HEADER AD

HEADER AD

WANNE WADAIWA KUFA KWA KIPINDUPINDI KAGERA

Na Alodia Babara, Bukoba

MLIPUKO wa kipindupindu umezuka katika wilaya ya Misenyi mkoani Kagera na  kusababisha vifo vya watu wanne huku wengine watano wakiendelea na matibabu katika hospitali ya Kajunguti iliyopo wilaya ya Misenyi 
 
Mkuu wa mkoa wa Kagera Fatma Mwassa akizungumza na waandishi wa habari Desemba 04, 2023 amesema kuwa, ugonjwa huo umegundulika Novemba 29, mwaka huu katika kata ya Bugorola kijiji cha Buchurago.

"Ugonjwa huu umezuka Novemba 29, 2023 katika kijiji cha Buchurago baada ya watu wawili waliotokea nchi jirani ya Uganda kuingia kwenye kijiji hicho na mpaka sasa watu wanne wameishapoteza maisha.

Watano wanaendelea na matibabu na mmoja kati yao amegundulika kuwa na dalili katika kisiwa cha Goziba na watatu wameruhusiwa kurudi nyumbani kutoka hospitali" amesema Mwasa.

       Mkuu wa mkoa wa Kagera Fatma Mwassa

Aidha amewataka wananchi mkoani Kagera kuchukua tahadhari kwa  kuchemsha maji ya kunywa, kuosha matunda, kuepukana na mikusanyiko isiyo ya lazima ili kujikinga na mlipuko huo.

Baadhi ya wananchi wameomba serikali kutoa elimu kwao jinsi ya kujikinga na kipindupindu huku wakieleza kuwa wanausikia tu masikioni mwao lakini hawana elimu na namna gani wajikinge.

Savera Mutimavu mkazi wa Manispaa ya Bukoba ameiomba serikali kutoa elimu kwa wananchi juu ya ugonjwa huo kwani wananchi hao hawana uelewa juu ya ugonjwa huo.

No comments