JAJI MTULYA : WANANCHI TUMIENI WIKI YA SHERIA KUPATA HUDUMA ZA MAHAKAMA
Na Jovina Massano, Musoma
WANANCHI mkoani Mara wameshameuriwa kuitumia wiki ya sheria kupata huduma za mahakama na kuijua mahakama ya Tanzania na wadau wake .
Hayo yamesemwa Januari 24/2024 na Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, Fahamu Mtulya alipokuwa anaongea na mwandishi wa DIMA ONLINE Mahakamani hapo.
Aidha amesema kuwa kila mtanzania anayo haki kikatiba kupata habari za nchi na mambo mbalimbali kama ibara ya 18 inavyoelezea haki ya kupata taarifa.
Amesema mahakama kwa kushirikiana na wadau wa sheria wameanza na maonesho kuwezesha wananchi kupata elimu ya huduma za taasisi mbalimbali.
Amesema watu wengi hawana uelewa juu ya sheria isipokuwa pale tatizo litakapotokea ndipo hufika kupata elimu ya sheria.
"Mahakama Kanda ya Musoma pamoja na wadau wote wa kisheria tumejipanga kutoa elimu ya sheria kwa wananchi bure katika wiki hii kuelekea siku ya sheria bila malipo yeyote", amesema Mtulya.
Ameongeza kwa kuainisha taasisi na wadau wa kisheria waliopo katika maonesho hayo yanayoendelea uwanja wa shule ya msingi Mukendo kuwa ni Mahakama, Baraza la usuluhishi na Uamzi (CMA), TRA ,TTCL, Baraza la Ardhi na nyumba, Kamishna msaidizi wa Ardhi, NSSF, Ofisi ya Taifa ya mashtaka (NPS).
Wadau wengine ni Ofisi ya wakili Mkuu wa Serikali, (SG), Mawakili wa kujitegemea, (TLS), Asasi za msaada wa kisheria,TAKUKURU,TCCIA,TWCC,NIDA,Uhamiaji ,Polisi, ,Magereza Jeshibla Zimamoto na Uokoaji, Ustawi wa Jamii, Urekebishaji Tabia, Shirika la Bima la Taifa, (NIC) na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).
Jaji huyo amesema kwamba kutokana na mabadiliko ya kisayansi, Mahakama Kuu Kanda ya Musoma inatoa huduma za Mahakama popote mtu alipo (kiganjani) ambapo mhitaji hutapata huduma ya shauri lake alipo (kufungua na kusikilizwa) bila kwenda umbali mrefu.
"Mahakama ya Tanzania inajukumu la kikatiba la kutoa haki, lakini dhamira yetu sisi ni kutoa haki kwa wakati na kuwafanya watanzania waifikie huduma ya Mahakama kwa urahisi na bei nafuu.
Katika kutekeleza hilo kikatiba tumeweka mpango mkakati 2021/2024/2025 yenye malengo makuu matatu, lengo kubwa kabisa ni kutoa huduma ya haki kwa wakati na limejiweka kwenye utumishi ambapo matumizi ya teknolojia(TEHAMA) yanafanyika"ameongeza Mtulya.
Amewakumbusha wananchi kutumia fursa hiyo ya sheria na wafike uwanjani kupata huduma kwa kuwa mjumuiko wa taasisi na wadau wa kisheria hutoa elimu hiyo ya sheria mara moja kwa mwaka.
DIMA ONLINE imezungumza na baadhi ya wananchi, Mkazi Manispaa ya Musoma, Rabati Nyamwanga amesema kuwa kuna umuhimu sana kwa jamii kujua sheria kwani pasipokuwa na ufahamu wa kutosha haki hukosekana.
"Sisi raia kujua sheria ni jukumu letu hii itatusaidia kuzitetea haki zetu kwani ukiwa na uelewa wa sheria hutaonewa katika kupata haki yako", amesema Rabati.
Mjasiriamali mkazi wa Buhare, Joyce Chibwana ameipongeza mahakama na wadau kwa kuandaa maonyesho hayo kwani inasaidia kujua umuhimu wa sheria na kutenda haki.
Amesema wananchi wengi hawana uelewa wa kutosha kuhusu sheria na kwamba utoaji elimu utasaidia kujua haki zao na kuondoa unyanyasaji kwa jamii na hivyo kupunguza ukatili kwa jamii.
Ameongeza kuwa uelewa mdogo wa sheria unakwamisha upatikanaji wa haki na badala yake jamii imekuwa ikilaumu jambo bila kujua haki na wajibu kwa wote.
" Pia watu hawathubutu kutumia fursa za wazi za kujifunza kwa kutoona umuhimu wake mpaka pale changamoto inapotokea ndipo huangaika kupata ufumbuzi na kujikuta unakosa haki stahiki" amesema Joyce.
Kilangi Mgasa Mkazi wa mtaa wa Mtakuja A Kata ya Mwisenge Manispaa ya Musoma, Kilangi Mgasa amewasihi wananchi kufika uwanjani hapo na kuweza kupata elimu kwani wengi hawana uelewa wa kutosha kuhusu sheria na utambuzi wa haki.
"Watu wengi huamini dhamana ni kutoa fedha ilihali ni bure na haki kwa mhanga pindi unapokuwa umekamatwa au kushtakiwa hivyo unakuta unaingia kwenye utoaji wa rushwa kununua haki yako bila kujua" amesema Kilangi.
Ameipongeza Mahakama na wadau wa kisheria waliopo katika maonesho hayo kwa kuisaidia jamii kupata uelewa kwa urahisi pasipo gharama yoyote.
Post a Comment