HEADER AD

HEADER AD

JESHI LA POLISI LAELEZA SABABU ZA KUSUASUA USHIRIKIANO NA VYOMBO VYA HABARI

>> RPC Tarime Rorya aeleza sababu za Jeshi la Polisi kutoa taarifa chache kwenye vyombo vya habari

>> Awahimiza Waandishi wa habari kuandika habari za kufichua badala ya kusubiri kupatiwa habari na Jeshi la Polisi

>>Amkumbuka Mwandishi wa habari gazeti la Mfanyakazi James Nhende kwa kuandika habari za uchunguzi

Na Dinna Maningo, Tarime

JESHI la Polisi mkoa wa Polisi Tarime Rorya limesema kuwa Duniani kote ushirikiano wa Polisi na Vyombo vya Habari umekuwa wa kusuasua kwa muda mrefu.

Hayo yameelezwa na Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Polisi Tarime Rorya ACP Mark Njera katika mdahalo kati ya Jeshi la Polisi Tarime Rorya na Chama cha Waandishi wa habari Mkoa wa Mara.

      Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Polisi Tarime Rorya ACP Mark Njera akizungumza wakati wa mdahalo kati ya Jeshi la Polisi na Waandishi wa Habari 

Mdahalo huo uliandaliwa na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) kwa ufadili wa Shirika la IMS uliohusu kujadili maswala ya ulinzi na usalama kwa Waandishi wa Habari wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao uliofanyika Novemba, 30, 2023 ukumbi wa Blue Sky mjini Tarime.

Kamanda Mark amesema kuwa katika kutekeleza sheria na taratibu, Polisi wamekuwa wakitoa taarifa chache kwasababu za kimsingi.

      Maafisa wa Jeshi la Polisi Tarime Rorya na Waandishi wa habari mkoa wa Mara wakiwa kwenye mdahalo

" Polisi wanatunza ushahidi, kwa ajili ya kupelekwa mahakamani, Polisi wanafundishwa kutotoa habari zinazohusu upelelezi kwani kwa kufanya hivyo kunaweza kuharibu kesi mbalimbali kwa namna moja au nyingine jambo linaloweza kusababisha kutotendeka kwa haki.

"Usiri na uaminifu huwekwa kwa kila afisa mwenye kiapo katika kutekeleza sheria, kwani sio kila Polisi ni msemaji katika vyombo vya habari na wananchi kwa ujumla" amesema RPC Mark.

Kamanda huyo amesema kuwa kutokana na utekelezaji wa sheria na taratibu, Vyombo vya habari kwa upande mwingine vina njia tofauti katika utekelezaji wa majukumu yao.


"Dhamira yao ni kutangaza ukweli. Waandishi bora siku zote ni wale ambao wanaonekana kuwa na bahati ya kuwa wa kwanza kuripoti matukio muhimu.Hapa kuna tofauti kubwa baina yetu maana 'Chombo kimoja kinatunza Siri huku kingine kinafichua siri' hali ambayo inapelekea kuharibu ushahidi" amesema. 

Kamanda Mark amevitaka vyombo vya habari kuamini kuwa Jeshi la Polisi katika kutekeleza sheria daima linaficha habari wakati wao ni masikio ya umma na ni wajibu wao kusema kama ilivyo.

       Maafisa wa Jeshi la Polisi Tarime Rorya wakiwa kwenye picha ya pamoja na Waandishi wa habari mkoa wa Mara

Kamanda huyo amewahimiza Waandishi wa habari mkoani Mara kuandika habari za kiuchunguzi badala ya kutegemea kupata habari Polisi.

Amewahimiza kufuatia baadhi ya Waandishi wa habari kulilalamikia Jeshi hilo kutotoa ushirikiano wa habari kwa Waandishi wa habari na hivyo kusababisha wananchi kukosa haki ya kupata habari kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 18.

"Mimi zamani nikiwa mdogo Nilikuwa nasoma magazeti kuna Mwandishi wa habari alikuwa anaandika gazeti la Mfanyakazi kwa wakati huo, alikuwa anaitwa James Nhende alikuwa anaandika taarifa za uchunguzi.

"James alikuwa mwandishi mzuri sana wa habari za uchunguzi wakati huo na mimi nilikuwa natarajia yakuwa mwandishi wa habari nikaangukia kwenye magwanda, waandishi ibueni habari " amesisitiza RPC Mark.

Akizungumzia haki ya uhuru wa mawazo amesema "Kila mtu ana uhuru wa kutoa taarifa lakini kuna mipaka, ukisoma Katiba hiyohiyo Ibara ya 30, 31 imeweka mipaka, tuna usiri wa kulinda wahanga na utekelezaji wa sheria.


Kamanda huyo amesema kuwa Jeshi la Polisi linawahitaji waandishi wa habari katika kuhabarisha na kuelimisha wananchi juu ya namna ya kushirikiana na Polisi katika kubaini, kuzuia uhalifu na kutanzua uhalifu.

Ameongeza kuwa kupitia vyombo vya habari elimu hufikia watu wengi zaidi na kwa wakati mmoja na kwamba Jeshi hilo linawahitaji waandishi wa habari na Waandishi wanawahitaji Polisi, hivyo sio rahisi kutenganisha uhitaji huo.

"Jambo muhimu kwa kila mmoja anavyotekeleza majukumu yake ni lazima kila mmoja afahamu majukumu ya mwenzake na mipaka yake. Kila mmoja anapotekeleza majukumu yake lazima atangulize Taifa na uzalendo pia" amesema Kamanda Mark.

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa habari mkoa wa Mara, Raphael Okelo amelishukuru Jeshi la Polisi Tarime Rorya kwa ukubali wao na kushiriki mdahalo kati yao na Waandishi wa habari huku akimpongeza RPC Mark kwa uvumilivu wa kushiriki mwanzo wa mdahalo hadi tamati.

Afisa mipango msaidizi wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa habari Nchini (UTPC) Edimundi Kipungu amesema UTPC inaendesha midahalo ya ulinzi na usalama kwa kushirikisha Jeshi la Polisi na Waandishi wa habari katika Mikoa mbalimbali.

     Afisa mipango msaidizi wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa habari Nchini (UTPC) Edimundi Kipungu akieleza madhira yanayowakumba waandishi wa habari.

Amesema lengo ni kujenga ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na Waandishi wa habari kwa manufaa ya jamii na mambo ya kuzingatia mwandishi anapochukua habari kwenye mazingira hatarishi.

Hata hivyo Jeshi la Polisi mkoa wa Polisi Tarime Rorya na Waandishi wa habari mkoa wa Mara wamekubaliana kushirikiana kwa pamoja katika masuala mbalimbali kuhakikisha usalama wa Waandishi unaimalika.




         Baadhi ya mafisa wa Polisi wakichangia mdahalo.



No comments