KAMPUNI YA AGAB HARDWARE &TIMBER SUPPLY YATOA MSAADA GEREZA LA CHATO
Na Daniel Limbe, Chato
IKIWA imebaki siku moja kwa baadhi ya waumini wa dini ya kikristo duniani kusherehekea sikukuu ya Krisimasi, baadhi ya wasamaria wema wamejitokeza kutoa misaada ya chakula na vinywaji kwa mahabusu na wafungwa waliopo gereza la wilaya ya Chato mkoani Geita.
Uamuzi huo unatajwa kuwa ni sadaka kwa wahitaji walioko ndani ya magereza hiyo ili waweze kusherehekea sikukuu ya kukumbuka kuzaliwa kwa mwokozi wa ulimwengu Yesu Kristo miaka zaidi ya 2000 iliyopita.
Miongoni mwa wasamaria hao ni Mkurugenzi wa kampuni ya "Agab Hardware & Timber supply" Aloyce Mwenda,ambaye ametoa mchele,kondoo,sabuni,mafuta ya kupaka,chumvi,na nyembe kwaajili ya usafi.
Mwenda amesema yapo makundi mengi yenye uhitaji katika jamii lakini kampuni yake imeguswa zaidi na wafungwa kwa sababu ni watu ambao wapo nje ya makazi yao ya kawaida ambayo ni rahisi kuhudumiwa.
" Sisi tumeguswa kuwasaidia wafungwa na mahabusu ili kuwaondolea unyonge wawapo gerezani lakini jambo la msingi zaidi ni pale tunapoelekea kusherehekea sikukuu ya krisimas basi na ndugu zetu waliopo gerezani watambue kuwa wao bado ni sehemu ya jamii ambayo inapaswa kumtii na kumheshimu mwenyezi Mungu wakati wote"amesema Mwenda.
Zacharia Hezron, msambazaji wa vifaa vya ujenzi wa kampuni ya Agab amesema wamelazimika kutoa msaada wa vitu mbalimbali ili kuonyesha upendo kwa wafungwa na mahabusu kwa sababu ni agizo la mwenyezi Mungu kuwajali wahitaji.
Mkurugenzi wa kampuni ya Agab, Aloyce Mwenda,akikabidhi Kondoo,mchele,sabuni za kuongea,mafuta,chumvi na nyembe za kufanyia usafi gerezani.
Msaada huo ni sehemu ya faida kidogo waliyopata kwa kipindi cha mwaka mmoja na kutambua thamani ya kuhudumia wasiojiweza na wenye uhitaji ili waendelee kumheshimu Mungu, kumuabudu na kumtukuza siku zote za maisha yao.
Akipokea misaada hiyo kwa niaba ya wafungwa na mahabusu, Kaimu mkuu wa magereza hiyo A/INSP. Pius Sambai, amepongeza baadhi ya taasisi, makampuni na watu binafsi walioguswa kusaidia wahitaji hao kwa kuwa suala hilo ni la kimungu.
Kaimu mkuu wa Gereza la wilaya ya Chato,A/INSP. Pius Sambai,akizungumza na vyombo vya habari baada ya kupokea msaada kutoka kwa wasamaria wema
"Gereza letu linawafungwa na mahabusu zaidi ya 405 hao wote wanahitaji kupata huduma za msingi kama chakula msaada wenu kwa hawa walengwa ni muhimu sana kwa sababu hawa ni sehemu ya jamii na hapa wapo kwenye chuo cha mafunzo na tunaamini siku moja watarejea huko uraiani wakiwa watu wema".
"Nitumie fursa hii kukupongezeni sana kwa moyo huu wa uzalendo, serikali yetu inahudumia miradi mbalimbali ya maendeleo ili kuhakikisha wananchi wanajikwamua na umaskini, pamoja na hayo yote haiwezi kufanya kila kitu kwa wakati mmoja, hivyo mnapotoa huduma kama hizi mnaisaidia serikali kutatua changamoto za jamii.
Post a Comment