TARURA : TUMESHAFANYA MAKISIO, SERIKALI IKITOA FEDHA LITAJENGWA DARAJA MTO TIGHITE
Na Dinna Maningo, Tarime
UKOSEFU wa Daraja katika Mto Tighite unaotenganisha Kata ya Matongo na Kata ya Kibasuka katika Halmashauri ya wilaya ya Tarime, mkoani Mara, umekuwa kero ya muda mrefu na usumbufu kwa wananchi na mifugo wakati wavukapo mto.
Wananchi na Viongozi katika Kata hizo matamanio yao ni kuona Serikali inawajengea daraja ili kurahisisha shughuli zao za kiuchumi na kijamii kutokana na kwamba msimu wa mvua maji hujaa mtoni na watu kushindwa kuvuka na wengine kustisha safari huku baadhi ya watu wakipoteza maisha kwa kusombwa na maji.
Ukosefu wa Daraja mto Tighite unawalazimu baadhi ya wananchi kulipa Tsh. 1000 ili kuvuka daraja la miti lililojengwa na mwananchi.
Wasio na fedha hulazimika kuvuka kwa kuogelea na kutembea majini vichwani wakiwa wamebeba mizigo huku ng'ombe ikishindwa kuvuka mto na hivyo kuvushwa kwa gharama ya sh.1000, kondoo na mbuzi sh. 500 na vijana wanaofahamu kuogelea.
Hali hiyo inailazimu DIMA Online kugonga hodi hadi ofisi ya Meneja Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini wilaya ya Tarime (TARURA) kufahamu nini mpango na mkakati wa serikali katika kutatua changamoto ya ukosefu wa daraja la kisasa mto Tighite.
Meneja Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini wilaya ya Tarime (TARURA), Charles Marwa anakili kuwepo kwa changamoto ya daraja na kusema kuwa tayari TARURA ilishafanya tathmini ya ujenzi ambapo makisio ya ujenzi wa daraja mto Tighite ni Tsh. Milioni 856.
" Pale pana changamoto, ni kweli napafahamu, kwa upande wa juu pale Nyamwaga sehemu ya kona nne tumejenga daraja na linatumika, kutoka pale hadi kufika Matongo ni km 20 ambapo mwananchi anayeishi Matongo hawezi kwenda kuvukia pale.
"Kwa hiyo pale Matongo kupitia mnadani panahitaji daraja. Sisi kama TARURA tumefika pale na tumejionea lakini pia tumefanya tathmini ya mahitaji ya ujenzi wa daraja mto Tighite na tayari makisio yalishawasilishwa serikalini kwa ajili ya kuombewa fedha za ujenzi wa daraja " anasema Mhandisi Charles.
Mhandisi Charles anasema mto Tighite panahitajika daraja lenye urefu wa mita 15-19 lakini pia urefu kwa maana ya kina cha takribani mita 4.5 hadi mita 5, na ni daraja ambalo litakuwa na njia mbili.
"Njia mbili kwa maana kwamba magari yatapishana upana wa mita 7 zikiwemo na njia za watembea kwa miguu. Likijengwa litarahisisha shughuli za kijamii pamoja na shughuli za kiuchumi na litawapunguzia mzunguko wananchi wa Nyamongo na Kibasuka anasema" Mhandisi Marwa.
"Daraja likijengwa litarahisisha shughuli za kijamii na kiuchumi ukizingatia Nyamongo kuna shughuli za uchimbaji wa madini ambazo zinahitaji mawasiliano.
"Kwa upande wa Kibasuka kuna shule, mashamba na huduma za kijamii, na upande wa Matongo kuna mnada, kwahiyo kuna uhitaji wa wananchi kutoka upande mmoja kwenda upande mwingine.
Anasema upande wa Kibasuka kwenda Mogabiri TARURA imefungua barabara kupitia mlima Mogabiri kuuunganisha mji wa Tarime mjini barabara yenye urefu wa km 6.5.
"Kwahiyo utaona km 6.5 za kutoka Tarime mjini mpaka Kibasuka ukiongeza na km.3 za kutoka Kibasuka kwenda Matongo ni km 9.5 umeshafika Nyamongo, tofauti na sasa hivi mtu akitoka Nyamongo kwenda Tarime mjini kupitia Nyamwaga ni zaidi ya km 42.
"Ukitoka Nyamwaga hadi Tarime mjini ni km 25, kutoka Nyamongo kwenda Nyamwaga ni takribani km 17. Umbali huo ni mkubwa, likiwekwa daraja pale Matongo mtu atafika haraka mjini Tarime umbali wa km 9.5.
"Kwahiyo daraja lile litakuwa na tija kubwa kama litajengwa. Tunaamini serikali italitengea fedha za ujenzi" anasema Meneja TARURA.
Mhandisi Charles anasema mbali na changamoto hiyo ya daraja serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imekuwa ikitoa fedha nyingi kujenga na kuboresha miundombinu ya barabara na madaraja.
Anasema kwa miaka mitatu ya hivi karibuni serikali imetoa fedha za matengenezo ya barabara yakiwemo madaraja na karavati katika halmashauri ya wilaya ya Tarime kutoka Tsh. Bilioni 1.09 hadi Bilioni 2.07 na katika halmashuri ya mji Tarime kutoka Tsh. Milioni 700 hadi Bilioni 2.5.
Anasema fedha hizo ni kutokana na tozo ya mafuta ambayo ni ongezeko la bajeti Tsh.100 kwa kila lita ya Dizeli na Petroli, fedha ya Jimbo la uchaguzi, na fedha kutoka mfuko wa barabara.
Anasema katika fedha hizo TARURA imewaondolea adha wananchi kwani imefanikiwa kujenga Vivuko, madaraja jumla 42 kwa baadhi ya Vijiji katika Halmashauri ya wilaya ya Tarime likiwemo daraja la Kebweye , Rosana na Nyarwana.
Tazama Video Mto Tighite unavyotesa wananchi mifugo
Post a Comment