HEADER AD

HEADER AD

MAKAMU WA RAIS NCHINI CUBA AKAGUA KIWANDA CHA TBPL PWANI


Na Gustafu Haule, Pwani

MAKAMU wa Rais wa Muungano wa nchi ya Cuba Salvador Valdes Mesa amefanya ziara ya kutembelea na kukagua kiwanda cha Tanzania Biotech Products  Limited (TBPL) kilichopo Kibaha Mkoani Pwani.

Kiwanda hicho kimejengwa kwa ushirikiano wa nchi mbili ikiwemo Tanzania na Cuba ambapo kazi yake ni kuzalisha viuadudu wa kutokomeza mazalia ya Mbu pamoja na kutengeneza dawa mbalimbali kwa ajili ya kuua wadudu wanaoshambulia mazao.

Kiongozi huyo kutoka nchini Cuba amefanya ziara hiyo Januari 24 mwaka huu  akiambatana na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Tanzania akiwemo Balozi anayewakilisha Tanzania nchini Cuba Humphrey Pole pole.

      Makamu wa Rais wa nchi ya Cuba Salvador Valdes Mesa akizungumza na viongozi mbalimbali wa Serikali katika kiwanda cha kuzalisha viuadudu wa mazalia ya Mbu.

Viongozi wengine waliokuwepo katika msafara huo ni Waziri wa Viwanda na Biashara Ashatu Kijaji ,Waziri wa afya Ummy Mwalimu,Waziri wa Maliasili na Utalii Angellah Kairuki wakipokelewa na mwenyeji wao Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge.

Aidha akiwa katika kiwanda hicho  makamu huyo wa Rais alitembelea na kukagua maeneo mbalimbali ya uzalishaji katika kiwanda hicho na kisha kuzungumza na  viongozi mbalimbali pamoja wafanyakazi wa kiwanda hicho.

Katika hotuba yake Makamu wa Rais Valdes Mesa, amesema kuwa anashukuru kwa kufanya ziara hiyo nchini Tanzania hasa katika kutembelea kiwanda hicho na kwamba historia ya nchi hizo mbili ilianza miaka mingi hususani katika maeneo ya ushirikiano ya uwekezaji.

      Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge (Kulia) akimpokea Makamu wa Rais wa nchi ya Cuba.

Amesema uanzishwaji wa kiwanda hicho umetokana na mazungumzo ya pamoja na viongozi wa juu ambapo lengo lake ni kutokomeza Malaria na kwamba kiwanda hicho ni kikubwa barani Afrika.

Amesema Cuba itaendelea kutoa ujuzi kwa ajili ya kuendeleza kiwanda hicho ili kiweze kuzalisha dawa za kutokomeza viuadudu wa Malaria na hata kuua wadudu wanaoshambulia mazao.

     Baadhi ya viongozi walioshiriki ziara ya Makamu wa Rais wa Cuba jana Mjini Kibaha.

"Ujio wangu hapa ni mara ya pili kwani mara ya kwanza nilikuja mwaka 2016 na leo 2024 nimekuja tena, lakini yote haya tunafanya kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano wetu hasa katika kuhakikisha kiwanda hiki kinazidi kuimarika,"amesema Valdes Mesa Makamu wa Rais wa Cuba.

Hatahivyo, amesema umuhimu wa kiwanda hicho ni mkubwa kwani licha ya kuzalisha viuadudu wa Malaria lakini pia ni sehemu ya kutoa ajira kwani mpaka sasa kiwanda kimetoa ajira zipatazo 100.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge, awali akizungumza kabla ya kumkaribisha Makamu wa Rais , amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan Kwa kufanyakazi kubwa ya kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji.

  Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge akizungumza na viongozi mbalimbali katika ziara ya Makamu wa Rais wa Cuba.

Ametumia nafasi hiyo kuwakaribisha watu kutoka nchini Cuba kuja kuwekeza Tanzania hususani Mkoa wa Pwani kwakuwa mazingira ya uwekezaji ni mazuri na Mkoa upo tayari kutoa ushirikiano kwa wawekezaji hao.

     Baadhi ya madaktari na wafanyakazi wa kiwanda cha viuadudu kilichopo Kibaha katika ziara ya Makamu wa Rais wa nchini Cuba

.


No comments