RC MARA : WANANCHI ITUMIENI WIKI YA SHERIA KUPATA UWELEWA WA HAKI
Na Jovina Massano, Musoma
MKUU wa mkoa wa Mara Said Mtanda amewahimiza wananchi kutumia fursa kufika kwenye maonesho ya wiki ya sheria yanayoendelea viwanja vya Mukendo mjini Musoma ambayo kilele chake ni Februari 01, 2024.
Ameyasema hayo juzi wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya sheria yaliyoambatana na maandamano kutoka Mahakama ya Wilaya Musoma mpaka uwanja wa shule ya msingi Mukendo na kuhutubia wananchi na wadau wa sheria.
"Wananchi wafike kwa wingi kwenye maonesho ya wiki ya sheria mpate elimu ya uelewa juu ya haki zao na kuifahamu sheria ili kuondoa changamoto mbalimbali inayohusiana na sheria" amesema Mtanda.
Pia amewaasa watumishi wa sekta za umma na sekta binafsi kuwa waadilifu katika utekelezaji wa majukumu yao na kujiepusha na vitendo vya rushwa ili kuongeza ufanisi kiutendaji.
Amesema wakitenda kazi kwa uadilifu na kujiepusha na vitendo vya rushwa itasaidia kutenda haki na kuleta amani, utulivu na usalama katika jamii.
RC Mtanda amesema maendeleo na ustawi wa Taifa yanategemea uwepo wa amani na usalama lakini vyote hivyo vinategemewa zaidi na uwepo wa haki katika jamii.
Aidha katika kuyatekeleza hayo Mahakama kwa ushirikiano wao na wadau wa sheria utawasaidia wananchi kupata uelewa mpana wa sheria na kutambua haki zao.
"Nikumbushe mfumo jumuishi wa haki jinai unarahisisha upatikanaji wa haki kwa wakati hivyo wananchi watapata muda mwingi kufanya shughuli zao za kiuchumi na kijamii na kuleta ustawi wa Taifa kwa ujumla," amesema Mtanda.
Wakati huohuo, amempongeza Mtendaji wa Mahakama Kuu Tanzania Kanda ya Musoma Festo Chonya kwa usimamizi mzuri wa miundombinu ya Mahakama za mkoa wa Mara kwa kufanyiwa marekebisho.
Naye Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Musoma Fahamu Mtulya amesema kuwa kutokana na utoaji wa huduma ya elimu kumechangia muitikio mkubwa kwa wananchi katika kufungua mashauri kwa kipindi hiki tofauti na miaka ya nyuma.
Amesema kwa mwezi huu wa Januari Mahakama imepokea mashauri zaidi ya 60 yakiwemo mashauri jinai, mauaji, mashauri ya kawaida na mashauri ya ardhi jambo ambalo si la kawaida ukilinganisha na Januari mwa Mwaka 2023.
Post a Comment