WALIMU TUMBI WAJIVUNIA UFAULU WA WASICHANA WOTE MATOKEO YA KIDATO CHA NNE
Na Gustafu Haule, Pwani
WANAFUNZI wakike 34 waliofanya mtihani wa kumaliza kidato cha nne mwaka 2023 katika Shule ya Sekondari ya Wananchi Tumbi iliyopo Halmashauri ya Mji Kibaha wamempa heshima Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuonyesha maajabu makubwa ya ufaulu.
Maajabu hayo yametokea kwa mara ya kwanza katika shule ya Kata Sekondari Tumbi kwa kuhakikisha wanafunzi wote wakike waliofanya mtihani huo kufaulu kwa kiwango cha juu jambo ambalo limepelekea shule hiyo kufanya vizuri kwa mkoa wa Pwani.
Ufaulu wa wanafunzi hao wa kike ni heshima kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na Makamu wa Rais Dkt.Philipo Mpango ambaye mwaka jana alitoa motisha ya Tsh.Milioni 50 Kwa walimu wa shule hiyo baada ya kupokea ripoti ya matokeo mazuri ya ufaulu shuleni hapo.
Mkuu wa shule ya Sekondari ya Tumbi Fidelis Haule, akizungumza na waandishi wa habari shuleni hapo Januari, 29,2023 amesema kuwa shule yake inajivunia kuona wanafunzi wote wakike waliosoma shuleni hapo wamefaulu kwa kiwango cha juu jambo ambalo kwake ni faraja.
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Kata Tumbi Fidelis Haule akimkabidhi zawadi mwanafunzi Esther Kilamwegula baada ya kufaulu vizuri katika matokeo ya kidato cha nne ya mwaka 2023 na kuwa msichana kinara aliyefaulu kwa kiwango cha juu shuleni hapo
Haule amesema kuwa katika wanafunzi hao 34 waliopata daraja la kwanza (Division One 14) huku mmoja wao anayejulikana kwa jina la Esther Kilamwegula akiwa na pointi nane wakati waliopata daraja la pili (Division Two 16 )daraja la tatu (Division Three 3) na daraja la nne (Division Four 1).
"Ufaulu wa wanafunzi wa kike katika Shule yetu imefikia asilimia 99 kwakuwa wote wamepata ufaulu wa juu na sisi kama Shule tunajivunia kuwa na matokeo haya ambayo yameleta heshima kwa mama yetu Rais Samia Suluhu Hassan,"amesema Haule
Amesema kuwa siri ya wanafunzi hao kufaulu imetokana na nidhamu nzuri inayotekelezwa na walimu pamoja na wanafunzi wa kike ,motisha kwa walimu ,utambuzi kwa wanafunzi wanaofanya vizuri na hata kuweka malengo katika ufundishaji.
"Sisi hapa shuleni kwetu tuna utaratibu wa kila mwaka wa kutoa pongezi kwa walimu wanaofanya vizuri katika masomo yao na huwa tunawapa vyeti lakini kwa wanafunzi wanaofanya vizuri pia tunawapa vyeti mbele ya wenzao ili kuwapa moyo wa kusoma kwa bidii,"amesema Haule.
Ameishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kukarabati miundombinu ya shule ikiwemo kujenga maabara, kuboresha madarasa, kuongeza viti na vifaa vya ufundishaji na kikubwa walichopanga na kulipa fadhila kwa Rais kwa kuhakikisha kila mwanafunzi wakike anafaulu vizuri.
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Tumbi Mkoani Pwani wakimsilikiza Mkuu wa Shule hiyo Fidelis Haule wakati akiwaelezea juu ya matokeo ya kidato cha nne yalivyoleta tija Kwa wasichana waliosoma shuleni hapo na kupelekea wanafunzi wote wakike kufaulu.
"Rais mama Samia ametuletea kila kitu, yaani majengo mazuri, walimu wakutosha kwahiyo tunakila sababu ya kumshukuru na ndio maana tukasema lazima tuhakikishe tunalipa fadhila na tumefanikiwa kwani wasichana wote wamefaulu tena kwa kiwango cha juu,",amesema Haule
Mkuu huyo amesema mikakati ya shule yake ni kuongeza juhudi na maarifa katika ufundishaji ili kuhakikisha wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne wanakuwa na matokeo mazuri zaidi na kwamba wanachohitaji ni kuona wanafunzi wakike wanazidi kuwa vinara katika ufaulu ili kuendelea kuunga mkono jitihada za Rais Samia katika kuboresha mazingira ya elimu hapa nchini.
Kufuatia matokeo hayo, Haule ametoa zawadi ya pesa kwa mwanafunzi wa kike aliyefanya vizuri katika mtihani huo Esther Kilamwegula huku akiwataka wanafunzi wa kidato cha nne wanaotarajia kufanya mitihani yao mwaka huu kuongeza jitihada katika masomo ili waweze kufaulu vizuri zaidi.
Kwa upande wake Esther Kilamwegula ambaye kinara wa matokeo hayo ,amesema kuwa watu wanafikiri sio rahisi kwa shule za Kata kufaulisha kwa alama za juu lakini kwa shule ya Sekondari Tumbi imewezekana.
Mwanafunzi wakike Esther Kilamwegula kinara matokeo kidato cha nne Shule ya Sekondari Kata ya Tumbi Kibaha Pwani akitoa ushauri kwa wanafunzi wa Shule hiyo
Kilamwegula amesema kuwa kupata ufaulu huo kunategemea juhudi za mwanafunzi mwenyewe na ushirikiano mzuri wa walimu na kwamba Tumbi imewezekana kwakuwa ushirikiano wa walimu na wanafunzi ni mzuri.
Hatahivyo, Kilamwegula amewashauri wanafunzi wa sekondari Tumbi kuendeleza ushirikiano mzuri na walimu wao kwa kuyafuata yale wanayofundishwa pamoja na kuhakikisha wanasoma kwa bidii na kwamba wakifanya hivyo watafikia malengo ya kufaulu vizuri na kwa kiwango cha juu.
Post a Comment