KAMPUNI YA WARACHA, KEMANYANKI ZAHIMIZA JAMIII KUTOWAFICHA WATOTO WASIOONA
>>Mkurugenzi Kampuni ya WARACHA asema baadhi ya watu huwaficha wasioona huku wazazi wakiongoza kuficha watoto wasioona
>>Meneja Rasilimali watu Kampuni ya KEMANYAKI ahimiza jamii kuwaibua watoto wasioona wapelekwe shule
>>Afisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Kemambo awaomba wanachama wasioona kushirikiana pamoja kuwaibua watu wasioona
Na Dinna Maningo, Nyamongo
IMEELEZWA kuwa baadhi ya jamii zenye watoto wenye ulemavu wa macho wasioona huficha watoto na hivyo kuwa chanzo cha kukatisha ndoto za watoto kwa maisha yao ya baadae.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya WARACHA LTD iliyopo Nyamongo, Wilaya ya Tarime mkoa wa Mara, Daudi Ryoba Tindo amesema kuwa baadhi ya jamii yenye watu wasioona wamekuwa na uoga, aibu na kuwaficha wasioona huku wazazi wakihusika zaidi kuwaficha watoto wasioona.
Daud ameyasema hayo wakati alipowatembelea wanachama wa Chama cha wasioona Tanzania (TLB) Wilaya ya Tarime katika kiko chao cha kujadili masuala mbalimbali ya Chama ambapo alifadhili kikao kwa kuwachangia fedha Tsh.Milioni moja (1, 000,000) kwa ajili ya chakula na usafiri.
"Nawasihi jamii, wazee, vijana, akina mama msifiche watu wenye ulemavu
jitahidini kuwaweka wazi watambulike ili waweze kufanya mambo ambayo ni malengo yao katika maisha.
"Kupata ulemavu siyo mwisho wako wa maisha, unaweza ukawa na ulemavu lakini bado maisha yako yakaendelea vizuri. Nawaomba wanatarime wote, Mara na kokote wasifiche walemavu.
David amewaasa watu wenye ulemavu wa macho wasioona kujiunga kwenye vyama vya wasioona ili waweze kutambulika na kusaidiwa.
Wanachama wasioona wilaya ya Tarime wakiwa katika picha ya pamoja na wafadhili waliofanikisha kufanyika kikao chao
Mkurugenzi huyo ameiomba Serikali na wadau mbalimbali kujitahidi kuwafadhili watu wenye ulemavu kwa kadri itakavyowezekana ili kutatua changamoto zao.
Meneja Rasilimali watu Kampuni ya Ujenzi ya KEMANYAKI Selina Mkaro amesema kuwa kuna watoto wengi wasioona wapo tuu mitaani wanazulula hawajapelekwa shuleni kupata elimu.
"Sisi tuwe mabalozi wazuri tushikamane kuhakikisha tunawaibua watoto walemavu wasioona waende shule, wakipata hiyo elimu watakuwa na uelewa wa mambo mengi na watafika mbali.
"Inapotokea changamoto ya kifedha msisite kutushirikisha, wadau tupo wengi, na nishauri mjiunge na Bima ya afya ni muhimu, tunajua huduma ya watoto ni bure lakini sidhani kama huwa ni bure maana kuna gharama ambazo huwa zinahitajika hivyo wanachama jiungeni na Bima ya afya kwa manufaa ya afya zenu" alisema Selina.
Meneja huyo aliyasema hayo aliposhiriki kikao cha wanachama wasioona kwaniaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya KEMANYAKI Nikolaus Mgaya ambaye alichangia chama hicho Tsh. Laki moja na elfu hamsini (150,000) ya vinywaji kwa ajili ya kikao cha wanachama wasioona.
Mwenyekiti wa Chama cha Wasioona wilaya ya Tarime Mseti Mwita alizipongeza Kampuni hizo kwa kuwafadhili fedha ambazo zimefanikisha waweze kufanya kikao cha chama.
Baadhi ya wanachama wa TLB Tarime wakiwa kwenye picha ya pamoja na wafadhili wa kikao kutoka kampuni ya Waracha na Kampuni ya Kemanyanki
Alisema kuwa watu wenye ulemavu wa kuona wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo umaskini unaosababisha washindwe kupata nauli za usafiri kushiriki vikao vya chama.
Aliongeza kwamba mara nyingi wanaposhirikisha wadau ili kufadhili vikao huwapuuza lakini kampuni hizo kupitia Mweka Hazina wa TLB Bhoke Orindo mkazi wa Nyamongo zilikubali kuwasaidia fedha kuendesha kikao.
Afisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Kemambo -Nyamongo Mary Kitesho Laizer, amewaomba wanachama wasioona kushirikiana pamoja kuwaibua walemavu wasioona ili waweze kupata huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo mikopo ya halmashauri.
"Sisi tuliopo Nyamongo tutaendelea kuleta wengine ambao ni walemavu wa macho wasioona, wapo wengine wametunzwa nyumbani hawajui waende wapi tutajitahidi kuwaambia wajiunge na mikopo ya walemavu ili wajikuze kiuchumi" alisema Mary.
Mwl. Johnson Mpenda wa shule ya Sekondari Ingwe akisoma taarifa ya TLB kwa niamba ya Katibu wa TLB wilaya ya Tarime.
Post a Comment