HEADER AD

HEADER AD

AFISA USHIRIKA, KILIMO KIZIMBANI KWA KUJIPATIA FEDHA KWA UDANGANYIFU

Na Mwandishi Wetu, Simiyu

AFISA Ushirika mkoa wa Simiyu, Mustafa Kimomwe pamoja na wenzake wawili wamefikishwa katika Mahakama ya wilaya ya Maswa mkoa wa Simiyu wakikabiliwa na shtaka la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kiasi cha Sh Milioni 1.3

Wengine waliofikishwa mahakamani ni pamoja na Baraka Azikiwe na Akram Abubakari ambao wote ni Maafisa kilimo wilaya ya Bariadi.

Washtakiwa hao wote kwa pamoja wamesomewa shtaka hilo na Wakili wa Serikali,Vaileth Mushumbusi na Mwendesha Mashtaka, Mkaguzi wa Polisi Yusuph Majombo wote kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka wilaya ya Maswa mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Hamis Mzee.

Ilidaiwa mahakamani hapo kati ya mwezi Julai na Agosti 2023 katika wilaya ya Maswa washtakiwa wakiwa na nia ya kudanganya walijipatia kiasi cha Tsh. Milioni 1.3 kutoka kwa viongozi wa Vyama Vya Msingi vya Ushirika vya Mwadila na Mwasita kinyume cha sheria.

Imeelezwa mahakama hapo kosa hilo ni kinyume cha kifungu 102 cha Makosa ya Jinai, Kanuni ya adhabu sura 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

       Sehemu ya jengo la Mahakama ya Wilaya ya Maswa

Baada ya Washtakiwa hao kusomewa maelezo ya kosa wanalodaiwa kulitenda walikana na upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.

Hakimu Mzee amesema dhamana ipo wazi kwa washitakiwa hao hivyo wanatakiwa kuwa na mdhamini mmoja kwa kila mshtakiwa wanaotambuliwa kisheria na watakaokidhi vigezo vya dhamana.

Kesi hiyo imehairishwa hadi Februari 7 mwaka huu kwa ajili ya washtakiwa kusomewa hoja za awali.


No comments