WANANCHI 6223 KIJIJI CHA MWASHEGESHI KUNUFAIKA NA MRADI WA MAJI
Na Samwel Mwanga, Maswa
CHAMA cha Mapinduzi(CCM)wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu kimemtaka Mkandarasi anayetekeleza mradi wa maji katika kijiji cha Mwashegeshi ambao utawahudumia wananchi 6223 wa kijiji hicho kuongeza kasi na kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati.
Kauli hiyo imetolewa Desemba 3 mwaka huu na Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Maswa, Onesmo Makota wakati alipoambatana na kamati ya siasa ya wilaya hiyo kutembelea na kukagua mradi huo wa maji unaotekelezwa na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mjini Maswa(MAUWASA) utakaogharimu kiasi cha Shilingi 516,635,775/=.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Maswa,Onesmo Makota(wa pili kulia) akizungumza katika eneo linapotekelezwa Mradi wa Maji wa Kijiji Cha Mwashegeshi.
Amesema kuwa wananchi wa kijiji hicho wana shauku kubwa ya kutumia maji hayo ya bomba yanayotokana na chanzo cha maji cha bwawa la New Sola (Maarufu Bwawa la Zanzui)kwa kuwa kijiji cha Mwashegeshi ni miongoni mwa vijiji vilivyoko pembezoni mwa bwawa hilo lakini hakikuwa na maji ya bomba.
Amesema kuwa anaikubali miradi ya maji inayotekelezwa na MAUWASA kwani kazi zao zinaonekana na iliyo mingi inakwenda vizuri na hii itawasaidia wakirudii kwa wananchi kuwaomba kura kuna kitu cha kuonyesha katika eneo hilo.
Amewataka wananchi wamsimamie mkandarasi aweze kukamilisha mradi huo kwa wakati uliopangwa na Desemba 29 mwaka huu.
Tenki la kuhifadhi Maji Lita 100,000 linalojengwa kwenye Mradi wa Maji wa kijiji Cha Mwashegeshi wilayani Maswa.
“Nazikubali sana kazi zinazotekelezwa na MAUWASA kwa miradi ya maji, miradi yenu mingi inakwenda vizuri, msimamieni mkandarasi amalize mradi huu kwa wakati kama mlivyosema kuwa atamaliza Desemba 29 mwaka huu ili tunaporudi kuomba kura kwa wananchi katika eneo hili tunakuwa na kitu cha kuwaonyesha tulichokifanya kama mradi huu wa maji,”amesema.
Makota ameipongeza serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za kutosha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji katika wilaya hiyo ukiwemo mradi huo na kuwataka wananchi kuutunza pindi utakapokamilika.
"Kwa hiki kinachofanyika sasa tuna kila sababu ya kumpongeza Rais wetu Dkt Samia Suluhu Hassan tumepata fedha za kutosha katika miradi ya maji katika wilaya yetu ukiwemo mradi huu wa maji wa kijiji cha Mwashegeshi" amesema.
Pia amempongeza mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki Stanslaus Nyongo na Mbunge Mashimba Ndaki wa jimbo la Maswa Magharibi kwa kuweka msukumo mkubwa kwenye miradi hiyo ya maji katika wilaya ya Maswa.
"Tunaamini miradi ya maji ukiwemo huu itakamilika kwa wakati na watu wetu watapata maji ya uhakika na sisi kama chama tutaendelea kutoa msukumo kuhakikisha yale tuliyoyaahidi wakati wa kampeni yanatekelezeka na maji yanapatikana kwa wananchi,"amesema .
Mkuu wa wilaya ya Maswa, Aswege Kaminyoge amesema kuwa hali ya upatikanaji wa maji katika maeneo ya mjini katika wilaya hiyo imefikia asilimia 78.1 na ifikapo mwaka 2025 itafikia asilimia 95 kama inavyoeleza katika ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025 kutokana na kutekelezwa kwa miradi mbalimbali ya maji inayofanywa na MAUWASA.
Mkuu wa Wilaya ya Maswa,Aswege Kaminyoge(mwenye fulana rangi nyeusi) akizungumza katika eneo linapotekelezwa Mradi wa Maji wa Kijiji Cha Mwashegeshi.
