WENYEVITI WA MITAA WAMTEGA MBUNGE MATHAYO KERO YA MITARO
Na Shomari Binda, Musoma
WENYEVITI wa Mitaa katika jimbo la Musoma mjini wamemfikishia kero ya mitaro mbunge wa jimbo la Musoma mjini Vedastus Mathayo wakimuomba asaidie mitaro ijengwe kuepusha mafuriko ambayo chanzo ni kutokuwepo mitaro ya kupitisha maji.
Maombi hayo yametolewa kwa mbunge huyo kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali hapa nchini likiwepo jimbo la Musoma mjini.
Wakizungumza kwenye kikao baina ya mbunge na wenyeviti wa mitaa wamesema yapo maeneo ambayo yameathirika kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
Mwenyekiti wa mtaa wa Machinjioni Omary Omary amesema mvua zinazonyesha zimefanya uhalibifu wa Barabara kutokana na kutokuwepo kwa mitaro.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa mtaa wa Songambele Juma Simba amesema iwapo mitaro itapatikana itakuwa ni msaada kwenye barabara.
Akijibu maombi ya wenyeviti hao kuhusu miundombinu ya barabara amesema maombi yaliyotolewa yanakwenda kufanyiwa kazi ili kuondoa kero hiyo.
Amesema kero hiyo imeonekana kubwa na inapaswa kupewa kipaumbele na ndio kazi ambayo anakwenda kuanza nayo.
Akizungumzia suala la maendeleo kwenye sekta ya elimu ,maji, afya na miundombinu, amesema mengi yamefanyika na hiyo itakuwa fursa ya kuwafanya wenyeviti wa mitaa kushinda uchaguzi wa mwaka 2024.
Mathayo amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi kwenye maeneo hayo na utekelezaji umefanyika.
Amesema wenyeviti wa mitaa katika jimbo la Musoma mjini wanapaswa kutembea vifua mbele na kumsemea vizuri Rais Samia kwa kile alichokifanya.
Mbunge huyo amesema wakati wa sasa wenyeviti wa mitaa ni vyema wakawa na mahusiano mazuri na wananchi wanaowaongoza na kuwatatulia matatizo yao.
Amesema ni vyema pia kujiepusha na muingiliano wa shughuli za uongozi na kufanya vikao vya kuzungumzia maendeleo yaliyopatikana.
" Tumekutana hapa kwaajili ya kuzungumzia maendeleo kwenye mitaa yetu na ntaomba kila mwenyekiti mwenye changamoto kwenye mtaa wake ntaomba azungumze changamoto kwenye mtaa wake.
" Rais Samia amefanya kazi nzuri kwenye jimbo letu na uchaguzi wa mwakani utakuwa mwepesi kwa sababu mengi tuliyo ahidi tumetekeleza",amesema Mathayo.
Post a Comment