HEADER AD

HEADER AD

RC MARA : SIO LAZIMA UWE NA CHEO KIKUBWA NDIO UFANYE MABADILIKO


Na Dinna Maningo, Bunda

MKUU wa Mkoa wa Mara Said Mtanda amesema kuwa mabadiliko chanya hayafanywi na watendaji wenye vyeo tu bali yanafanywa na watumishi wote wenye vyeo vikubwa na wasio na vyeo.

RC Mtanda aliyasema hayo wakati  akifungua kikao cha tathmini ya Maendeleo ya Elimu Mkoa wa Mara kinachofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Mji wa Bunda.

Mtanda amewaataka walimu na wasimamizi wa elimu wa ngazi mbalimbali kuongeza ubunifu na kujiongeza katika utendaji wao wa kazi utakaochochea mabadiliko chanya kwa walimu na wanafunzi wanaowasimamia na kuacha alama chanya katika utendaji wao. 

         Mkuu wa Mkoa wa Mara Said Mtanda

“Sio lazima mtu uwe na cheo kikubwa ndio ufanye mabadiliko, unaweza kuwa huna cheo lakini kwa namna unavyochapa kazi na kuongeza ubunifu unaweza kuleta mabadiliko makubwa katika eneo lako kuliko hata mtu mwenye madaraka makubwa ambaye hana ubunifu” alisema Mtanda. 

Amewataka Walimu kujiendeleza kimasomo pamoja na kuchangamkia fursa mbalimbali zilizopo katika maeneo yao ya kazi. 

Pia  Mtanda amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri ambao hawajakamilisha ujenzi wa shule mpya na kuzisajiri kufanya kazi usiku na mchana na kuhakikisha wanasajiri shule hizo ili ziweze kuanza kuchukua wanafunzi Januari, 2024. 

Aidha, amewataka Wakurugenzi, Wasimamizi wa Elimu ngazi mbalimbali kuwasikiliza walimu na kujitahidi kutatua baadhi ya changamoto zinazowakabili ambazo utatuzi wake  upo katika ngazi yao na hauhitaji fedha. 

Mtanda amewataka wasimamizi wa Elimu kuweka malengo katika utekelezaji wa majukumu yao na katika maisha yao binafsi na kuisemea vizuri  Serikali kwa mambo mazuri inayoyafanya kwa wananchi wa mkoa wa Mara. 


Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Elimu na Mafunzo  Makwasa Bulenga aliwapongeza wasimamizi wa elimu na walimu wa mkoa wa Mara kwa jitihada kubwa wanazozifanya katika kufundisha wanafunzi na kuwasimamia walimu. 

Bulenga alieleza kuwa mwaka  2022 Mkoa ulipanga kufaulisha kwa asiliamia 100 kwa mitihani ya Taifa ya Kidato cha Sita na mwaka 2023 Mkoa umefaulisha kwa asilimia 100 ukiwa na daraja la nne kwa mwanafunzi mmoja tu na kuongeza kuwa matokeo ya mitihani mingine bado hayajatoka lakini anamatumaini kwa kazi iliyofanyika mkoa wa Mara utafanya vizuri.

Hata hivyo, Bulenga alisema kwa upande wa mitihani ya kidato cha nne, pili, darasa la saba na darasa la nne bado juhudi zaidi zinahitajika katika kuongeza ufaulu wa wanafunzi katika mitihani ya kitaifa ya madarasa hayo.  

“Kwa umoja wetu tumepiga hatua kubwa sana katika maendeleo ya elimu ya mkoa wa Mara japo kuna maboresho zaidi yanahitajika hususan katika shule za msingi na kidato cha kwanza hadi cha nne” alisema Bulenga. 

 Bulenga alieleza kuwa pamoja na mafanikio mbalimbali yaliyopatikana katika mkoa wa Mara kwa mwaka huu, bado Mkoa una upungufu mkubwa wa walimu wa masomo ya Sayansi na hivyo kuathiri ufundishaji wa wanafunzi katika masomo hayo. 

Akizungumzia kuhusu ujenzi wa shule mpya, Bulenga alisema tayari baadhi ya Halmashauri zimeshakamilisha ujenzi wa shule mpya na kuzisajiri huku baadhi ya Halmashauri zikiendelea na ukamilishaji wa shule hizo. 

Mkuu wa Shule ya Sekondari Sazira, Halmashauri ya Mji wa Bunda, Edigga Sibora alimshukuru mkuu wa mkoa huo kwa kufungua kikao hicho cha tathmini na kuahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote yalitotolewa.

“Sisi tunaahidi hatutakuangusha katika kuleta mabadiliko katika maeneo yetu ya kazi na katika maisha yetu sisi wenyewe” alisema Sibora. 

Kikao hicho kimehudhuliwa na Makatibu Tawala wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Wasimamizi wa Elimu ngazi ya Mkoa, Halmashauri, wadau wa elimu na baadhi ya walimu wakuu na wakuu wa shule.


No comments