Home
/
Barabara
/
WANANCHI, WAFUGAJI NYAMONGO- KIBASUKA WAIOMBA SERIKALI IWAJENGEE DARAJA MTO TIGITE
WANANCHI, WAFUGAJI NYAMONGO- KIBASUKA WAIOMBA SERIKALI IWAJENGEE DARAJA MTO TIGITE
Na Dinna Maningo , Tarime
WANANCHI wa Kijiji cha Matongo, Kata ya Matongo -Nyamongo pamoja na wanachi wa Kijiji cha Nyarwana, Nyakunguru Kata ya Kibasuka, Wilaya ya Tarime mkoa wa Mara, wameiomba Serikali kuwajengea daraja ili kuwaondolea adha na usumbufu pindi wavukapo mto kwenda mnadani na mashambani.
Wakizungumza hivi karibuni na DIMA Online kandokando ya mto huo, wananchi na wafugaji wamesema kuwa kwa miaka mingi wamekuwa wakiteseka kuvuka mto kwa kuogolea ndani ya maji huku wengine wakivuka daraja la miti lililotengenezwa na mwananchi kwa kulipa sh. 1,000.
Daraja la miti lililojengwa na mwananchi ambalo mtu akivuka hutozwa sh.1000 kupita katika daraja hilo.
Wamesema kutokuwepo daraja la kisasa wanapata karaha kutokana na nguo zao kulowa maji na hivyo kujikuta wakichelewa mahali waendako wakisuburi nguo zikauke waendelee na safari.
Mwita Marwa mkazi wa kijiji cha Matongo -Nyamongo amesema kuwa mto huo umeshaua watu wakati wakivuka mto na wengine kuokolewa baada ya kusombwa na maji.
" Mto Tigite umekuwa kero sana kwa wananchi na mifugo ili uvuke maji unalazimika kuogelea, kuna watu walishakufa wakati wa kuvuka mto na wengine kusombwa na maji na kuokolewa.
"Wakati mwingine tunashidwa kwenda shambani kupalilia mazao pindi mvua inaponyesha nyingi mto hufurika maji, tunaomba serikali yetu itusaidie tunateseka sana."amesema Mwita.
Makuri Matiko mkazi wa Itandora amesema kuwa kukosekana kwa daraja baadhi ya wananchi wanalazimika kuvuka kwenye daraja la miti lililotengenezwa na mwananchi ambapo kila mtu hutozwa sh. 1000 na wengine hushindwa kuendelea na safari baada ya kukosa pesa ya kulipa.
"Mwananchi mmoja alijitolea akatengeneza daraja la miti ili uvuke unalipa sh. 1000, kwenda na kurudi kwa mtu mmoja, wasio na fedha huogekea na wasiofahamu kuogelea ukatisha safari, hali hii inarudisha nyuma maendeleo ya wanachi wa vijijini" alisema Makuri.
Ghati Chacha mkazi wa kijiji cha Nyarwana amesema kuwa wanawake na watoto wanashindwa kwenda mnadani kwakuwa sio wengi wenye uwezo wa kuogelea.
Mnada
" Wengi hatujui kuogelea na wengine wanakosa sh.1000 ya kulipa kuvukadaraja, matokeo yake tunashindwa kununua mahitaji au kuuza bidhaa zetu mnadani." alisema Ghati.
Chacha Mwita mkazi wa kijiji cha Nyarwana amesema kuwa wanateseka kuvusha mifugo kwenda kuuza mnadani kwakuwa pindi maji yanapokuwa mengi mifugo kama ng'ombe na mbuzi huogopa kuvuka mto jambo ambalo linawakosesha fedha kutekeleza mahitaji yao.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nyabibago, Kijiji cha Matongo, Chales Ryoba amesema kuwa wananchi wanaopita ni wengi hasa baada ya kuwekwa mnada katika Kitongoji hicho .
"Tangu mnada uletwe hapa watu wengi wamekuwa wakivuka mto kuleta bidhaa zao na mifugo na wengine kununua mahitaji, wanateseka sana kwenye huu mto.
Amesema kuwa changamoto hiyo ilishafikishwa hadi kwa Meneja Wakala wa barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) wilaya ya Tarime na aliahidi kushughulikia swala hilo lakini bado changamoto hiyo haijazaa matunda.
Meneja Wakala wa Barabara Vijijini na Mjini (TARURA) wilaya ya Tarime Mhandisi Charles Marwa amesema kuwa changamoto hiyo anahifahamu na kwamba tayari swala hilo limeshafikishwa serikalini na pindi fedha zitakapopatikana daraja hilo litajengwa.
Post a Comment