HEADER AD

HEADER AD

MAUWASA KUBORESHA HUDUMA ZA UPATIKANAJI WA MAJI


Na Samwel Mwanga, Maswa

MAMLAKA ya Maji na Usafi wa Mazingira Mjini Maswa (MAUWASA) imedhamilia kuboresha hali ya upatikanaji wa maji katika mji wa Maswa na vijiji 18 mara baada ya kupata pampu mpya tano za kusukuma maji kutoka Wizara ya Maji.

Mkurugenzi Mtendaji wa MAUWASA Mhandisi Nandi Mathias amesema hayo Desemba 12 mwaka huu baada ya kumaliza kazi ya ufungaji wa pampu hizo kwenye mitambo ya kusambaza maji iliyoko katika bwawa la New Sola(Bwawa la Zanzui) ambacho ndicho chanzo kikuu cha maji cha mamlaka hiyo.

        Mkurugenzi wa Mauwasa,Mhandisi Nandi Mathias akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani).

Amesema kuwa pampu hizo ambazo zimenunuliwa na Wizara ya maji kwa kushirikiana na MAUWASA kwa gharama ya Tsh. Milioni 779 ni sehemu ya pampu 16 ambazo zinapaswa kununulia ili kuboresha hali ya upatikanaji wa Maji katika mji wa Maswa na Vijiji vipatavyo 18.

Mhandisi Nandi amesema kuwa  pampu zilizopo za kusukuma maji ambazo ni 16  ni za muda mrefu na kwa sasa zimechakaa  na ufanisi wake wa utendaji wa kazi umeshuka  kwa asilimia 70 na zilifungwa mwaka 1989 na sasa zimefikisha miaka 34 na zilipaswa kutumika kwa miaka 10 na baadaye zibadilishwe.

       Moja ya pampu mpya iliyofungwa katika mitambo ya kusukuma maji ya Mauwasa iliyoko  kwenye chanzo cha Maji cha bwawa la New Sola lililoko wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu.

"Tunazo pampu 16 katika mitambo yetu ya kusukuma maji kutoka bwawani kwenda kwa wananchi lakini pampu hizo ni za muda mrefu tangu zifungwe mwaka 1989 sasa ni  miaka  34 zimechakaa na hata utendaji kazi wake yaani ufanisi umepungua kwa  asilimia 70 kitaalamu zilipaswa zibadilishwe baada ya miaka 10,”amesema

Amesema kutokana na hali hiyo hata gharama za matengenezo zimekuwa kubwa pamoja na pampu hizo kutumia kiasi kikubwa cha umeme na kuongeza gharama za uendeshaji kuwa kubwa kwa mamlaka hiyo sambamba na maeneo mengine kutopata huduma ya Maji.

       Pampu mpya mbili zilizofungwa na Mauwasa kwa ajili ya kusukuma maji kwa wananchi wa mji wa Maswa.

"Pampu zikiwa chakavu ni tatizo zinatuingiza gharama kubwa ya matengenezo ya mara kwa mara na hata umeme unaotumika kuziendesha ni mwingi na hivyo mamlaka kubeba mzigo mkubwa wa uendeshaji na kuna baadhi ya maeneo Maji hayafiki kutokana na pampu kutokuwa na nguvu ya kutosha ya kusukuma maji,"amesema.

Ameendelea kueleza kuwa kupatikana kwa pampu hizo kutapunguza baadhi ya changamoto hizo huku akitolea mfano kila mwezi wamekuwa wakilipa kiasi cha Sh Milioni 30 kwa ajili ya umeme lakini kwa sasa wanaweza kulipa Tsh. Milioni 25 na yale maeneo ambayo yalikuwa hayapati maji kabisa hasa ya vijijini kutokana na uchakavu wa pampu hizo yatapata maji.

Aidha ametumia fursa hiyo kuishukuru Wizara ya Maji na kumshukuru Rais wa Awamu ya sita Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kutolea kwa fedha kwa ajili ya ununuzi wa pampu hizo na kuomba pampu zilizobaki ambazo ni 11 nazo zinunuliwe ili waweze kutoa huduma bora ya maji safi na salama kwa wananchi wanaowahudumia.

      Moja ya pampu mpya iliyofungwa katika mitambo ya kusukuma maji ya Mauwasa iliyoko  kwenye chanzo cha Maji cha bwawa la New Sola lililoko wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu.

Naye Suzana John mkazi wa kijiji cha Zanzuia ameiomba MAUWASA kuhakikisha  kuwa wananchi wa maeneo hayo yanapata maji kwa muda wote mara baada ya kufungwa kwa pampu hizo ili nao waweze kupata huduma ya maji safi na salama.

"Tumefurahi kwa jinsi serikali kupitia MAUWASA inavyowajali wananchi wa wilaya ya Maswa ili waweze kupata huduma ya Maji safi na salama kwa kutuletea pampu hizo mpya.

" Ninaamini na nyingine zitakuja hivyo hizi zilizokuja zimefungwa zianze kazi ili sisi tulioko maeneo ya vijijini tupate Maji muda wote kama wanavyopata wa mjini tusiwe na siku za mgao kama ilivyo sasa,"amesema.
 
       Jengo la kuhifadhia pampu za kusukuma maji lililoko kwenye eneo la Bwawa la New Sola ambalo linahifadhi pampu za kusukuma maji za Mauwasa.

No comments