“MAUWASA kwa sasa inatekeleza miradi mingi ya maji na ifikapo mwaka 2025 tutafikia lengo la utoaji wa maji asilimia 85 mjini kwa wilaya yetu ya Maswa kutokana na miradi tuliyonayo na kwa sasa hali ya upatikanaji wa maji kwenye maeneo ya mjini ni asilimia 78.1,”
“Hivyo pia niwaombe viongozi wa CCM tushirikiane na serikali kuhakikisha wananchi wa maeneo haya hawaingizi mifugo yao kwenye hifadhi ya bwawa la New Sola ambacho ndicho chanzo kikuu cha maji katika mji wa Maswa na Vijiji 11 kwani kwa sasa watapata maji kupitia mradi huo sambamba na mifugo yao,”amesema.
Mwalimu Mwashi Shilile ambaye ni mjumbe wa kamati ya siasa ya wilaya hiyo amesema kuwa serikali ya awamu ya sita imeonyesha kwa vitendo dhamira yake ya dhati ya kumtua mama ndoo kichwani kwa kutekeleza miradi ya maji ukiwemo mradi huo ambao utawapunguzia muda wakinamama wa kwenda kutafuta maji ukizingatia ndiyo wamekuwa na majukumu mengi katika kuhudumia familia.
Naye Diwani wa Kata ya Nguliguli,Peter Mliyandengu amesema kuwa maji hayo waliyasubiri kwa kipindi kirefu cha zaidi ya miaka 30 sasa wataanza kuyatumia mwishoni mwa mwezi huu
Ameiomba MAUWASA kuhakikisha maji hayo yanafika maeneo yote ya kijiji hicho hasa kwa wakati walioko karibu na bwawa hilo ili waweze kukitunza chanzo hicho cha maji.
Awali Mkurugenzi Mtendaji wa MAUWASA, Mhandisi Nandi Mathias akitoa taarifa ya mradi huo amesema kuwa kukamilika kwa mradi utasaidia uboreshaji upatikanaji wa maji safi na salama kwa matumizi ya binadamu.
Mkurugenzi wa MAUWASA,Mhandisi Nandi Mathias(wa kwanza kushoto)akisoma taarifa mbele ya Mwenyekiti CCM Wilaya ya Maswa,Onesmo Makota(wa kwanza kulia)taarifa ya ujenzi wa Maji katika Kijiji cha Mwashegeshi
Amesema utapunguza magonjwa yatokanayo na maji yasiyo salama na utasaidia uhifadhi wa bwawa la New Sola ambalo wananchi walio wengi wamekuwa wakipeleka mifugo yao kunywa maji.
Mhandisi Nandi amesema kuwa kwa sasa utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 67na unatekelezwa na Mkandarasi BAL BUILDER LTD wa Kidatu,Morogoro na kazi ambazo zimekwisha kufanyika ni pamoja na ulazaji wa bomba kilomita 11 na ujenzi wa vituo 6 vya kuchotea maji na ujenzi wa chemba 7
Amesema kuwa jitihada zingine zinazoendelea kufanyika ni pamoja na ujenzi wa tenki lenye uwezo wa kuhifadhi maji lita 100,000,ujenzi wa mbauti moja ya kunyweshea mifugo maji na ulazaji wa bomba za chuma kwenye mito lenye mita 180.
Mhandisi Nandi ameeleza changamoto ya kasi ya utekelezaji wa mradi ilipelekea ujenzi wa tenki kumpatia Mkandarasi mwingine kwa makubaliano ya pande zote za kimkataba.
Aidha alitumia fursa hiyo kukishukuru Chama cha Mapinduzi(CCM)kupitia Ilani yake ya uchaguzi ya Mwaka 2020-2025 iliyoelekeza huduma za maji Mjini kufikia asilimia 95.
MAUWASA inaendelea kupokea fedha za miradi ya maji kwa ajili ya utekelezaji wa ilani hiyo ili kufikia malengo ya kutua mama ndoo kichwani.
Ameishukuru serikali inayoongozwa na Rais,Dkt Samia Suluhu kwa kuendelea kutoa fedha kuwezesha miradi ya maji katika mamlaka hiyo.
Post a Comment