UKOSEFU DARAJA MTO TIGHITE MKUKI UNAOCHOMA WANANCHI, MIFUGO NYAMONGO - KIBASUKA
>>Wavuka daraja la miti kwa kulipa 1000
>>Shughuli za wananchi zakwama, Vifo
>>Mifugo yahofia kuvuka mto yavuka kwa kuchapwa viboko na kupondwa mawe.
Na Dinna Maningo, Tarime
UKOSEFU wa Vivuko, Madaraja katika Vijito na Mito, ni moja ya changamoto kubwa inayowatesa na kuwakera wananchi na kuwapa usumbufu wanapotumia barabara au njia wakati wanapoenda katika majukumu yao kupata huduma za kijamii na shughuli za kiuchumi.
Mto Tighite unaotenganisha Kata ya Matongo-Nyamongo na Kata ya Kibasuka katika Halmashauri ya wilaya ya Tarime, mkoani Mara, umekuwa kero na usumbufu wakati wa msimu wa mvua.
Mto TighiteMsimu wa mvua nyingi mto hujaa maji na hivyo kusababisha adha kwa wananchi wanaovuka mto kwenda mnadani kupeleka bidhaa mbalimbali ikiwemo biashara ya mifugo na shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Naianza safari hadi Kitongoji cha Nyabibago kijiji cha Matongo kuliko na mnada ambao ufanyika siku ya jumatatu ya kila wiki.
Watu kutoka maeneo mbalimbali hufika kuuza na kununua bidhaa pamoja na mifugo, wengine kwenda katika shughuli mbalimbaji Nyamongo na Kata ya Kibasuka.
Mnada wa mifugo na bidhaa mbalimbali uliopo Kijiji cha MatongoLengo la kufika katika mnada huo ni kufahamu ni kwa namna gani wananchi wanavyopata adha kuvuka mto Tighite lakini pia namna mifugo inavyopata shida kuvuka mto pindi inapopelekwa kuuzwa mnadani.
Napiga kambi kwa saa kadhaa kuona yanayojiri mto Tighite, ama kweli wahenga wanasema kwamba pangu pakavu tia mchuzi, wananchi wa Kata ya Matongo na Kibasuka wanahitaji msaada wa daraja la kisasa.
Katika mto huo kuna daraja la miti lililojengwa na mwananchi ambaye hutoza watu fedha sh. 1,000 pindi mtu anapotaka kupita darajani. Anatumia changamoto hiyo kama fursa ya kujipatia kipato.
Daraja la miti mto TighiteNazungumza na baadhi ya wananchi wanaovuka mto huo kufahamu ni kwa namna gani mto Tighite unavyowapa adha na karaha.
Baadhi ya wananchi wanaeleza kutokuwa na uwezo wa kifedha kuwawezesha kulipa sh. 1000 ili wavuke katika daraja hilo pindi wanapoenda kutekeleza shughuli zao za kiuchumi.
Rehema Maulidi mkazi wa Itandora kijiji cha Nyakunguru anasema msimu wa mvua wazee na watoto hushindwa kuvuka mto kwenda mnadani kijiji cha Matongo wanapokosa sh. 1000 kuwawezesha kuvuka katika daraja la miti.
"Niliolewa huku Itandora nimekuja hapa mnadani kununua vitu, huwa tunapata shida sana mvua ikiwa nyingi inabidi tuvuke daraja la miti kwa kulipa sh. 1,000, ukiwa hauna unatembea majini tena ukiwa umebeba mizigo kichwani, wasioweza hawaendelei na safari.
Rehema anasema kwamba serikali ikiwajengea daraja zuri kila mtu atapita kwa uhuru, watoto watapita na watu wenye umri mkubwa watapita kwenda mnadani na kwenye shughuli zingine za kiuchumi na kwamba hawatavuka mto kwa kutembea na mizigo kichwani.
Katika daraja hilo la miti mwananchi anapolipa sh. 1000 ili kuvuka darajani kijana anayetoza fedha humpaka rangi katika kidole kisha huruhusiwa kuvuka darajani.
