HEADER AD

HEADER AD

PrEP DAWA KINGA YA UKIMWI INAYOTOLEWA KWA KIFICHO

>>Watoa huduma watoa kinga kwa siri

>> Jamii bado haijatambua uwepo na matumizi ya dawa ya PrEP

>>Serikali yatakiwa kuitangaza hadharani ili watu waitambue na kuitumia

Na Daniel Limbe, Chato

UGONJWA wa Ukimwi bado ni tishio kubwa kwa jamii na kwamba jitihada mbalimbali zinahitajika ili kuepukana na maambukizi mapya ya virus vya ugonjwa huo.

Miongoni mwa jitihada hizo ni pamoja na uhamasishaji wa matumizi ya dawa ya PrEP (pre-exposure prophylaxis) ambayo inatajwa kuwa bora zaidi katika kuzuia maambukizi mapya ya Virusi vya UKIMWI (VVU) na kupunguza makali ya VVU.

Licha ya dawa hiyo kuruhusiwa kutumika hapa nchini, jamii bado haijatambua uwepo wake kutokana na baadhi ya watoa huduma za afya kutoa kinga hiyo kwa usiri mkubwa, uchunguzi wetu umebaini.

Mwandishi wa Makala haya amefanikiwa kuzungumza na baadhi watumiaji wa dawa hiyo (majina halisi tunayahifadhi) ambao wamedai kuwa waliitambua PrEP baada ya kupewa na watoa huduma za afya wakiwa kwenye maeneo ya mikusanyiko ikiwemo kwenye vilabu ya kuuza pombe nyakati za usiku.

Dawa ya kupunguza makali ya Virusi vya UKIMWI (VVU)

Neema John (siyo jina halisi) ambaye ni mhudumu wa King Stone Grocery, anasema yeye hutumia dawa hizo pale anapokuwa na mpenzi mpya ambaye hajui historia yake na kwamba huzitumia saa tatu kabla ya kwenda kujamiiana.

Alizitambua baada ya kuelimishwa na baadhi ya vijana waliokuwa wateja wake wa vinywaji, ambao walikuwa wakitembelea eneo hilo mara kwa mara huku wakiwa wamevalia mabegi mgongoni hata nyakati za usiku ambapo walimshawishi kuzitumia dawa hizo ili kumkinga na maambukizi mapya ya VVU.

"Nakumbuka siku hiyo nilikuwa na rafiki yangu wa kiume tuliyekuwa tumekubaliana kwenda kufanya mapenzi, tulikunywa pombe kwa muda mrefu baadaye kijana mmoja wa kiume akaniita akiwa na begi lake mgongoni ndo akanipa hizo dawa na kunisihi sana kuzitumia".

"Tangu hapo ndipo nilipoifahamu kinga hiyo ambayo niliendelea kuitumia mpaka wale vijana tulipopoteana, huenda baada ya rais Magufuli kufariki nao wakahamishwa". anasema Neema.

Samson Erick (siyo jina halisi) ambaye ni mtumiaji wa dawa kinga ya PrEP anasema iwapo asingekuwa akitumia dawa hiyo huenda mauti ungeshamfika kitambo kutokana na kitendo chake cha kujamiiana na wanawake pasipo kuvaa mipira ya kiume.

Anasema wapo vijana ambao huzunguka kwenye maeneo ya mikusanyiko na kutoa elimu ya kujikinga na maambukizi ya Ukimwi ambao pia huelezea uwepo wa dawa kinga iwapo mtu ataona hawezi kutumia kondomu.

"Tunashukuru kwa mpango mzuri wa serikali kutuletea kondomu hadi huku mialoni kwetu, kama unavyoona hili boksi sasa halina kondomu hata moja inamaanisha watu wanazitumia japo siyo wote"anasema Erick.

Katika eneo la machimbo ya dhahabu Musasa, kata ya Makurugusi wilayani hapa baadhi ya wachimbaji wadogo wa madini wanaonekana kushangaa uwepo wa dawa kinga kwaajili ya kuzuia maambukizi ya VVU.

