HEADER AD

HEADER AD

TAKUKURU KAGERA : WAANDISHI WA HABARI FICHUENI VITENDO VYA RUSHWA

 

Na Alodia Babara, Bukoba

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), mkoa wa Kagera imewasihi waandishi wa habari mkoani humo kutoa ushirikiano kwa taasisi hiyo katika kuelimisha jamii na kufichua vitendo vya rushwa kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.

Mkuu wa TAKUKURU Pilly Mwakasege ameyasema hayo Januari 30, mwaka huu wakati akifungua mafunzo ya siku moja yaliyotolewa na taasisi hiyo kwa waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali mkoani Kagera.

    Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Kagera Pilly Mwakasege akizungumza na waandishi wa habari mkoani humo katika mafunzo yaliyotolewa na taasisi hiyo.

Amesema kuwa wanawategemea waandishi wa habari kuwapa ushirikiano katika kuwapatia taarifa mbalimbali zinazohusu vitendo vya rushwa kwa sababu ni watu muhimu katika jamii na wanauwezo wa kufika kokote pia wanaaminiwa sana na jamii.

Amesema kuwa, vyombo vya habari vikitumika vizuri vitaleta mabadiliko kwa jamii kwani watapatikana  viongozi bora na si bora viongozi ambao watasimamia vizuri miradi ya maendeleo na kukemea viashiria vya rushwa.

Amewasisitiza waandishi wa habari kutumia kalamu zao vizuri kwa kuandika mema yaliyofanywa na Serikali kuliko kuitumia tofauti kwani itakuja kuleta athari za rushwa na akaomba kupitia semina hiyo ili wakawe mabalozi na watoe ushirikiano kwa taasisi hiyo.

Aidha amesema kupitia elimu ambayo itatolewa na TAKUKURU kupitia vyombo vya habari na kuwafikia wananchi itasaidia kujua kwamba  wanapaswa kuchagua kiongozi wa eneo lao ambaye anazitambua changamoto zilizopo kwa undani.



Amesema kiongozi wa eneo husika atasimamia vizuri maendeleo yao nakwamba viongozi watambue kuwa wanapopigiwa kula ile nafasi waliyoipata siyo eneo la kutafuta fulsa au mtaji bali ni sehemu ya kwenda kushirikiana na wananchi wao kuwaletea maendeleo.  

“Kiongozi anayetoa rushwa ni yule ambaye hajiamini na hakujiandaa kwa wananchi wake, mkoa wa Kagera tunataka uchaguzi utakapofanyika wachaguliwe viongozi wenye maadili mema watakaosimamia ipasavyo miradi ya maendeleo ya wananchi” amesema Mwakasege

Kwa upande wake  Mkuu wa Dawati la Elimu kwa Umma TAKUKURU katika mkoa huo, Esther Mkokota amesema  rushwa ni adui wa haki na kuwa ina minya haki za watu kuchagua au kuchaguliwa, hivyo waandishi wa habari waelimishe watu juu ya kuacha taama ambayo ni kisababishi kikubwa cha rushwa.

        Esther Mkokota mkuu wa dawati la elimu kwa umma takukuru mkoa wa Kagera akitoa elimu kwa waandishi wa habari mkoani Kagera

Amesema kuwa kuna watu wanapowaona wenzao wana mali wanazitamani mali hizo bila kujiuliza mali hizo walizipata kwa njia ipi na hivyo kusababisha wajihusishe na rushwa jambo ambalo litasababisha mtu kama huyo kuchukuliwa hatua za kisheria.

Mkokota ameeleza kuwa, jamii ijue kuwa rushwa ni jia ya mkato ambayo inatumika kufikia lengo na endapo watachagua viongozi kwa kupewa rushwa wajue watakuwa wamepata viongozi wasiokuwa na sifa, rushwa inazorotesha maendeleo ya nchi na miradi inajengwa chini ya kiwango kutokana na kusimamiwa na kiongozi asiye na maadili mema.

Ameongeza kusema kuwa, wataendelea kutoa elimu kwa wananchi ili wachague viongozi bora wenye maadili watakaosimamia miradi ya maendeleo

No comments