Mwananchi akipakwa rangi kidoleni baada ya kulipa sh. 1000 ili kuvuka mto katika daraja la miti.Hufanya hivyo ili kumsaidia aliyelipa fedha kwa siku hiyo asiweze kutozwa tena fedha pindi harudipo kutoka kwenye shughuli zake, wasio na fedha hukataliwa kuvuka darajani.
Justine Stephano anasema baada ya baba yake kuona watu wakiteseka kuvuka mto akaona bora awasaidie, akawatengenezea daraja la miti ili watu wapate unafuu.
"Mto ukijaa maji tunakuja hapa darajani mimi na kaka yangu kukusanya fedha, mtu akifika kuvuka kupitia daraja letu analipa sh.1000 anaenda kwenye shughuli zake akirudi anapita bila kulipa tena.
" Huwa tunawawekea alama ya wino wa makapeni kwenye kidole ili tusiwachanganye kati ya waliolipa na ambao hawajalipa" anasema Justine.
John Mwita ni mkazi wa Kijiji cha Nyarwana Kata ya Kibasuka anasema mto Tighite umekuwa kero kwa muda mrefu na kukatisha shughuli zao, wakati wa msimu wa mvua maji hujaa mtoni na kusababisha maafa.
John Mwita ni mkazi wa Kijiji cha Nyarwana Kata ya Kibasuka"Huu mto unatutesa sana maji yakijaa watu wanalazimika kuogelea kuvuka kwenda mnada wa Matongo na shughuli zingine kule Nyangoto, wengine hushindwa kuogelea na kusombwa na maji, wapo wanaookolewa na wengine wamepoteza maisha wakati wakijaribu kuvuka mto.
"Tunaiomba Serikali yetu itujengee daraja na barabara kutoka hapa darajani kupita Nyarwana iungane na ile iliyotengenezwa inayopita Mogabiri kwenda Tarime mjini.
" Changamoto hii ni ya miaka yote kwa wale wasioweza kuvuka mto hukatisha safari na kurudi majumbani hadi siku maji yatakapopungua" anasema John.
Mifugo yahofia kuvuka mto
Ukosefu wa daraja umekuwa kero na usumbufu kwa wafugaji na mifugo kwani nikiwa katika mto huo wafugaji wanaonekana wakihangaika kuvusha ng'ombe, kondoo na mbuzi.
Ng'ombe wakivuka mtoNg'ombe huingia ndani ya maji ili kuvuka mto, inapofika kwenye kina kirefu cha maji huogopa kwendelea na safari na kugeuza kurudi watokako.
Hali hiyo inawalazimu wenye mifugo kuivusha kwa kutumia nguvu na huiswaga majini kwa kuichapa viboko na kuiponda kwa mawe kuhakikisha inavuka mto, isiyoweza kuvuka bila kupata usaodizi husombwa na maji na kufa.
Wafugaji na vijana wakimlazimisha ng'ombe kuvuka mto kwa kumtupia mawe baada ya ng'ombe huyo kugoma kuvukaWafugaji wenye pesa inawabidi kuvushiwa mifugo yao na vijana wenye uwezo wa kuogelea majini kwa kulipa sh.1000 kwa kila mwenye ng'ombe na sh.500 kwa mbuzi na kondoo .
Mhere Mwita ni mfugaji mkazi wa Kata ya Kibasuka anaeleza adha wanayoipata, "Tuna shida sana wakati wa mvua tunateseka kuvuka mto, ng'ombe wanahangaika sana wanaogopa kuvuka na wengine maji yakiwazidi wanasombwa na maji na kufa.
Mhere Mwita ni mfugaji mkazi wa Kata ya Kibasuka"Tunaiomba Serikali itujengee daraja bora, itusaidie wananchi tunaovuka mto kwenda Kata ya Matongo. Serikali ituonee huruma hata sisi tuna haki ya kupita juu ya daraja lililojengwa kisasa kama ilivyo kwenye maeneo mengine" anasema Mhere.