Nikutokana na kile wanachosema kutokuwepo kwa elimu ya kupambana na maambukizi hayo zaidi ya mamlaka za serikali kufika eneo lao na kuweka kondomu kwenye baadhi ya makasha yaliyopo kwenye machimbo hayo.

"Kwa ujumla sisi wachimbaji hatujui sana matumizi ya kinga tofauti na kondomu, hiyo ya vidonge unayosema wewe kwa kweli mimi siijui wala sijawahi kuiona huku mgodini, labda kwa wenzangu ila mimi siwezi kusema uongo siijui kabisa"anasema Erick.

Hata hivyo uchunguzi wa Mwandishi umebaini kuwa, baadhi ya vijana hutamani kutumia njia za kujikinga na maambuki mapya ya VVU lakini wanapotumia mipira ya kiume(Condoms) huwapungizia radha ya tendo la ndoa, kuwachelewesha kumaliza tendo na wengine kukerwa na harufu itakanayo na mafuta ya mipira hiyo.

Mwita Chacha (siyo jina halisi) ambaye ni mtumishi wa hospitali ya wilaya ya Chato, anakiri kuwa miongoni mwa watumiaji wa PrEP katika kujikinga na maambukizi ya VVUambapo anasifia kuwa kinga hiyo huenda ikawa mwarobaini ya kumaliza ugonjwa wa Ukimwi chini.


"Matokeo ya kinga hiyo binafsi nayakubali sana kwa kuwa nimewahi kuitumia baada ya kama saa tatu nikaenda kufanya ngono na mdada mmoja ambaye tupo naye hapa kazini ila yeye huwa ni mwathirika wa VVU nilivyomaliza tendo nikawa na hofu kubwa lakini baada ya miezi mitatu kupita nilipima afya na nikawa mzima.

"Kama haitoshi baada ya miezi sita nilipima tena nikawa mzima kabisa. ilivyofika miezi tisa nikapima tena nikawa mzima wa afya tele...kwahiyo ipo haja kubwa kwa serikali kuihamasisha dawa hiyo ili wengi waijue maana hapa hospitali tunazo nyingi tu za kutosha"anasema Chacha.

Kauli ya Mratibu wa Ukimwi 

Kwa mujibu wa Mratibu wa Ukimwi wilaya ya Chato mkoani Geita, Dk. Lilian Kagaruki, anasema dawa ya PrEP ni kinga tiba muhimu sana kutumiwa na watu walio katika hatari ya kuambukizwa, wanandoa ambao mwenzi mmoja ana VVU na mwingine hana.

Anasema wengine ni wale wasichana wanaouza miili yao (madada poa), wanaume wanaofanya mapenzi ya jinsia moja na wale waraibu wa dawa za kulevya.

" PrEP inaaswa kuanza kutumiwa na mtu kabla ya kuambukizwa VVU na kwamba iwapo atathibitika kuwa na maambukizi mapya ya Ukimwi tunamshauri kuanza kutumia ARV"amesema.

Dk. Kagaruki anasema wilaya ya Chato ni miongoni mwa wilaya ambazo bado jitihada kubwa za mapambano dhidi ya ukimwi zinapaswa kupewa kipaumbele kutokana eneo kubwa kuzungukwa na shughuli za uvuvi wa samaki na uchimbaji madini.

Hata hivyo anasema PrEP inapaswa kutolewa kwa mtu ambaye amepatiwa elimu sahihi ya matumizi na kwamba haitolewi kama njugu kwa kuwa inaweza kusababisha madhara mengine kiafya iwapo mtumiaji hatozingatia masharti anayopewa.

Dk. Kagaruki anakiri kuwa dawa hiyo imeonyesha matokeo makubwa kwa aslimia 99 ya watu wanaoitumia huku akiitaka jamii kutoona aibu kujitokeza kupata ushauri wa kitaalamu kabla ya kuanza matumizi yake.

Wataalam wa afya wanashauri kinga tiba hiyo itumiwe siku saba kabla ya kushiriki tendo la ngono ili kutoa mwanya kwa dawa hiyo kusambaa vizuri mwilini ili kuongeza ufanisi wake.

