CHATO YAKUMBWA NA KIPINDUPINDU, DC AAGIZA MWALO UFUNGWE
Na Daniel Limbe, Chato
WAKATI serikali ikiendelea kutoa tahadhali ya mvua kubwa zinazoendelea kunyesha pamoja na kuimalisha usafi wa mazingira nchini, mwanamke mmoja wilayani Chato mkoani Geita ameripotiwa kupatikana na ugonjwa wa kipindupindu.
Mgonjwa huyo (jina limehifadhiwa) ni wa kwanza kubainika kuwa na ugonjwa huo ndani ya wilaya ya Chato licha ya mkoa wa Geita kusajili jumla ya wagonjwa 8 baada ya wengine saba kupatikana wilayani Mbongwe huku kukiwa na kifo kimoja kati ya wagonjwa hao.
Kutokana na hali hiyo, Mkuu wa wilaya ya Chato, Mhandisi Deusdedith Katwale, amefika eneo alilobainika mgonjwa huyo kwenye mwalo wa samaki wa Miembeni uliopo kijiji cha Nyabugera Kata ya Mganza ili kuwathibitishia wananchi uwepo wa mlipuko wa ugonjwa huo, kuchukua tahadhari za kiafya pamoja na kutoa elimu ya kujikinga na maradhi hayo.
Mkuu wa wilaya ya Chato,mhandisi Deusdedith Katwale,akizungumza na wananchi wa Nyabugera ili kujikinga na kipindupindu.
Katika kunusuru kueneza kwa ugonjwa huo, Katwale amelazimika kutoa kauli ya serikali kwa kuufunga kwa muda mwalo wa samaki wa Miembeni ili kushinikiza wananchi kuchimba vyoo kwaajili ya matumizi ya kibinadamu baada ya kubaini baadhi ya wavuvi kujisaidia kwenye makazi ya watu na wengine vichakani kinyume cha kanuni za afya.
Akitoa elimu kwa Umma, Kaimu Mganga mkuu wa wilaya hiyo, Dkt Deogratias Kubanzibwa, amesema baada ya mgonjwa mmoja kupatikana eneo hilo hatua za haraka zimechukuliwa kuhakikisha mgonjwa anaanzishiwa matibabu ya haraka kwenye kituo cha afya Mganza na kwamba hali yake inaendelea kuimarika ukilinganisha na awali.
Ametumia fursa hiyo kuwataka wote watu wote walioshirikiana na mgonjwa huyo tangu alipowasili eneo hilo kujitokeza ili wafanyiwe vipimo iwapo wameambukizwa vimelea vya ugonjwa wa kipindupindu ili waanzishiwe matibabu haraka kwa lengo la kunusuru kutokea maambukizi mapya ya ugonjwa huo.
Mkuu wa wilaya ya Chato,Mhandisi Deusdedith Katwale,(aliyesimama kwenye jiwe) akipokea maoni ya wananchi.
Kadhalika amewataka kuzingatia kanuni za afya na usafi wa mazingira ikiwa ni pamoja na kutumia vyoo, kunawa mikono kwa maji safi na sabuni baada ya kutoka chooni na kabla ya kula.
Pia kunywa maji yaliyochemshwa au kutibiwa kwa dawa za maji (Walter Guard) kula vyakula vyenye joto pamoja na kutunza na kulinda usafi wa mazingira yanayo wazunguka.
Mwenyekiti wa usimamizi wa raslimali za uvuvi ndani ya ziwa Victoria (BMU) Mwalo kwa Miembeni, Gady Rashidi, amekiri jamii ya wavuvi kutozingatia sheria na kanuni za usafi wa mazingira huku akimshukuru maelekezo ya serikali yenye lengo la kunusuru maisha ya jamii.
Hata hivyo ombi la Mwenyekiti wa kijiji cha Nyabugera, Methusela Mgema, kutaka mwalo huo usifungwe ili kuruhusu shughuli za uzalishaji mali kwa jamii hiyo ziendelee wakati jitihada za uchimbaji wa matundu matatu ya vyoo ukifanyika zimegonga.
Mkuu wa wilaya amesema maelekezo aliyotoa kwa wananchi hao yanatoka moja kwa moja Wizara ya afya.
Post a Comment