HEADER AD

HEADER AD

PIKIPIKI 157, SILAHA 11 ZAKAMATWA

Na Alodia Babara, Bukoba

JESHI la polisi mkoani Kagera limekamata silaha 11 zikiwemo bunduki 2 aina ya AK 47 zikiwa na magazine tatu, risasi 115, bastola aina ya glock 17 na bunduki aina ya gobore.

Kamanda ya wa jeshi la polisi mkoani Kagera Blasius Chatanda akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 14,2023 amesema kuwa, jeshi hilo  linaendelea kufanya oparasheni mbalimbali na kuimarisha ulinzi na usalama wa wananchi katika mkoa huo ambapo katika oparasheni iliyofanyika kuanzia Septemba, 2023 hadi sasa silaha 11 zilikamatwa.

       Kamanda ya wa jeshi la polisi mkoani Kagera Blasius Chatanda akionyesha moja ya silaha zilizokamatwa kwenye oparasheni iliyofanyika kuanzia Septemba,2023 hadi sasa

“Katika kudhibiti matukio ya utekaji  nyara hasa kwa wafugaji katika mkoa wetu wa Kagera tumefanikiwa kukamata watuhumiwa 14 wa utekaji, tumekamata silaha mbili aina ya AK 47zikiwa na magazine tatu pamoja na risasi 115 na bastola aina ya grock 17” amesema Chatanda.

Aidha amesema katika kudhibiti matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha na ujangiri jumla ya bunduki nane aina ya gobore zimekamatwa na kati ya hizo nne zilisalimishwa na watuhumiwa watano kufikishwa mahakamani kwa hatua za kisheria.

Amesema jeshi hilo limeendelea kudhibiti wimbi la wizi wa watoto na kufanikiwa kukamata watu wanne ambao walihusika na wizi wa watoto na watoto wanne walikamatwa wakiwa hai.

Ameongeza kuwa, watuhumiwa hao walifikishwa mahakamani kwa hatua mbalimbali ili kujibu tuhuma zinazowakabili.

Wakati huo huo, amesema pikipiki za wizi ambazo hazikuwa na nyaraka zozote zipatazo 157 zimekamatwa mkoani Kagera pamoja na nchi jirani ya Burundi baada ya kufanyika oparashen.

Amesema pikipiki 157 zilizokamatwa kati ya hizo 92 zilikamatwa nchini Burundi zikiwa na usajili wa namba za Tanzania zikiwa zinatumika nchini humo, huku pikipiki 65 zikikamatwa mkoani Kagera.

“Kwa sasa pikipiki hizo bado ziko Burundi baada ya kukamilisha taratibu zote za kuzirejesha hapa nchini tutawatangazia wananchi ili waje kuzitambua, na pikipi zilizopo mkoani hapa watu waje kuzitambua” amesema Chatanda.

Mmoja wa waendesha pikipiki maalufu boda boda manispaa ya Bukoba Enock Novath ameliomba jeshi la polisi kuimalisha ulinzi ili kudhibiti matukio ya wizi wa pikipiki ambayo yameshamili katika mkoa wa Kagera.

Joanes Festo mkazi wa manispaa ya Bukoba amedai kuwa mwaka huu ameibiwa pikipiki mbili na kutoa taarifa kituo cha polisi na kuwa hakuna pikipiki yake ambayo imeishapatikana.

Ameliomba jeshi la polisi kuwa zinapotolewa taarifa za wizi wa pikipiki msako uanze mara moja na siyo kusubili oparasheni kwani kufanya hivyo zitakamatwa pikipiki kabla hazijasafirishwa kwenda nje ya mkoa.



No comments