Kadhalika wanasema ni vyema ikatumika mfululizo kwa kumeza kila siku mpaka pale mhusika atakapoona hayupo tena katika mazingira ambayo ni hatarishi kwa afya yake.

Licha ya matokeo makubwa ya ufanisi wa kinga hiyo, uchunguzi umebaini jamii kubwa bado haijatambua uwepo dawa hiyo kutokana na kutolewa kwa usiri mkubwa na kukosekana kwa taarifa sahihi kwa jamii ukilinganisha na ilivyo kwa dawa za kufubaza makali ya ugonjwa wa Ukimwi(ARV)

Nchini Tanzania, PrEP ni mwanga mpya katika kunusuru afya ya jamii kwa kupunguza maambukizi mapya ya VVU kutokana na ukweli kwamba hapo awali hapakuwa na dawa kinga ya kudhibiti maambukizi ya VVU zaidi ya kutumia Condom,kubaki na mpenzi mmoja au kuacha kabisa kufanya ngono.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anawapongeza wadau wa mapambano dhidi ya Ukimwi kutokana na jitihada kubwa zilizofanyika kupunguza maambukizi mapya ya VVU nchini.

       Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa

Akiwa katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Ukimwi duniani yaliyofanyika Desemba mosi 2023 mjini Morogoro,alisema maambukizi mapya miongoni mwa watu wazima wenye zaidi ya miaka 15 yanaendelea kupungua kutoka watu 72,000 waliokuwepo mwaka 2016/17 hadi watu 60,000 kwa mwaka 2022/23 sawa na upungufu wa aslimia 0.18 ambapo aslimia 0.24 ni wanawake na aslimia 0.11 ni wanaume.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la afya duniani (WHO) iliyotolewa Septemba 2015, ilipendekeza watu walio katika hatari kubwa ya kuambukizwa VVU, wanaojulikana kama watu walio katika hatari, wapewe PrEP kama chaguo sahihi la kuzuia maambukizi hayo.

Hata hivyo Shirika la umoja wa mataifa la kupambana na Ukimwi (UNAIDS) linasema Dunia ipo mbioni kutokomeza Ukimwi ifikapo 2030 mara tu programu muhimu za afya zitakapofadhiliwa kikamilifu.

Eneo la Jangwa la Sahara ambako aslimia 65 ya watu wote wenye VVU wanaishi,linapiga hatua kubwa katika kutokomeza ugonjwa huo ikiwemo Tanzania.

Kwa mujibu wa UNAIDS, Tanzania, Botswana, Eswatini, Rwanda na Zimbabwe tayari zimefikia lengo la "95-95-95" ikiwa na maana kwamba aslimia 95 ya wanaoishi na VVU wanajua hali zao, aslimia 95 wanapata matibabu ya kurefusha maisha na aslimia 95 wanaopata matibabu wamefubaza virusi hivyo.

Aidha jaribio la chanjo ya VVU linaendelea nchini Tanzania,Uganda na Afrika kisini ambapo linahusisha mchanganyiko wa chanjo za VVU na Pre- exposure prophylaxis (PrEP) kwa wakati mmoja.

 Nini kifanyike

Kwa kuwa dawa hiyo imeonyesha matokeo makubwa kwa watumiaji wadau wa masuala ya afya wanasema ni wakati muafaka kwa serikali kuitangaza hadharani ili wengi waitambue na kuitumia kwa ufasaha badala ya kutolewa kwa kificho.

Serikali iongeze idadi ya watoa huduma za kinga hiyo ili wayafikie kwa haraka makundi yaliyopo kwenye hatari kubwa ya kuambukizwa VVU.

Kliniki za huduma ya Baba, mama na mtoto zitumike kuitangaza PrEP ili watu waitumie katika kudhibiti maambukizi mapya ya ugonjwa huo.

Jamii isione aibu kwenda kwenye vituo vya kutolea tiba kupata ushauri na kuomba kinga hiyo ili kunusuru maisha yao na wenzao.

Maeneo yote yanayotumika kupima VVU yawezeshwe kuwa na dawa hiyo ili iwe rahisi kupatikana hadi vijijini.

                

No comments