HEADER AD

HEADER AD

BARAZA LA ARDHI NA NYUMBA TARIME LINAHUDUMIA WILAYA MBILI LIKIWA NA WATUMISHI WAWILI

Na Dinna Maningo, Tarime

UKOSEFU wa Watumishi katika Baraza la Ardhi na Nyumba wilaya ya Tarime mkoani Mara, unasababisha ucheleweshaji wa utatuzi wa mashauri ya wananchi kwa wakati.

Ucheleweshaji huo unatokana na baraza kuwa na watumishi wawili huku Mwenyekiti wa baraza hilo akihudumia wilaya mbili ya Tarime na Rorya.

Akizungumza na DIMA Online wakati wa kilele cha siku ya sheria nchini inayoadhimishwa kila Februari, 01 ya kila mwaka, Mwenyekiti wa baraza la Ardhi na Nyumba wilaya ya Tarime Mahelele Musa Sukumba, amesema baraza linakabiliwa na uhaba wa watumishi  pamoja na ukosefu wa gari la ofisi.

       Mwenyekiti wa baraza la Ardhi na Nyumba wilaya ya Tarime Mahelele Musa Sukumba

" Baraza tuna changamoto tunazokumbana nazo ambazo ni wingi wa mashauri ukilinganisha na watumishi. Baraza lina watumishi wawili walioajiriwa ambao ni mwenyekiti mmoja na karani pamoja na mchapaji ambaye ni wa mkataba.

"Baraza la wilaya linatakiwa liwe na angalau Wenyeviti wawili, baraza linahudumia wilaya mbili ya Tarime na Rorya, hii inapelekea ucheleweshaji wa kusikilizwa mashauri kwa wakati" amesema.

Mwenyekiti huyo amesema kuwa akienda likizo siku 28 kazi zote husimama na kwamba ukosefu wa watumishi unawapa wananchi kero na usumbufu.

 " Nikienda likizo kazi zote zinasimama wateja wakifika wanapigwa tarehe hadi Mwenyekiti atakapotoka likizo hii inaleta mgogoro na kero kwa wananchi ikizingatiwa wengine wanatoka mbali wanagharamika usafiri" amesema Mahelele.

" Rorya haina baraza la wilaya wananchi wanalazimika kuja Tarime kupata huduma, baraza linaanza saa mbili asubuhi, ili mtu wa Rorya awahi kusikiliza  shauri lake analazimika kuondoka kuja kulala Tarime, wengine hawana pesa za kulala gesti.

Ameongeza kusema " Akichelewa kufika anakuta shauri lake limeshasikilizwa na wakati mwingine asipoonekana shauri lake linafutwa, hii inatupa shida wananchi huona wanaonewa " amesema Mahelele.

Mwenyekiti huyo amesema baraza halina gari la usafiri tangu lianzishwe 2007, Mwenyekiti wa baraza akitaka kwenda kukagua eneo lenye mgogoro analazimika kutumia gharama zake au wenye mashauri kuchangia fedha za usafiri.

Akizungumzia idadi ya mashauri yaliyokamilika na yanayoendelea kusikilizwa kwa kipindi cha Januari hadi Desemba, 31, 2023 amesema wilaya ya Rorya inaongoza kwa kuwa na mashauri mengi yapatayo 256 ikilinganishwa na Tarime yenye mashauri 170.

" Kwa kipindi cha mwaka mmoja Baraza limemaliza mashauri 440 , mashauri yaliyopo barazani yanayoendelea kusikilizwa ni 426 ambapo mashauri 256 yanatoka wilaya ya Rorya na mashauri 170 yanatoka Tarime" amesema.

Amesema idadi kubwa Rorya inatokana na wananchi kujua umuhimu wa kufungua mashauri kwenye baraza kuliko kujichukulia sheria mkononi.

Ameongeza kuwa wilaya ya Tarime ina idadi ndogo kwakuwa ikitokea migogoro ya ardhi baadhi ya watu hujichukulia sheria mkononi na kufanya maamuzi badala ya kuyapeleka kwenye baraza ili yashughulikiwe kisheria.

Joseph Onyango mkazi wa Shirati wilayani Rorya aliiomba Serikali kuanzisha baraza la ardhi na nyumba Rorya ili kuwasogezea huduma karibu na wananchi kwa kile alichosema kuwa ili wapate huduma wanalazimika kwenda Tarime.


No comments