ya Maswa,Venance Saria wakati wa kilele cha Maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia yaliyofanyika katika viwanja wa Madeco mjini Maswa.
Amesema kuwa seriikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliweka utaratibu wa kuadhimisha siku hizo kwa lengo la kukumbusha jamii juu ya kupinga ukatili wa kijinsia unaondelea katika jamii.
Saria ambaye ni Afisa Tarafa ya Nung’hu iliyoko wilayani humo amesema kuwa serikali imeweza kutunga sheria, sera na miongozo mbalimbali inayosaidia katika kutokomeza ukatili wa kijinsia katika jamii hivyo basi ukatili unapotokea mahali popote jamii inatakiwa kutoa taarifa haraka.
Baadhi ya Wananchi waliojitokeza katika viwanja vya Madeco mjini Maswa wakati wa maadhimisho ya Siku 16 za ukatili wa kijinsia wilayani humo.
“Hali ya ukatili katika wilaya yetu bado si nzuri kwa sababu takwimu zinaonesha bado wanawake na watoto ndiyo wahanga wakubwa wa ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto nah ii inasababisha kukosekana kwa haki za msingi wanazostahili kupewa,”
"Ukatili wa kijinsia ni kovu kwa yeyote aliyefanyiwa kitendo hicho, ni wajibu wetu kushirikiana kutoa taarifa ili wahusika wawajibishwe, tusifumbie macho hivi vitendo ni wajibu wetu sote kutoa taarifa ili tuweze kutokomeza ukatili wa aina yeyote katika jamii zetu"amesema.
Pia ametumia fursa hiyo kulishukuru Shirika la World Vission Tanzania kwa kushirikiana na Halmashauri ya wilaya hiyo katika kupinga vitendo hivyo vya ukatili wa kijinsia sambamba na kufanikisha maadhimisho hiyo.
Naye Mratibu wa Mpango wa Maendeleo ya Jamii Shishiyu,(Shishiyu AP),Betty Isaack amesema kuwa maadhimisho hayo ya mwaka huu yenye Kauli Mbiu”Wekeza kuzuia ukatili wa kijinsia”iwe chachu kwa jamii kupitia elimu tuliyoipata kuchukua hatua katika uwekezaji wa kutoa taarifa dhidi ya vitendo hivyo vya ukatili wa kijinsia.
Mratibu wa Shishiyu AP,Betty Isaack wa Shirika la World vission Tanzania akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku 16 za ukatili wa kijinsia wilaya ya Maswa yaliyofanyika uwanja wa Madeco mjini Maswa.
Amesema mapambano hayo yasiwe ya wadau pekee yake bali liwe jukumu la kila mmoja wetu ili tuweze kuhakikisha tumaliza au tunapunguza vitendo hivyo katika jamii kwani vina athari kubwa katika ustawi wa maisha ya mwanadamu.
Kamanda wa polisi wilaya ya Maswa aliyewakilishwa na Mrakibu Msaidizi wa Polisi(ASP)Ramadhani Mkimbu amesema kuwa vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa sasa si kwa wanawake na watoto tu bali hata wanaume wanafanyiwa.
ASP, Ramadan Mkimbu wa Jeshi la Polisi wilaya ya Maswa akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku 16 za ukatili wa kijinsia wilaya ya Maswa yaliyofanyika uwanja wa Madeco mjini Maswa.
Amesema ni vizuri vikatolewa taarifa kwenye vituo vya polisi ambapo kuna madawati ya Jinsi la Jeshi la polisi ambalo linashughulikia malalamiko yote yanayohusiana na ukatili huo
‘Jeshi la polisi limeanzisha haya madawati ya Jinsi nchini nzima kwa hiyo iwapo umefanyiwa au umeona mtu amefanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia katoe taarifa na ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa kwa mtu aliyefanya vitendo hivyo ambavyo havikubaliki katika jamii,”amesema.
Awali Afisa Ustawi wa Jamii wilaya ya Maswa, Grace Mmasi akitoa taarifa ya kazi zilizofanyika katika siku kumi na sita za kupinga ukatili wa kijinsia kuanzia Novemba 25 mwaka huu hadi Desemba 10 mwaka huu.
Afisa Ustawi wa Jamii wilaya ya Maswa,Grace Mmasi akitoa taarifa ya kazi zilizofanyika katika siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia,siku ya maadhimisho hayo yaliyofanyika katika viwanja wa Madeco mjini Maswa.
Amesema kuwa kupitia divesheni ya maendeleo ya jamii na kitengo cha ustawi wa jamii wameweza kutekeleza afua za kupinga ukatili wa kijinsia kwa kutoa elimu kwa makundi mbalimbali katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.
“Tumeweza kutoa elimu ya ukatili ya wa kijinsia kwa makundi mbalimbali katika maeneo mbalimbali ya wilaya ya Maswa na tumewafikia wanaume 911 na wanawake 1105 na mada mbalimbali zilifundishwa ambazo ni pamoja na mbinu za kijikinga na ukatili,aina ya ukatili, madhara ya ukatili,maeneo ya kupeleka taarifa za ukatili na msaada wa kisheria kwa jamii,”amesema.
Akitoa taarifa halisi ya ukatili katika wilaya hiyo kuanzia Mwezi Januari hadi Oktoba mwaka huu amesema kuwa takwimu zinaonesha kuwa wanawake waliofanyiwa vitendo vya ukatili ni 626 na wanaume ni 154 na kwa takwimu hizo inaonesha wazi wanawake ndiyo wahanga wa ukatili wa kijinsia.
Baadhi ya viongozi waliojitokeza katika viwanja vya Madeco mjini Maswa wakati wa maadhimisho ya Siku 16 za ukatili wa kijinsia wilayani humo
“Hali halisi ya ukatili katika wilaya yetu ya Maswa kuanzia mwezi Januari hadi Oktoba mwaka huu inaoesha kuwa wanawake ndiyo wanaendelea kuwa wahanga wa vitendo hivyo kwani waliofanyiwa vitendo hivyo ni 626 na wanaume ni 154,”amesema.
Baadhi ya Viongozi wa wilaya ya Maswa waliojitokeza katika viwanja vya Madeco mjini Maswa wakati wa maadhimisho ya Siku 16 za ukatili wa kijinsia wilayani humo
Baadhi ya Wananchi waliojitokeza katika viwanja vya Madeco mjini Maswa wakati wa maadhimisho ya Siku 16 za ukatili wa kijinsia wilayani humo
Post a Comment