HEADER AD

HEADER AD

ULEVI, MIGOGORO YA NDOA YATAJWA CHANZO CHA UKATILI WA KIJINSIA


Na Alodia Babara, Bukoba

WASTANI wa Migogoro ya familia 45 hupokelewa kila mwezi katika ofisi ya ustawi wa jamii manispaa ya Bukoba mkoani Kagera, migogoro inayosababisha ukatili kwa wanawake na watoto.

Ofisa ustawi wa jamii manispaa ya Bukoba Japheti Kanoni akizungumza na Mwananchi digital Desemba 05,2023 amesema kuwa vitendo vya ukatili vimekuwa vikisababishwa na migogoro ya familia na ulevi wa kupindukia.

Kanoni ametaja takwimu za vitendo vya ukatili kwa kipindi cha robo mbili za mwaka April hadi Juni na Juni hadi Septemba mwaka huu kuwa, April hadi Juni ukatili  wa kimwili idadi ya  matukio yalikuwa  manne, ukatili wa kingono matatu, kihisia 48 na utelekezaji wa familia 20.

Ofisa ustawi wa jamii manispaa ya Bukoba Japheti Kanoni

"Juni hadi Septemba mwaka huu matukio ya ukatili wa kimwili yalikuwa manne, ukatili wa kingono matukio manne, ukatili wa kihisia matukio 26 na utelekezaji wa familia matukio sita" alisema Kanoni 

Judith Mwakyusa ni wakili wa Serikali mwandamizi  amesema kwa kipindi cha Agosti hadi Novemba  mwaka huu kesi 68 za vitendo vya ukatili wa kijinsia zilipokelewa polisi na kisha kufunguliwa majarada mahakamani na kusikilizwa na kutolewa maamuzi ambapo kesi 48 kati ya hizo Jamhuri ilizishinda na hivyo wahusika kuchukuliwa hatua mbalimbali.

Amesema kesi za ukatili wa kijinsia zinazoongoza ni za watoto chini ya miaka 18 ambazo ni kesi 41za ubakaji kati ya 68,  matukio 28 yanahusu ukatili wa kudhuru mwili, ngono, ulawiti, utelekezaji na kuwa kesi nyingi zinashindwa kuendelea na kuondolewa mahakamani kutokana na walalamikaji kutohudhuria au wengine kuelewana na watuhumiwa au kugoma kutoa ushahidi.

"Mfano kuna kesi ya binti alibakwa akapata ujauzito kesi ikafikishwa mahakamani akahojiwa na kukubali mwisho wa siku alibadilisha na kusema mtuhumiwa aliyekuwa anashikiliwa hausiki na ujauzito huo, naishauri jamii kuondoa usiri pale wanapoona matendo ya ukatili yanaendelea katika jamii waripoti na kutoa ushirikiano kwa mamlaka zinapohitaji uthibitisho ili watuhumiwa wachukuliwe hatua kali”amesema Mwakyusa

Aidha ameeleza kuwa, wilaya ya Bukoba ndiyo inayoonekana kuongoza kwa matukio ya ukatili wa kijinsia 

yapatayo16, Missenyi 15, Muleba 14, Biharamulo 10, Ngara manane, Kyerwa matatu na mawili Karagwe.

Alinda Kajuna mkazi wa manispaa ya Bukoba aliiomba serikali kuwachukulia hatua wale wote wanaohusika na vitendo vya ukatili wa kijinsia kwani vinaharibu ndoto za watoto.

No comments