SERIKALI ILIVYOVUTIWA NA UTENDAJI KAZI WA MKURUGENZI MWAUWASA MRADI WA MAJI BUTIMBA
>>Waziri Aweso asema alivyomteua kelele zilikuwa nyingi kwamba hajasomea Uhandisi
>>>Kitaaluma Neli Msuya alikuwa Afisa Habari kabla yakuwa Kaimu Mkurugenzi MWAUWASA
Na Nashon Kennedy, Mwanza
Wataalam wa uchumi wanasema pamoja na kwamba kazi ni ajira bali pia ni kipimo cha utu ambacho humfanya mhusika kuheshimika katika jamii na kuwa sehemu ya kuongeza tija katika uchumi wake na wa taifa lake.
Neli Msuya ni Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira jijini Mwanza, amekuwa kivutio kikubwa kutokana na utendaji wake wa kazi katika kusimamia mradi wa maji Butimba mkoani Mwanza.
Hivi karibuni mwezi Januari, 2024, Serikali kupitia Wizara ya Maji na Kamati ya Bunge ikatoa pongezi kwa Mkurugenzi huyo.
Waziri wa Maji Jumaa Aweso akizungumza mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti iliyokuwa kwenye ziara ya kikazi jijini humo na kuutembelea mradi huo kuona jinsi unavyotoa huduma kwa wananchi anampongeza Msuya kwa usimamizi wa mradi.
Waziri Aweso anasema Neli Msuya licha ya kuteuliwa kwa muda mfupi kuiongoza MWAUWASA , amefanya kazi kubwa na ya mfano wa kuigwa .
Aweso aanasema hali ambayo MWAUWASA imepitia katika kipindi kifupi kilichopita ilikuwa ngumu kutokana na kuwepo changamoto nyingi, hatua ambayo ilisababisha Wizara kufanya mabadiliko ya haraka ya uongozi uliokuwepo.
“ Tulikuwa tunaumiza kichwa, tumlete nani MWAUWASA, ili aje ku rescue situation, mwenyezi Mungu akatuongoza, nikamuomba dada yangu Neli Msuya aje hapa kukaimu”, anasema Aweso.
Kwani lazima Wahandisi tu ?
Aweso anasema licha ya kumteua Msuya kwenda kuiongoza mamlaka hiyo ya maji, kitaaluma hakuwa Mhandisi ni Ofisa Habari lakini amefanya kazi bila kutetereka wala kuyumba.
Waziri Juma Aweso akiteta jambo na Mkurugenzi wa MWAUWASA Neli Msuya
“Nilipomteua kelele zilikuwa nyingi sana, kwamba yeye sio Engineer (Mhandisi), niwaambie ndugu zangu, tunapozungumzia MD kwa maana ya Mkurugenzi yeye ni Managing Director kazi yake ni kuwaongoza watu" anasema Waziri Aweso.
Anasema tangu ateuliwe ndani ya muda mfupi kuiongoza mamlaka hiyo, jiji la Mwanza limekuwa kimya na ameusimamia mradi wa maji Butimba umekamilika na umeanza kutoa huduma ya maji.
“Ame manage (ongoza) watumishi vizuri, ameikabili siasa iliyohusu maji, ame manage mradi na umeimarika, wanawake wanaweza tena wanaweza sana”, anasema.
Waziri huyo anaiomba Bodi ya MWAUWASA wasichelewe kumpandisha cheo kuwa Mkurugenzi Mtendaji Kamili wa Mamlaka hiyo ya maji.
“ Msimcheleweshe kumpandisha cheo, leteni jina lake nilithibitishe”, anasema Waziri Aweso.
Blandiya Elikana ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza anaieleza Kamati hiyo ya Bunge kuwa, kukamilika kwa mradi huo wa maji wa Butimba unakwenda kupunguza adha kubwa ya maji ambayo ilikuwa inawakabili wakazi wa jiji la Mwanza.
