JESHI LA POLISI : WAMILIKI WA VYOMBO VYA HABARI WAWAPATIE MAFUNZO YA USALAMA WAANDISHI WA HABARI
>>RPC Tarime Rorya asema Waandishi wa habari wanatakiwa kuwa salama
>> Awataka wamiliki wa vyombo vya habari wawapatie waandishi wao mavazi maalum yatakayowatambulisha
>> Awataka waandishi wa habari kuzigatia maelekezo ya wasimamizi wa usalama wanapokuwa kazini
Na Dinna Maningo, Tarime
JESHI la Polisi mkoa wa Polisi Tarime Rorya limesema kuwa Waandishi wa habari wanahitaji kuwa salama katika kufanikisha kazi zao za kuhabarisha Jamii.
Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Polisi Tarime Rorya, ACP Mark Njera
akizungumza katika mdahalo uliowashirikisha baadhi ya Maafisa wa Polisi Tarime Rorya na Wanachama wa Chama cha Waandishi wa habari mkoa wa Mara (MRPC) uliofanyika Novemba, 30, 2023 mjini Tarime, amesema kuwa ili Mwandishi wa Habari awe salama awapo kwenye majukumu yake ni lazima azingatie yafuatayo;
"Usalama uanze na yeye kwanza, Ashirikiane na Polisi na wadau wengine kutoa elimu kwa jamii ili sote tushirikiane kubaini na kuzuia uhalifu zikiwepo vurugu ambazo zitasababisha kupata msukosuko wawapo kazini au kwenye makazi yao na shughuli zingine binafsi" amesema Kamanda Mark.
Kamanda Mark amewataka wamiliki wa Vyombo vya habari wawapatie mafunzo ya usalama Waandishi wao wa habari pamoja na mavazi maalum yatakayowatambulisha kama vile vizibao (Reflector) na mengineyo.
" Na wanapokuwa kazini wakipewa maelekezo na wasimamizi wa usalama waweze kutii mara moja, kwani baadhi ya maeneo wanayofanyia kazi yaweza kuwa hatarishi au maalum katika kulinda vielelezo mbalimbali" amesema.
RPC Mark ameongeza kusema mdahalo huo uliowashirikisha Waandishi wa habari mkoa wa Mara na Jeshi la Polisi Tarime Rorya iwe daraja katika kulinda amani, kusimamia sheria na taratibu, kuzuia na kubaini makosa, pamoja na kulinda mali za wananchi wa mkoa wa Mara.
Afisa mipango msaidizi wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa habari Nchini (UTPC) Edimundi Kipungu amesema UTPC inaendesha midahalo ya ulinzi na usalama kwa kushirikisha Jeshi la Polisi na Waandishi wa habari katika mikoa mbalimbali.
Amesema lengo ni kujenga ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na Waandishi wa habari kwa manufaa ya jamii na mambo ya kuzingatia mwandishi anapochukua habari kwenye mazingira hatarishi.
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa habari mkoa wa Mara, Raphael Okelo amelishukuru Jeshi la Polisi Tarime Rorya kwa ukubali wao na kushiriki mdahalo kati yao na Waandishi wa habari huku akimpongeza RPC Mark kwa uvumilivu wa kushiriki mwanzo wa mdahalo hadi tamati.
Post a Comment