HEADER AD

HEADER AD

DC MASWA : BODABODA WOTE WAWE NA LESENI

Na Samwel Mwanga, Mwanga

MKUU wa wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Aswege Kaminyoge amewataka madereva wote wa pikipiki za kusafirisha abiria maarufu kwa jina la bodaboda kuwa na leseni ambazo zinaruhusu kuendesha vyombo hivyo vya moto kwani suala hilo lipo kisheria.

Ametoa agizo hilo Januari 24 mwaka huu wakati akizungumza na madereva wa bodaboda mjini Maswa kusikiliza changamoto ambazo wanakutana nazo katika kufanya shughuli zao za kusafirisha abiria katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya hiyo.

Amesema kuwa asilimia kubwa ya madereva hao hawana leseni za kuendesha vyombo hivyo jambo ambalo ni kinyume cha sheria za usalama barabarani ambazo zinamtaka kila mmoja anayeendesha chombo cha moto kuwa na leseni ya udereva.

       Mkuu wa wilaya ya Maswa mkoani Simiyu,Aswege Kaminyoge (aliyesimama) akizungumza na madereva wa bodaboda, bajaji, baiskeli na magari madogo wanaofanya biashara ya kusafirisha abiria.

Dc Kaminyoge amesema kuwa suala la kuwa na leseni halikwepeki na ni kibali ambacho kinamruhusu kuendesha pikipiki hiyo na itasaidia kuwa suluhisho la ajali zisizo za lazima hivyo ni lazima wapate mafunzo ya udereva na kupata cheti na ndipo wapate leseni hizo.

“Madereva wote wa bodaboda katika wilaya ya Maswa ni lazima wawe na leseni na kwa tafsiri rahisi ya lugha ya Kiswahili ni kibali au ruhusa ya kuendesha hiyo pikipiki,”amesema.

Katika kuhakikisha madereva hao wasiyo na leseni wanapata mafunzo ya udereva kabla ya kupata leseni hizo amemwagiza Mkuu wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Binza(Binza VTC)ambacho pia kinatoa mafunzo ya awali ya udereva kutoa mafunzo bure  ya muda mfupi wa siku tatu kwa madereva hao ili waweze kupata vyeti na hatimaye waombe leseni za udereva kupitia jeshi la polisi.

        Madereva wa bodaboda mjini Maswa wakiondoka baada ya kikao Chao na Mkuu wa wilaya ya Maswa.

“Nakuagiza Mkuu wa chuo cha Binza VTC ambacho ni chuo cha serikali kilichoko katika wilaya yetu kuandaa program ya kutoa bure mafunzo ya muda mfupi wa siku tatu tatu kwa madereva wote wa bodaboda katika wilaya ya Maswa ili waweze kupata vyeti.

"Hatimaye waombe leseni kupitia jeshi la polisi na wale walioko nje ya makao makuu ya wilaya wafuateni huko huko walipo serikali itatoa mafuta ya gari nah ii ofa natoa mwisho ni januari 30 mwaka huu,”amesema.

Mkuu wa kikosi cha Usalama barabarani wilaya ya Maswa, Mkaguzi msaidizi wa Polisi, James Nyorobi amesema kuwa madereva bodaboda na wengine wa magari madogo ya kusafirisha abiria wamekuwa wakiendesha vyombo hivyo bila ya kuwa na leseni.

   Mkuu wa Polisi wilaya ya Maswa,SSP Maganga Ngosha (aliyesimama) akizungumza na madereva wa bodaboda,bajaji,baiskeli na magari madogo.

Amesema hali hiyo hujikuta wakikamatwa na kupigwa faini kwa mujibu wa sheria na pia wamekuwa wakiwapatia elimu ili waweze kupata mafunzo ya udereva na hatimaye kupata leseni hizo.

Amesema kuwa watumishi wa serikali katika wilaya hiyo wanatumia pikipiki za serikali wengi wao hawana leseni hivyo amewaomba na wenyewe wachangamkie fursa hiyo iliyotolewa na Mkuu wa wilaya ya Maswa ili waweze kupata mafunzo na hatimaye watunukiwe vyeti na kupata leseni zitakazowawezesha kuendesha pikipiki hizo.

Katibu tawala wa wilaya ya Maswa, Athuman Kalanghe ametoa ushauri kwa madereva hao kutojihusisha na vitendo vya uhalifu na pindi wanapoona vinatokea ni vizuri kutoa taarifa katika vyombo vya ulinzi na usalama na hasa jeshi la polisi ili hatua zichukuliwe mara moja.

“Kuna matukio ya uhalifu yanatokea usiache kutoa taarifa kwenye kituo cha polisi,watu wa namna hiyo wapo wengi kwenye vituo vya bodaboda wamejificha humo. 

" Utakuta anapotea tu hajulikani alipo kumbe amekwenda kufanya vitendo vya uhalifu akirudi ni visingizio kibao mkiwagundua watu wenye tabia hizo toeni taarifa ili washughulikiwe na pia jipeni muda wa kupumzika,”amesema.

Naye Mkuu wa Polisi wilaya ya Maswa, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi(SSP)Maganga Ngosha amesema kuwa kumekuwa na wimbi wa wizi wa pikipiki hizo za bodaboda hivyo kwa sasa wanakuja na mwarobaini ambao ni kuzifunga GPS pikipiki zote ili inapoibiwa waweze kuifuatilia na kuwakamata wezi.

“Kwa sasa tunaibiwa sana pikipiki licha ya kupambana na wizi huo kwa sasa tutakuja na utaratibu wa kuzifungia GPS kila pikipiki na kutakuwa na gharama kidogo hivyo niwaombe tutakapoanza utaratibu huo mtuunge mkono na lengo kubwa ni kukomesha vitendo hivyo,”amesema.

Nao baadhi ya madereva wa bodaboda wameeleza changamoto zinazowakabili katika kufanya shughuli zao za kila siku na mojawapo ni kutokuwa na maeneo mazuri kwa ajili ya vituo vya kuegesha pikipiki zao, kubambikiwa kesi katika kituo cha polisi na mikataba wanayoisani na watu wanaowapatia pikipiki kuwa si rafiki kwao.

Nzengo Kilala amesema kuwa wanapokamatwa kwa makosa ya usalama barabarani lakini wakifika katika kituo cha polisi wanabambikiwa kesi nyingine nzito na matokeo yake wananyimwa dhamana hadi wapate msaada kutoka kwa viongozi wa serikali akiwemo Mkuu wa wilaya.

Frank Gamuga amesema kuwa mikataba ambayo inafungwa kati yao na mwenye pikipiki kwa upande mmoja inakuwa si rafiki kwao hivyo wameiomba serikali iweze kuwatengenezea mkataba wa kisheria ambao utakuwa na ulinganifu kwa pande zote mbili.

Wiston Sleum amesema kuwa kwa sasa hawana maeneo mazuri kwa ajili ya maegesho ya pikipiki zao kwa baadhi ya vituo wamekuwa wakikaa maeneo ambayo ni hatarishi wa usalama wao na pikipiki zao na hivyo kuiomba serikali kuwapatia maeneo ya maegesho ambayo yatakuwa salama kwao.




No comments