Anaishukuru serikali kwa kuupatia mkoa wa Mwanza fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati likiwemo daraja kubwa na la kisasa la Kigongo-Busisi ambalo ni la pili kwa ukubwa Afrika Mashariki.
“Daraja hili litatusaidia sana katika kuhakikisha usafiri wa abiria na bidhaa unakuwa rahisi, ipo miradi mingi ikiwemo vijijini ambayo itasaidia kutatua changamoto za maji”, anasema Elikana.
Agizo kwa MWAUWASA
Katika hatua nyingine, Waziri Aweso anaiagiza Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira jijini Mwanza (MWAUWASA) kuhakikisha kuwa wakazi wa jiji la Mwanza wanaunganishiwa huduma ya maji kutoka kwenye mradi wa maji Butimba ambao kwa sasa umekamilika.
Wajumbe wa kamati hiyo na watalaam wa maji wakiwa kwenye mradi wa maji wa Butimba.
Aweso amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kiasi cha Tsh. Bilioni 82 zilizowezesha kukamilika kwa mradi huo mkubwa.
Anaitaka mamlaka hiyo kutokuwa na sababu ya watu kushindwa kuunganishiwa huduma za maji hasa baada ya kukamilika kwa mradi huo unaozalisha lita milioni 48 kwa siku na wenye uwezo wa kuhudumia watu 450,000.
Anasema mwananchi yeyote anayehitaji kuunganishiwa maji, aunganishiwe huduma hiyo kwa muda mfupi ili wananchi wa jiji la Mwanza waweze kufurahia huduma ya maji safi na salama kupitia mradi huo.
“Naipongeza sana Bodi ya Maji kwa usimamizi na ufuatiliaji mzuri wa mradi huo na tumeona Mkandarasi amefanya kazi yake.
"Naushukuru pia uongozi wa chama na serikali ya mkoa wa Mwanza kwa usimamizi na ufuatiliaji mzuri wa mradi huo wakati wote tangu ulipoanza kijengwa.
Mwelekeo wa Serikali
Waziri Aweso anasema mwelekeo wa serikali na Wizara ya Maji chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ni ujenzi wa miradi mikubwa ya maji ya kimkakati.
Walioketi kushoto niWaziri wa Maji Jumaa Aweso, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Bajeti Danieli Siro akifuatiwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Omary Kigua wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa kamati hiyo katika mradi wa chanzo cha maji Butimba
Anasema kwa sasa serikali kupitia Wizara ya maji inasimamia ujenzi wa miradi katika miji 28 kwenye maeneo yaliyoainishwa kuwa na changamoto kubwa ya maji
“Kila eneo kwa sasa lina mkandarasi wa utekelezaji wa miradi hiyo ya miji 28”, anasema.
Anasema Rais Samia ameipatia maelekezo Wizara ya Maji kuwa ifikapo mwaka 2025 asilimia 85 ya upatikanaji wa maji uwe vijijini na asilimia 95 iwe mjini.
“Sasa hivi tuna asilimia 88 ya upatikanaji maji mjini na asilimia 77 ya upatikanaji wa maji vijijini”, anaesema.
Anasema kuna miradi ya maji zaidi ya 244 inayotekelezwa kwa hivi sasa nchini na kwamba kukamilika kwa miradi hiyo maeneo ya mjini itawesha kufikiwa kwa asilimia 95 ya upatikanaji maji mjini ifikapo 2025.
Anaongeza kusema kuwa ipo miradi mingine zaidi ya 1500 inayotekelezwa maeneo ya vijijini na kwamba jukumu la wizara ni kuhakikisha miradi yote inasimamiwa kuhakikisha inakamilika kwa wakati ili serikali iweze kufikisha lengo la kutoa huduma ya maji vijijini la asilimia 85 ifikapo mwaka 2025.