Petro Maginga mkazi wa kijiji cha Nyarwana anasema " Tunapata shida sana na huu mto, tunaleta mifugo ili tuuze tununue chakula lakini maji yanakuwa mengi tunashindwa kuvuka na inakuwa shida kuvuka na chakula ukiwa umebeba kichwani au begani.
"Serikali iangalie hili jambo hatuna raha tunateseka, huu mto Tighite unatusumbua sana, nguo zinalowana unaenda mnadani nguo zikiwa zimelowa maji hadi tunaona aibu kuchangamana na watu tunaomba Rais Samia mama yetu angalia hii kero inatutesa.
Zakaria Msuma mkazi wa kijiji cha Nyakunguru anasema mifugo hupoteza maisha pindi inapovuka mto na hivyo kuwasababishia hasara.
Daniel Asheri mkazi wa kijiji cha Nyarwana anaiomba serikali kuwajengea daraja kwani kila wanapopeleka mifugo yao mnadani hutozwa sh. 5,000 pesa ya ushuru wa ng'ombe, sh. 3,000 ushuru wa Kondoo na Mbuzi.
Daniel Asheri mkazi wa kijiji cha NyarwanaKukosekana kwa daraja la kuunganisha Kata ya Matongo na Kata ya Kibasuka imekuwa ni fursa kwa vijana wadogo. Baadhi ya watoto hushindwa kwenda shule na kufanya vibarua vya kuvusha mifugo katika mto huo hadi ng'ambo ya mto.
Ujipatia ujira wa sh. 1000 wanapovusha ng'ombe za kila mmoja na sh. 500 wanapovusha mbuzi au kondoo.
Vijana wadogo wakivusha ng'ombe kwenda ng'ambo ya mto, malipo ni sh.1000 kwa kila mwenye mifugoNazungumza na mtoto mmoja aitwae Jafari Hussein mkazi wa Kitongoji cha Mwara, Kijiji cha Nyarwana anaeleza jinsi mto Tigite unavyowanufaisha kifedha pindi maji yanapojaa.
" Mto ukijaa maji huwa tunakuja hapa kutafuta riziki kuvusha watu na mifugo. mimi na wenzangu tunajua kuogelea kwasababu miaka yote tunautumia huu mto na tunaishi nao jirani. watu wakipita kwenda mnadani sisi ndiyo tunavusha mifugo yao wao wanapita darajani wengine wanaogelea.
"Ukivusha mifugo ya mtu anakulipa sh. 1000 unamvushia ng'ombe zake awe mmoja au wengi gharama ni sh.1000 na mbuzi ni sh.500 kwa siku za mnada tunavusha mifugo mingi na tunawavusha watu wale wasiokuwa na pesa, tunaweza kukusanya zaidi ya elfu 30,000 kwa siku.
Jafari anasema kuwa, pesa hizo huwasaidia kununua nguo na zingine huwapelekea wazazi wao kununua mboga na chakula na zingine kula shuleni.
Vijana wadogo wakivusha kondoo aliyeshindwa kuvuka mto kwenda ng'ambo ya mto, malipo ni sh.500 kwa kila mwenye mifugo mifugo ya mbuzi na kondo.Anasema kuwa hata kama wanapata pesa bado wanahitaji daraja la kisasa kwani wapo wanaowalipa fedha na wakati mwingine hudhulumiwa fedha pindi wanapovusha mifugo ya watu.
Mbali na vyanzo mbalimbali vya mapato vilivyopo Kata ya Matongo inayopakana na Mto Tighite ina chanzo kikubwa cha Mapato cha Mgodi wa Dhahabu wa North Mara Barrick unaoingizia serikali kuu, halmashauri ya wilaya ya Tarime mapato ya mabilioni ya fedha zikiwemo fedha za Uwajibikaji wa Makampuni kwa Jamii (CSR) na Mrabaha.
Waswahili wanasema kwamba Kitanda usichokilalia hujui kunguni wake, shida inayompata mwenzio huwezi kujua tabu yake maana haijakufikia wewe.
........Itaendelea
Post a Comment