Anasema Rais Samia ameipatia Wizara ya Maji magari ya uchimbaji visima kwa kila mkoa kwa ajili ya uchimbaji wa visima kwa takribani vijiji 2000 vinavyopata huduma ya maji ambayo sio ya uhakika.
Neli Msuya wa kwanza kulia akiwa na baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Mwauwasa, wakimsikiliza Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Bajeti Danieli Siro( hayupo pichani).
“ Hatutegemei Wahandisi wa mikoa ama wilaya ambapo magari hayo yamepelekwa, halafu yasifanye kazi, lazima yatumike kwa ajili uchimbaji wa visima ili watu waweze kupata huduma ya maji safi na salama ”, anasema.
Akizungumza mara baada ya kupokea wajumbe wa kamati hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza anaipongeza kamati hiyo ya Kudumu ya Bunge kwa usimamizi mzuri wa bajeti ya serikali.
RC Makalla anasema kuwa kwa muda mrefu kamati imekuwa na changamoto kubwa ya maji na kukiri kwamba hata yeye binafsi alipokuwa Naibu Waziri wa Maji alipata malalamiko mengi ikiwemo maji kusafirishwa kutoka ziwa Victoria kwenda mikoa ya Shinyanga na Tabora wakati mkoa wa Mwanza haupati huduma za maji za kutosha.
Anasema ujio wa kamati hiyo katika mkoa wa Mwanza, watu wafahamu kuwa mkoa wa Mwanza ni mkoa wa pili kwa kila jambo hapa nchini, ikiwemo idadi ya watu baada ya jiji la Dar es Salaam na kwa kuchangia katika pato la uchumi la taifa baada ya Dar es Salaam.
Anasema mkakati wa mkoa wa Mwanza ni kuona mkoa huo unakuwa wa kwanza kiuchumi kutokana na kazi kubwa na nzuri inayofanywa Rais Samia katika mkoa huo ikiwemo utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati.
Makalla anasema mradi wa maji Butimba ni mradi mkubwa wenye mitambo ya kisasa na utazalisha jumla ya lita za maji milioni 48 kwa siku na kwamba kwa kiasi kikubwa mradi huo utapunguza upungufu wa maji katika jiji la Mwanza.
Kamati ya Bunge yapongezwa
Waziri Aweso anaishukuru Kamati hiyo kwa kuendelea kuipatia fedha Wizara ya Maji kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji.
Anasema miaka ya nyuma, Wizara hiyo ilikuwa ni Wizara ya kero na lawama na moja ya changamoto kubwa iliyokuwa inaikabili ilikuwa ni suala zima la upatikanaji wa fedha.
Anasema ipo miradi ambayo ilijengwa yeye akiwa bado shuleni anasoma lakini ilikuwa bado haijakamilika akiutolea mfano mradi wa maji Mugumu ulioko wilayani Serengeti ambao ulijengwa tangu mwaka 1980 lakini bado haujakamilika.
Aweso anesema katika kila kipindi cha bajeti, changamoto kubwa imekuwa ni ufinyu wa bajeti lakini Kamati hiyo ya bajeti imekuwa ikitenga fedha kila ilipopatikana na kuiwezesha Wizara kutekeleza miradi ya maji kwa awamu katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Anasema mafanikio hayo yametokana na mchango mkubwa wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti ambapo aliwapongeza viongozi wa Kamati hiyo na wajumbe wote.
“Sijui nitumie lugha gani Mwenyekiti wa Kamati ambayo unaweza kuielewa, lakini kwa dhati ya moyo wangu, kabla Wizara hatujapita kwenye bajeti kuu ya serikali, mmekuwa mkituita na kutuelekeza”, anasema.
Anasema mahitaji ya maji katika jiji la Mwanza ni lita milioni 172 lakini uzalishaji wa maji katika jiji hilo unaofanywa na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira (Mwauwasa) kupitia chanzo chake cha maji cha Capripointi lina uwezo wa kuzalisha maji lita milioni 90 tu.
Anasema kutokana na hali hiyo jiji hilo linakabiliwa na upungufu mkubwa wa maji wa takribani lita milioni 182 na kufafanua kuwa changamoto nyingine kubwa inayosababisha kuwepo kwa kelele zinakuwa nyingi ili hali wananchi hawana maji ni kuona ziwa Victoria liko karibu na wananchi hawana maji.
“ Nitumie nafasi hii kumshukuru Rais kwa kutupatia fedha zaidi ya euro milioni 31 zilizotusaidia kujenga mradi wa maji Butimba”, amesema.
Aidha amewapongeza wabunge wote wa jiji la Mwanza na Ilemela kwa kuwapigania wananchi wao ndani na nje ya bunge na kuhakikisha mradi huo mkubwa wa maji Butimba umetafutiwa fedha na serikali na kujengwa na hivi karibuni utaanza kutoa huduma ya maji.
“Kwa namna ya kipekee nimpongeze Mkuu wa Mkoa kwa usimamizi wa mradi huu pamoja na Kamati yakeya Usalama Mkoa, alikuwa Mhandisi Mkuu, kwenye usimamizi wake, wakati mwingine alioa maelekezo magumu sana”, amesema.
Amesema Mkuu huyo wa mkoa aliusimamia mradi huo kwa karibu kutokana na kuwa mzoefu wa Wizara hiyo ya maji, ambapo aliwahi kuwa Naibu wa Wizara hiyo na kwamba changamoto za maji anazifahamu.
PONGEZI KWA AWESO
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Amos Makalla amempongeza Waziri wa Maji Jumaa Aweso kwa kazi kubwa anayoifanya ya ufuatiliaji, usimamizi na utekelezaji wa miradi ya maji nchini.
Anasema mradi huo wa maji wa Butimba utawanufaisha wakazi wa Nyamagana, Ilemela, Misungwi na Magu na anaipongeza kamati hiyo kwa usimamizi mzuri wa fedha za bajeti zinazotolewa na serikali kwa ajili ya utelelezaji wa miradi maendeleo nchini.
Bunge laridhishwa na mradi
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Daniel Siro amepongeza Bunge kuhidhinisha fedha mradi wa maji wa Butimba uliojengwa kwa Tsh. Bilioni 82.
Aidha kamati hiyo inaupongeza uongozi wa Mkoa wa Mwanza kupitia kwa Mkuu wa Mkoa wa Amos Makalla na uongozi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira( Mwauwasa) kwa usimamizi mzuri wa mradi huo ambao umekamilika na umeanza kutoa huduma.
“Sisi kama Kamati inayosimamia uchumi wa bajeti ya nchi hii na utekelezaji wake tunaipongeza serikali , kazi nzuri imefanyika hapa na tumeridhika na kazi inayoendelea kupitia mradi huu”, anasema.
Maiko Joseph mkazi wa jijini Mwanza anasema mamlaka ya maji Mwanza inafanya kazi kubwaya usambazaji wa huduma za maji.
Anasema jiji la Mwanza kwa sasa linakabiliwa na idadi kubwa ya watu ambayo pengine inaweza ikaonekana mamlaka hiyo haimalizi changamoto ya maji kwa haraka.
“Binafsi MWAUWASA inajitahidi kwenye suala la huduma ya maji, wanastahili kila siku utaona wanahangaika kila mahali kutatua changamoto za maji”, anasema Maiko.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Bajeti Danieli Siro akinawa mikono baada ya kupanda mti kwenye mradi wa maji Butimba.
Rejea
>>>Neli Msuya Mwaka 2022 akiwa Mkurugenzi wa Mawasiliano DAWASA alishinda Tuzo ya Afisa Mawasiliano Bora kutoka Sekta ya Maji na Usafi wa Mazingira ( Best Public Relations Practitioner of the year 2022, Water &Sananitation Sector).
Post a Comment